Simba imeendelea na mikakati ya kukiimarisha kikosi chake ambapo
sasa imewasainisha nyota wengine wanne makinda.
Hatua hiyo ya Simba inakuwa ni muendelezo wa kukifanyia
marekebisho kikosi chake ambacho hakikufanya vizuri msimu uliopita baada ya
kushika nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu Bara.
Simba ambayo inaonyesha kuelekeza akili yake katika kusaka nyota
makinda, juzi iliwasainisha nyota waliokuwa na kikosi chao cha vijana, mabeki
Emily Mgeta na Omari Salum. Pia ilimsainisha nyota wa zamani wa Tanzania
Prisons, Sino Agustino ambaye ameonyesha kukubalika kwa mashabiki wa klabu hiyo
katika majaribio yaliyofanyika chini ya kocha Abdallah Kibadeni.
Wekundu pia wamemsainisha kiungo mwingine mshambuliaji kinda,
Marcel Kaheza.
Akizungumza na Championi
Jumatatu mara baada ya zoezi hilo, Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Simba,
Joseph Itang’are ‘Mzee Kinesi’ alisema kusainishwa kwa nyota hao kumetokana na
mapendekezo ya Kibadeni ambaye ameonyesha kuridhishwa na uwezo wa wachezaji
hao.
“Tumezingatia mapendekezo ya kocha, kati ya hawa wachezaji wote
unaowaona leo yeye (Kibadeni) ndiye aliyetaka tuwape mikataba, bado tunaendelea
na usajili kwa kuwa kuna nafasi kama ya mshambuliaji na beki wa kati. Tunaendelea
kutafuta nyota sahihi tunaowataka,” alisema Mzee Kinesi.
Awali, Simba iliwasainisha makinda wake wapatao 10 na Championi
Jumatatu lilikuwa la kwanza kuandika na kutoa picha zao.
0 COMMENTS:
Post a Comment