Shirikisho la Soka Afrika (Caf)
limefanya mabadiliko ya mwamuzi wa mechi ya mchujo kusaka tiketi ya Fainali za
Afrika kwa Wachezaji wa Ligi ya Ndani (Chan) kati ya Tanzania, Taifa Stars na
Uganda, The Cranes, itakayochezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam.
Mwamuzi aliyeondolewa kutokana na
sababu za kiufundi ni Jean Claude Birumushahu aliyekuwa mwamuzi msaidizi namba
moja. Nafasi yake sasa inachukuliwa na Herve Kakunze pia kutoka Burundi.
CAF imemuondoa mwamuzi huyo baada ya
kufeli katika mtihani wa waamuzi (Cooper Test) kwa waamuzi wa Burundi
wanaotambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) uliofanyika
nchini humo siku tatu zilizopita.
Waamuzi hao na Kamishna wa mechi
hiyo Gebreyesus Tesfaye kutoka Eritrea wanatarajiwa kuwasili nchini kesho
(Julai 11 mwaka huu) kwa ndege za Kenya Airways na EgyptAir kwa muda tofauti.
Nayo Uganda Cranes inatarajiwa
kuwasili nchini kesho (Julai 11 mwaka huu) na itafikia hoteli ya Sapphire.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Uganda (FUFA) bado halijatuma taarifa rasmi juu ya
ujio wa timu hiyo.
Wakati huo huo, makocha wa Taifa
Stars, Kim Poulsen na wa Uganda, Milutin Micho pamoja na manahodha wao watakuwa
na mkutano na Waandishi wa Habari utakaofanyika keshokutwa (Julai 12 mwaka huu)
saa 5 asubuhi kwenye ofisi za TFF kuzungumzia mechi ya Jumamosi.







0 COMMENTS:
Post a Comment