Na Saleh Ally
KIUNGO nyota wa Kenya, McDonald Mariga Wanyama hadi sasa ameweka
rekodi ya mchezaji kutoka Afrika Mashariki kucheza ligi kubwa mbili na michuano
mikubwa zaidi kwa klabu Ulaya.
Amecheza Italia ‘Serie A’ akiwa na Inter Milan na Parma, halafu Real
Sociedad ya Hispania ‘La Liga. Lakini kumbuka alitwaa ubingwa wa Ligi ya
Mabingwa Ulaya akiwa na Inter chini ya Jose Mourinho.
Mdogo wake, Victor Wanyama, anakipiga katika kikosi cha Celtic ya
Scotland. Tayari amekuwa gumzo kwani pamoja na klabu hiyo kumnunua kwa pauni
900,000 tu kutoka Ubelgiji, iliwaambia Man United na Arsenal kwamba inahitaji
pauni milioni 25 kumuachia.
Kweli Mariga anatokea katika familia ya mpira, maana baba yake, Noah Wanyama alikuwa winga
hatari wa AFC Leopards, wadogo zake wawili Thomas
na Sylvester wanacheza Sofapaka
na Sony Sugar
katika Ligi Kuu ya Kenya. Dada yao mdogo, Mercy ni nyota wa mpira wa kikapu.
Ukiona hivyo, maana yake Mariga na Wanyama wanatokea katika familia ya
wanamichezo hasa, ingawa mwisho wanachofanya wanaing’arisha nchi yao.
Kenya sasa ina wachezaji wa kiwango cha kina Mariga, wanaweza kucheza
timu moja na wale wa Manchester United, Arsenal, Real Madrid, Barcelona na
wanafundishwa na makocha hadi wenye hadhi ya Mourinho!
Tanzania haina mchezaji kabisa ambaye inaweza kujivunia. Awali
lilionekana ni tatizo la Afrika Mashariki lakini sasa limebaki na kuwa tatizo
Tanzania tu.
Uganda wana wachezaji zaidi ya 20 walio nje ya nchi yao, kati ya hao
wapo wanaocheza Ulaya na anayecheza Heart of Midlothian ya Scotland, huyo ni kiungo
David Obua.
Tanzania yuko nani, anacheza wapi na kwa sababu gani inakuwa vigumu?
Mtu gani ni tatizo au nchi yetu?
Mwaka 2002, Kenya iliifunga Kilimanjaro Stars katika fainali ya Kombe
la Chalenji na kubeba kombe mbele ya mashabiki kibao kwenye Uwanja wa CCM
Kirumba mjini Mwanza. Kinda Denis Oliech akafunga bao la tatu la ushindi,
matokeo yalikuwa 3-2.
Jiulize wachezaji wa Tanzania Bara waliocheza na Oliech wakati ule
wako wapi, vipi hata mmoja hakufanikiwa? Lakini Mariga alikuja nchini miaka
miwili iliyopita akiiongoza Harambee Stars ambayo ilipata sare ya bao 1-1 dhidi
ya Stars.
MFANO: ANGALIA WANYAMA AKIWA NYUMBANI KWAKE SCOTLAND..
Ukimuangalia uchezaji wake, halafu angalia uchezaji wa viungo wetu
wengi, bado utaona wapo wengi wenye uwezo kama wake au zaidi.
Nani anaumia kutaka kujua wapi tunakwama halafu aanzishe safari ya kutafuta
suluhisho zaidi ya ukimya?
Viongozi:
Matatizo yanaweza kuwa mengi sana, lakini uwezo wa viongozi pia ni
tatizo. Si wale wanaoangalia mbele au wanaokubali mafanikio kwa wengine.
Kwanza hawapo tayari kuzipatia klabu zao maendeleo na kuangalia mfumo
wa kukuza vijana. Pia wapo tayari kumuondoa mchezaji anayefanya majaribio au
kumzuia asiende ili acheze mechi ya Simba dhidi ya Yanga hata kama tayari
bingwa kapatikana.
Mfumo:
Mfumo ni tatizo, hauwaonyeshi wachezaji kwamba wanaweza kwenda mbali
zaidi ya kucheza Yanga au Simba ambako wengi wanaamini ndiyo ‘mwisho wa
mbingu’.
Bado hawajiamini, hata waliopata nafasi ya kwenda kufanya majaribio
UIaya na kufanikiwa, wanaona Simba na Yanga zinatosha au bora wakacheze
Uarabuni!
Wachezaji:
Hata wao ni tatizo, kwanza hawana wivu wa maendeleo na hawaumii na kufeli.
Asilimia kubwa bado wanaona soka kama sehemu ya kujifurahisha.
Asilimia kubwa hawana tamaa ya kuvuka kutoka walipo na kwenda mbali,
ajabu zaidi wengine wanasisitiza siyo kitu kibaya kwao. Inawezekana kwa kuwa
hakuna aliyelipia kipaji chake kwa Mwenyezi Mungu, hivyo haoni hasara yoyote.
Inawezekana kabisa hata kwa kuangalia, Mariga na Wanyama si wachezaji
bora kuliko wa kwetu, lakini tamaa ya mafanikio na kutaka kutimiza ndoto imewafikisha
walipo.
Ukiangalia kwa kina sababu ni nyingi sana. Mfano wa Mariga na Wanyama
unakuwa mzuri kwa kuwa Kenya hatuna tofauti nao na wakati mwingine ligi yetu ni
bora kuliko yao. Vipi wao wanafanikiwa nasi hakuna kitu!
Lazima kuwe na tabia ya kujipima, hasa kwa kuangalia jirani au mtu wa karibu
yako anavyofanikiwa. Basi tuumie na tuamini Tanzania ina wachezaji wa kulipwa wenye
uwezo wa kucheza katika nchi zilizofanikiwa kisoka, tujue hiyo ni sehemu ya
kuinua soka nchini. Tafakari..!!!












0 COMMENTS:
Post a Comment