Timu mbili
nchini Kenya zimejitosa kumuwania kipa wa zamani wa Simba, Juma Kaseja ili
zimsajili kwa ajili ya msimu ujao.
Wakala wa
kuuza wachezaji nchini, John Ndumbaro amealiambia Championi Jumatatu kuwa, timu
hizo mbili zimemtaarifu kuwa zinataka kumsajili Kaseja kwa ajili ya msimu ujao.
“Kuna timu
ambazo nisingependa kuzitaja hadi hapo kutakapokuwa na makubaliano kwa kuwa ni
suala la Kaseja mwenyewe kukubali au la.
“Mimi
nafanya kazi na timu hizo katika masuala ya kuuza wachezaji, sasa zimenieleza
nia yao ya kumsajili Kaseja baada ya kusikia amemaliza mkataba wake na Simba na
hawajamuongezea.
“Nafikiri
mazungumzo yataanza hivi karibuni na kama kutakuwa na mafanikio, basi tunaweza
kutangaza ni timu zipi na mambo yamekuwaje. Kwa kifupi hapa ni suala la maslahi
na uamuzi wa mwenyewe Kaseja,” alisema Ndumbaro ambaye ni mdogo wa wakala
mwingine Damas Ndumbaro.
Kaseja sasa
yuko huru baada ya kumaliza mkataba na Simba ambayo imetangaza haitamuongezea
mkataba mpya na kumpa ruhusa ya kuendelea na ‘mishe’ zake.
Kaseja
alikuwa mapumzikoni nyumbani kwao Kigoma ambako pia amekuwa akiendelea na
mazoezi mepesi na vijana wengine mjini humo.
Wakala huyo
alisema ndani ya wiki moja anatarajia kuwa amejua uamuzi wa Kaseja na iwapo
atakuwa amekubali kujiunga na timu kati ya hizo mbili ambazo zinaendelea
kupambana katika Ligi Kuu Kenya.







0 COMMENTS:
Post a Comment