![]() |
| TENGA, KUSHOTO KWAKE NI ANGETILE OSIAH, KATIBU MKUU WA TFF |
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amesema hakuna hila yoyote katika marekebisho ya
Katiba kwa vile yametokana na maagizo ya Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa).
Akizungumza na Wahariri wa Michezo
kwenye ofisi za TFF, Dar es Salaam leo (Julai 9 mwaka huu), Rais Tenga
amewahakikishia wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Dharura kuwa dhamira ya marekebisho
hayo ni nzuri, kwani lengo ni kila mtu apate haki yake.
Amesema Mkutano huo utakaofanyika
Jumamosi (Julai 13 mwaka huu) utakuwa na ajenda moja tu ya kuingiza Kamati ya
Maadili, na Kamati ya Rufani ya Maadili katika Katiba ya TFF kama
ilivyoelekezwa na Fifa ili baadaye uanze mchakato wa uchaguzi.
“Katika kuunda Kamati ya Maadili
tumeangalia ile ile ya Fifa, tusitengeneze kitu kipya, yaondolewe yale
yanayotakiwa kuondolewa, na yaongezwe yale yanayotakiwa kuongozwa. Kwa sababu
tumeangalia mazingira kwa Tanzania ni tofauti na Ujerumani au nchi za sehemu
zingine,” amesema.
Rais Tenga amewataka wajumbe wafike
kwenye Mkutano wakiwa na mtazamo wa kujenga, kwani kuna maagizo ya Fifa ambayo
wanatakiwa kuyatekeleza ili wasonge mbele.
“Tutawaeleza kwanini hili limewekwa
na lile limeondolewa. Mpira unataka unit (kitu kimoja), ni mchezo wa kila mtu.
Baada ya hapa tunaanzisha mchakato wa uchaguzi. Watu wanaingia wakiwa wamoja,
wanatoa hoja wanasikilizwa. Wanahukumiwa kwa hoja,” amesema na kuongeza
utatolewa muda wa kutosha wajumbe ili wayaone na kuelewa marekebisho hayo.
Rais Tenga pia alizungumzia kipindi
hiki cha usajili na kutaka klabu ziwaachie wataalamu wa mpira wa miguu kwani
ndiyo wanaojua upungufu wa timu, hivyo wanaweza kusajili wachezaji sahihi.
Amesema tatizo kubwa la klabu za
Tanzania ni kuwa timu zao hazina uwezo wa kuhimili dakika 90, hivyo watu
wanapaswa pia kuzungumzia aina ya mazoezi ambayo timu zao zinafanya badala ya
kubakia kutaja tu majina ya wachezaji wanaotaka kusajiliwa.








0 COMMENTS:
Post a Comment