Simba itaivaa Yanga katika mechi ya
Ligi Kuu Bara, kesho kwenye Uwanja wa Taifa. Awali vyanzo vilielezwa kuwa
Israel Mujuni Nkongo ndiye angechezesha mechi hiyo. Baada ya gazeti hili kuweka
wazi jambo hilo wiki iliyopita, inadaiwa wahusika wakabadilisha ratiba na
kumpanga Martin Saanya wa Morogoro.
Kitendo cha kumbadili Nkongo
kimezua malumbano makubwa hadi Simba kutishia kutaka kutocheza mechi hiyo ya
kesho kwa madai kuna mpango wa ‘kuwamaliza’.
Inaonekana Nkongo ameondolewa baada
ya Championi kujua kuhusu yeye na kuandika mapema suala la kwamba aliwahi kumpa
kadi nyekundu Haruna Niyonzima wa Yanga na kuzua zogo kubwa katika mechi ambayo
nusura ivunjike.
Lakini hakuna anayejua vituko
lukuki vya Saanya. Mwamuzi huyo mwembamba kwa umbo, ana mambo mengi ambayo
amewahi kuyafanya katika michezo ya Ligi Kuu Bara aliyochezesha na unaweza
kuita vituko au viburudisho.
Polisi Dodoma wamchapa makonde
Msimu uliopita alipata kipigo cha
nguvu mara baada ya kuchezesha mechi ya Polisi Dodoma dhidi ya Azam kwenye
Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
Ilielezwa ‘aliibeba’ Azam na
kusababisha Polisi ifungwe bao 1-0, matokeo ambayo yalichangia timu hiyo ishuke
daraja. Waliomtembezea kichapo walifanya hivyo wakati alipokuwa kwenye vyumba
vya kubadilishia nguo uwanjani hapo.
Baadaye Shirikisho la Soka la
Tanzania (TFF) liliwafungia mechi tatu wachezaji waliompiga na faini ya
shilingi milioni moja kwa kila mchezaji aliyehusika ambapo walikuwa tisa.
Kocha Azam amlalamikia
Saanya ndiye aliyechezesha mechi ya
Ngao ya Hisani kati ya Azam na Simba mwanzoni mwa msimu huu, Simba ilishinda
mabao 3-2, lakini aliyekuwa Kocha wa Azam, Bunjak Boris ‘Bocca’ alilalamika
kuwa mwamuzi huyo ana uwezo mdogo wa kuchezesha soka.
Bocca alidai Saanya aliinyima Azam
penalti mbili na kuipa Simba penalti isiyo halali na kudai kuwa aliichangia
‘kuiua’ timu yake.
Ajichanganya kutoa kadi
Saanya alimpa kadi ya njano kiungo
wa Simba, Amri Kiemba, badala ya beki Said Nassor ‘Chollo’ katika mechi dhidi ya
Coastal Union miezi mwili iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa ambapo Simba
ilishinda kwa mabao 2-1.
Kiemba alimfuata na kumueleza kuwa
siyo yeye aliyecheza rafu bali ni Chollo aliyemkwatua Twaha Hussein lakini
Saanya hakutaka kumuelewa kabisaa!
Ugomvi wa Julio & Kiiza
Msimu uliopita Yanga ikiwa chini ya
Kosta Papic ilisafiri kwenda kucheza Mkwakwani Tanga, Saanya ndiye alikuwa
kati.
Mechi ilikuwa na upinzani mkubwa,
wakati fulani Kocha wa Coastal Union, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, ambaye sasa ni
kocha msaidizi wa Simba alizozana na wachezaji wa Yanga, Hamis Kiiza na Kiggi
Makasi.
Saanya alilaumiwa kwa kupoteza
muda, kwani badala ya kutumia filimbi, bila ya kujali ana mwili mdogo, alikuwa
akilazimisha kuingia katikati ya Julio na Kiiza au Kiggi huku akitumia muda
mwingi kuzungumza.
Yanga ilishinda bao 1-0
lililofungwa na Kiiza ambaye alikwenda kushangilia kwenye benchi la Coastal huku
akionyesha ishara ya kumziba mdomo Julio. Baada ya mechi, Julio alilalamika kuwa
Saanya alichangia kuharibika kwa mchezo huo kwa kuwa aliona matendo mengi ya
wachezaji wa Yanga ambayo si ya kiungwana lakini hakuchukua uamuzi.
Coastal v Yanga tena
Pamoja na kwamba ndiye alichezesha
mechi kati ya Yanga na Coastal msimu uliopita, TFF ilimpa mechi ya timu hizo
mjini Tanga msimu huu tena! Safari hii, Yanga ilishinda kwa mabao 2-1 na
Coastal Union wakalalamika kwamba Saanya amekuwa akiwaua kila mechi hasa zile
wanazokutana na vijana hao wa Jangwani.
0 COMMENTS:
Post a Comment