July 6, 2013


*Asisitiza, soka ya Tanzania ni sawa na kibarua cha Mhindi…
 Na Saleh Ally
SAKATA la kiungo nyota wa Simba, Amri Kiemba kutaka kujiunga na Yanga na baadaye kubaki katika klabu yake hiyo limekuwa ni gumzo la chinichini kwa kipindi kirefu sasa.

Taarifa za Kiemba kuwa katika hatua za mwisho kusaini Yanga zilienea kila sehemu na hata baadhi ya wadau wa Yanga kutangaza amesajili tayari, hali ambayo ilizua utata.

Pamoja na kwamba takribani mwezi sasa, bado kumekuwa na hamu kubwa kwa mashabiki wengi wa soka kutaka kujua kama kweli kulikuwa na tukio kama hilo au la.
 
KIEMBA NA SALEH ALLY
Championi Ijumaa liliamua kukata mzizi wa fitna na kumtafuta Kiemba ili aelezee kuhusiana na hali hiyo ya yeye kutakiwa na Yanga au zilikuwa ni taarifa zisizo rasmi.

Awali baadhi ya viongozi wa Yanga walilizungumzia suala hilo na kusema hawakuwahi kabisa kutaka kumsajili Kiemba kama ambavyo ilikuwa imeripotiwa!

Kiemba ni kati ya viungo nyota nchini, amewahi kuchezea timu mbalimbali na kufanya vizuri. Yanga, Moro United na Miembeni ni kati ya timu alizosukuma gozi akiwa katika kiungo.

Ingawa umri unamtupa mkono taratibu, lakini ni kati ya wachezaji gumzo kutokana na uwezo wake. Tayari timu za Israel na Morocco zimeonyesha nia ya kutaka kumsajili kutokana na uwezo wake.

Katika mahojiano na gazeti hili, Kiemba ambaye anasifika kwa kuzungumza moja kwa moja bila ya kupindisha maneno, anasema alikuwa tayari kwenda Yanga kwa kuwa katika soka anachoangalia zaidi ni maslahi yake.

Kiemba anathibitisha kweli alifanya mazungumzo na Yanga baada ya kumfuata na walikuwa wamefikia katika hatua ya mwisho kabisa baada ya yeye kukubali kusaini kuichezea timu hiyo kwa mara nyingine.

Championi: Labda ilikuwaje kuhusiana na Yanga?
Kiemba:  Walionyesha nia ya kutaka kunisajili, nami niliwasikiliza na kutaka kujua walichonacho, basi tutakaa ana kuzungumza.

SALEHJEMBE: Mazungumzo yenu yaliishia wapi?
Kiemba: Baada ya mazungumzo na kuwaeleza nilikuwa ninahitaji kiasi gani, basi wao walikwenda kujipanga halafu wakarudi na kuniambia walikuwa tayari kunipa dau ambalo nilikuwa nimetaka.


SALEHJEMBE: Sasa kipi kilikuzuia kusaini na kutua Jangwani tena?
Kiemba: Walipokuja nikiwa tayari kusaini kukajitokeza kitu kimoja ambacho kikasababisha mambo yote kukwama katika hatua za mwisho.

SALEHJEMBE: Kitu kipi?
Kiemba: Yanga walikuwa na fedha zao ambazo ningechukua na kusaini, tatizo likawa ni moja, mshahara. Walitaka kunipa mshahara ambao nilikuwa naupata Simba, kitu ambacho sikukubaliana nacho.

SALEHJEMBE: Kiasi gani labda?
Kiemba: Kweli siwezi kutaja, ila Yanga walisema wana kiwango chao cha wachezaji wa nyumbani wanacholipwa ambacho ni cha juu. Sasa mshahara wangu ulikuwa umefikia zaidi ya hapo na mimi waliotaka kunipa nilikuwa nalipwa Simba. Kama kweli ni suala la maslahi kusingekuwa na tofauti.

SALEHJEMBE: Sasa nini kikaendelea?
Kiemba: Nakumbuka ilikuwa Jumapili, nikaendelea kushikilia msimamo na kuwaambia mshahara niliokuwa nataka, wao wakakwama hapo na mimi nikaona basi.

SALEHJEMBE:Maana yake mngeelewana mshahara, basi ungesaini?
Kiemba: Hakika ingekuwa hivyo, kikubwa kwa sasa naangalia maslahi maana soka ya Tanzania haina tofauti na kibarua cha Mhindi.

Championi: Una maanisha nini?
SALEHJEMBE: Kama unafanya kazi kwa ‘Mhindi’, siku moja anaweza kuamka na kusema, “wewe, leo hakuna kazi, kwenda jumbani”. Siku hiyohiyo kibarua kikawa kimeisha. 

SALEHJEMBE:Sasa vipi ukaamua kusaini Simba na awali ulikuwa umeamua kusaini Yanga?
Kiemba: Nilikuwa nimemaliza Simba mkataba miezi miwili iliyopita na hawakuwa wamenifuata na walionekana hawako siriazi. Katika hali ya kawaida nilianza kujua wanaweza wasinitake tena au vinginevyo, kama nilivyokuambia soka ni sawa na kibarua cha Mhindi.

SALEHJEMBE: Sasa baada ya hapo Simba ikawaje?
Kiemba: Sijui walipata taarifa za Yanga, maana siku hiyohiyo usiku walianza kunipigia simu na Jumatatu wakanifuata na kunipa mkataba ambao niliwaomba waniachie ili niupitie na watu wangu wausome halafu watauijia, nikabaki nao.

SALEHJEMBE:Yanga walikuwa mmeishashindwana?
Kiemba: Hapana, huenda wangerudi, niliona hizo dalili, lakini baada ya kuusoma mkataba wa Simba na kuwapa watu wangu siku hiyo ya Jumatatu, nikawarudishia lakini wao ili kuonyesha wamepania na huenda hofu ya Yanga, wakaacha fedha kabisa zikalala mapokezi.

SALEHJEMBE:Mwisho ukaamua nini?
Kiemba: Jumanne ndiyo siku niliyosajili Simba, maana walirudi na mkataba wakiwa wamefanya marekebisho ambayo kwangu niliona si sahihi. Basi, tukafikia mwafaka na kusaini.

SALEHJEMBE: Yanga hawakurudi tena?
Kiemba: Nafikiri walisikia nimeishasaini Simba tena, hivyo hakuna aliyerudi tena.

SALEHJEMBE: Kwa hiyo tofauti ya mshahara waliotaka kukupa Yanga na wanaokulipa Simba ni kiasi gani?
Kiemba: Sitataja, ila mshahara wa Simba ni mzuri zaidi.

SALEHJEMBE:Sawa, ninashukuru sana kwa uwazi na ushirikiano, ninakutakia maandalizi mema katika mechi ya michuano ya Chan dhidi ya Uganda.
Kiemba: Nashukuru sana.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV