Na Saleh
Ally
NILIONA ujumbe kwenye ‘ukuta’ wa mtandao wa
kijamii wa Facebook wa Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe
akieleza namna analivyoshangazwa na rafiki yake mmoja ambaye alilaumu Taifa
Stars kufungwa na Morocco mabao 2-1 ikiwa ugenini.
Zitto
alieleza namna ambavyo alishangazwa na rafiki yake huyo na kumjibu kwamba Stars
imefungwa kimchezo na Wamorocco haohao walilala kwa mabao 3-1 wakiwa hapa
nyumbani, hivyo hakukuwa na geni Stars kufungwa ugenini.
Lakini
Zitto alisema angeandika makala katika gazeti la Raia Mwema kuhusiana na suala
hilo, nikaamua kulifuatilia na kutaka kujua. Kweli juzi nikasoma makama
aliyoandika ambayo alianza na kuwafafanulia watu ambao wamekuwa wakimuuliza
vipi anaonyesha kujikita katika michezo.
Naye akawa
majibu kadhaa akitolea mfano historia ya soka ya Hispania ikiwa ni pamoja na
sehemu kadhaa ambazo amani ilirejeshwa na mchezo wa soka baada ya mambo kubwa
mamgumu, alikuwa sahihi.
Kabla
sijatua katika hoja ya msingi, naongezea hapo kwamba Zitto ni mwanamichezo,
inawezekana alisahau kuwaambia alikuwa kati ya wagombe wa Chama cha Soka
Tanzania (Fat) mwanzoni mwa miaka ya 2000 lakini akashindwa.
Wakati huo
Zitto akiwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM) alinivutia sana na
kampeni zake, alikuwa mgombea kijana zaidi na kutokana na kuonyesha alikuwa na
malengo na mipango ya baadaye, nilijitolea kuwa mmoja wa waliojaribu kuona
anashinda, kwa kuwa niliamini angeweza kusaidia kupatikana kwa mabadiliko
katika soka ya Tanzania, lakini akashindwa.
Nataka
kusisitiza kwamba Zitto kweli ni mwanamichezo, ninaamini upande wa michezo
tulimpoteza kwa kuwa hakuwa na fedha ya kuhonga na inaonyesha wapiga kura wengi
wanafanya kila uchaguzi ni mtaji wao, huenda Zitto angesaidia mabadiliko kwa
kiasi kikubwa katika soka yetu ambayo kweli mashabiki wanaipenda lakini yenyewe
bado haijawapenda.
Kilichonigusa
katika makala ya Zitto ni kuhusiana na pale alipoeleza kuwa alilazimika
kupambana na kiongozi mmoja wa Shirikisho la Soka la Morocco ambaye alikuwa
akilazimisha wachezaji wa Stars waingie katika chumba ambacho kilikuwa
kimepuliziwa dawa ya kuwamaliza nguvu.
Zitto
aliamua kupambana na kiongozi huyo kwa kuwa alijua iwapo wachezaji wa Taifa
Stars wataingia katika vyumba hivyo basi kutakuwa na tatizo kubwa na madhara
kwa timu yetu.
Huo ndiyo
uzalendo halisi, kwani Watanzania wengi sana hawapambani kwa ajili ya Taifa
Stars na badala yake wanapambana dhidi ya Taifa Stars.
Hii imekuwa
ni kawaida kaida kabisa, hata kama ukienda katika mechi kwenye Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam wakati Stars inacheza utashangazwa sana na hali ya mashabiki
wengi.
Mashabiki
hao wamekuwa wakitumia muda wao mwingi sana kulaumu kila kinachofanywa na
wachezaji au kocha pale uwanjani. Lakini ukiangalia hata ushangiliaji wao
unakuwa chini sana.
Muda mwingi
wanazungumza kulaumu tu, hata matukio ya uwanjani hawayaoni vizuri na kila
mmoja anataka kuonyesha yeye anajua zaidi ikiwezekana hata kuliko kocha, kitu
ambacho si sahihi na wala si msaada kwa timu yetu ya taifa.
Nasema
hivyo nikichukulia mfano wa Stars kupoteza mechi hiyo dhidi ya Morocco tena kwa
mabao 2-1, wako ambao wamekuwa wakilalama mfululizo katika mitandao ya kijamii
na wengine wakituma ujumbe wa maoni katika gazeti hili pia wakitoa lawama zao.
Wako
wanaamini Stars ilistahili kushinda hivyo walichofanya ni uzembe, lakini wengine
wanalaumu Kocha Kim Poulsen kumtoa Thomas Ulimwengu. Kwangu naona ni kama
kichekesho kwa kuwa Poulsen ndiye aliamua kumuanzisha mchezaji huyo.
Anajua kila
kinachotakiwa na utaona katika dakika alizokuwa ndani, Ulimwengu hakufanya kitu
kizuri kwani naye ni binadamu na siku zinatofautiana. Hivyo kama kocha kujaribu
njia nyingine ni jambo sahihi kwa kuwa kila kitu kinatakiwa haraka maana ni
dakika 90 tu za mchezo.
Sidhani
kama lawama ndiyo dawa ya kuisaidia Stars, bado kuna mapambano mbele mfano
keshokutwa dhidi ya Ivory Coast. Lazima tukubali, uzalendo wa kuendelea
kuungana hata kunapokuwa na matatizo ndiyo muhimu.
Kuiona
Taifa Stars ni “bonge la timu” pale inaposhinda tu haitakuwa sawa, Morocco ni
timu kubwa na maarufu lakini tuliifunga. Inawezekana pia kuifunga Ivory Coast,
lakini si kwa kufanya lawama ndiyo msingi.
Kukosoa kwa
maana ya kujenga ni jambo zuri, lakini kushambulia au kulaumu kila wakati si
kitu bora kama njia ya kuisaidia Taifa Stars. Ni aibu kwa sisi Watanzania hasa
wapenda michezo kupambana dhidi ya timu yetu tena ikiwa vitani.
Watanzania
dhidi ya Taifa Stars ni sawa na Mtanzania kujishambulia mwenyewe. Kila mmoja
wetu anapaswa kujiuliza mara mbili kabla na baada ya mechi ya Stars ikiwa
vitani, alisaidia kitu gani au mchango wake ulikuwa ni upi na kiasi gani.
Kila la
kheri wanajeshi wa Tanzania kupitia michezo katika mechi ya keshokutwa, Ivory
Coast ni wagumu na wazoefu, lakini mnaweza kuwashangaza na wanafungika.
0 COMMENTS:
Post a Comment