Kiingilio cha chini katika mechi ya
mchujo ya Kombe la Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN) kati ya
Tanzania (Taifa Stars) na Uganda (The Cranes) itakayochezwa Jumamosi (Julai 13
mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ni sh. 5,000 kwa viti vya rangi
ya kijani.
Viti vya kijani katika uwanja huo
wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 60,000 viko 19,648. Kwa upande wa viti vya
rangi ya bluu ambavyo viko 17,045 kiingilio ni sh. 7,000. Kiingilio kwa viti
vya rangi ya chungwa ambavyo viko 11,897 ni sh. 10,000.
Viingilio vya daraja la juu ni kama
ifuatavyo; VIP C yenye watazamaji 4,060 ni sh. 15,000 wakati sh. 20,000 ni kwa
VIP B yenye watazamaji 4,160. VIP A yenye watazamaji 748 kiingilio chake ni sh.
30,000.
Mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya
mwisho kuwania tiketi ya kucheza fainali hizo zitakazofanyika mwakani nchini
Afrika itachezeshwa na mwamuzi Thierry Nkurunziza kutoka Burundi. Mechi ya
marudiano itachezwa jijini Kampala kati ya Julai 26 na 28 mwaka huu.
Tiketi kwa ajili ya mechi hiyo
itakayoanza saa 9 kamili alasiri zitaanza kuuzwa siku moja kabla ya mchezo
(Ijumaa) katika vituo vifuatavyo; Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Sokoni
Kariakoo, mgahawa wa Steers ulioko mtaa wa Ohio/Samora, Oilcom Ubungo, Kituo
cha Mafuta Buguruni, Dar Live Mbagala na BMM Barbershop iliyoko Sinza Madukani.
Katika vituo hivyo tiketi zitauzwa
katika magari maalumu. Magari hayo pia yatafanya mauzo ya tiketi uwanjani siku
ya mechi.
Tunapenda kuwakumbusha watazamaji
kutonunua tiketi mikononi mwa watu au katika maeneo yasiyohusika ili kuepuka
kununua tiketi bandia, hivyo kukosa fursa ya kushuhudia mechi hiyo.







0 COMMENTS:
Post a Comment