Mwaka 2009
nilikuwa kati ya Watanzania waliokuwa katika msafara wa timu ya soka ya taifa,
Taifa Stars iliyokuwa inashiri michuano ya Kombe la Mataifa Afrika kwa
wachezaji wanaocheza timu za ligi za nyumbani maarufu kama Chan.
Michuano
ilipigwa Ivory Coast katika miji miwili ya Abidjan na Bouake na hakuna ubishi
kulikuwa na hofu kubwa kuhusiana na suala la usalama ingawa inaonekana kiasi
fulani mambo yalikwenda kimyakimya na hata nilipoeleza kuhusiana na hali hiyo,
kuna baadhi ya viongozi kutoka TFF wakati huo walinilaumu.
Kama
kawaida sikujali kwa kuwa nilichokuwa ninaandika ndicho kilikuwa kinatokea kwa
kuwa Abidjan kulikuwa na amani na ndiyo yalikuwa makao makuu ya serikali ya Rais
Laurent Gbagbo na mji wa Bouake kama Dar es Salaam na Singida, yalikuwa makao
makuu ya wapinzani chini Allassane Watalla.
Kwa kuwa
wapinzani walikuwa Bouake na serikali ya nchi hiyo ilitaka amani, basi kundi
moja lilipangwa Bouake. Stars ilifanikiwa kuingia katika hatua ya mtoano na
tukalazimika kusafiri hadi katika mji huo.
Hakukuwa na
amani kwa kuwa tulisafiri na wanajeshi ambao walikuwa na mafunzo ya hali ya juu
na silaha nzito kwenye gari. Pikipiki zaidi ya tatu, halafu tulikwenda mwendo
wa kasi, chini kabisa ilikuwa ni kilomita 150 kwa saa.
Yote hii
ilikuwa ni hofu ya usalama na timu haikulala Bouake, hii ni kuthibitisha
hakukuwa na amani na Stars ililazimika kufanya mazoezi zaidi ya kilomita 60 na
Mji Mkuu wa Yamoussoukro ambao ulionekana angalau ni salama na timu ndiyo ikawa
inakaa hapo.
Hofu wakati
wa safari ilikuwa kubwa sana, hakuna aliyekuwa ana asilimia mia kwamba
tungefika salama bila ya kushambuliwa kila tulipokuwa safarini ambacho ni kitu
kibaya sana.
Kitu cha
kushukuru kwamba tulirudi salama, kwani miaka kadhaa baadaye vita iliripuka na
Gbagbo akaondolewa madarakani kwa aibu kwa kukamatwa kama paka huku Watalla
aliyekuwa waziri mkuu wakati huo akichukua madaraka.
Wakati huo,
michuano hiyo ya Chan ilitumika kama sehemu ya kurejesha amani ya Ivory Coast,
lakini bado nasema kuwa Ivory Coast wakati huo tulikuwa tukichezea “sharubu za
Simba”. Ndiyo maana naona haitakuwa sahihi Simba, Yanga na Falcon kuinua mguu
hapa kwenda kucheza Sudan.
Tayari
Yanga na Tusker ya Kenya hadi tunakwenda mitamboni zilikuwa zimetangaza kujitoa
Kombe la Kagame, huenda nyingine zikaongezeka, lakini ukweli ni kwamba vichwa
vya wachezaji wa timu za Tanzania si kwa ajili ya kuweka mambo sawa Sudan.
Watu wa
Sudan wanatafuta amani, kweli ni kitu kizuri lakini si sahihi amani hiyo
kupatikana huku Watanziania wakiingia katika sehemu ambayo si salama. Hili
lazima liangaliwe kwa umakini.
Katibu Mkuu
wa Cecafa, Nicholas Musonye ameonyesha kutokuwa na hofu, sawa. Hofu yangu mimi
ni kwamba Musonye anachoangalia ni fedha zinazopatikana katika michuano hiyo na
si matatizo ambayo watayaopata Yanga, Simba na Falcon.
Mjadala huu
ni mzuri, lakini utakuwa mzuri zaidi kama Simba na Falcon nao watafuata nyayo
za Yanga kwa kuwa si vizuri kubahatisha mambo katika sehemu hatari kwa faida
ya wengine.
Kweli
Musonye na Cecafa wao wanafaidika, lakini hasara itakuwa kubwa kwa timu
zitakazoshiriki hasa kama yatatokea matatizo. Vizuri kukaa mbali kabla ya
hatari na Cecafa kama ilivyosema mashindano yataendelea tu, basi vema
yaendelee.
Atakayeziona
timu za Tanzania zimekuwa na uoga basi ni bora iwe hivyo kwa kuwa hatari ya
Darfur ni kubwa kuliko inavyochukuliwa kwa hali ya kawaida tu, usalama ni kitu
muhimu sana kwa Watanzania, bado serikali ya Sudan haina uhakika na hili
asilimia mia.
Stars
ilijiweka katika wakati mgumu, ilikuwa rehani kuwafaidika Ivory Coast. Safari
hii hapana kwa timu zetu, michuano hiyo ikifanyika sehemu yenye usalama,
zitashiriki tu.
0 COMMENTS:
Post a Comment