BUYINZA (KUSHOTO) WAKATI AKIKIPIGA KCCA KABLA YA KUTUA VIETNAM.. |
Simba imeonyesha imepania kurekebisha makosa
yaliyoisumbua msimu uliopita baada ya kumchukua beki mwingine Mganda kutoka
Vietnam kuja kujiunga na timu hiyo.
Beki huyo, Asuman Buyinza anatarajia
kutua nchini kesho na kuanza mazoezi na Simba chini ya Kocha Abdallah Kibadeni.
Habari za uhakika kutoka ndani ya
Simba zimeeleza Buyinza atakuwa katika kikosi cha Simba kwa wiki mbili akifanya
mazoezi na Kibadeni ndiye atatoa uamuzi.
Miaka miwili iliyopita, Buyinza
alikuwa beki tegemeo na nahodha wa KCCA ya Uganda kabla ya kujiunga na klabu
kubwa ya Vietnam ya Da Nanga kwa dau la dola 50,000.
“Kweli anakuja nchini na tayari
ameishatumiwa tiketi. Tumeelezwa ni beki mzuri na tumemfuatilia kwa muda,”
kilieleza chanzo.
“Lakini mfumo wa ufanyaji kazi wa Simba
kwa kipindi hiki ni kuliacha benchi la ufundi lifanye kazi yake, hivyo
tutamuachia kocha aamue baada ya kuiona kazi yake,” kilieleza chanzo cha
uhakika.
Simba ina beki mwingine Mganda, Samuel
Ssenkoomi ambaye anatokea URA ya nchini humo ingawa kutokuwa na kimo kirefu
imekuwa sababu inayowapa hofu mashabiki wa Simba.
Hata hivyo, Ssenkoomi ameonyesha
kujiamini kwamba anaijua kazi yake, lakini bado hajaonyesha cheche zake baada
ya kukumbana na mkasa wa kuumia, siku chache baada ya kutua nchini.
Msimu uliopita, Simba ilisumbuka sana
katika safu hiyo ya ulinzi na hasa beki wa kati hasa baada ya kuondoka kwa
Kelvin Yondani na kujiunga na Yanga.
Mchezaji mwingine ambaye pia ni Mganda
ambaye Simba inahaha kumpata ni Moses Oloya ambaye pia anakipiga katika timu ya
Xuan Thahn Sai Gon ya Vietman pia ingawa Yanga nayo imeanza kutia mkono
ikionyesha kuwa na ‘njaa; pia ya kumpata Oloya ingawa mambo yamekuwa
yakifanyika kwa siri kubwa.
0 COMMENTS:
Post a Comment