Kuuzwa kwa beki Shomari Kapombe kumekuwa
ni gumzo kubwa, lakini inaonekana mashabiki na wanachama wengi wa Simba
wamekuwa hawaelewi mambo yalivyokwenda.
Simba imeamua kumuachia Kapombe ajiunge
na klabu ya daraja la nne ya AS Cannes ya Ufaransa. Klabu hiyo haijapata lolote
katika kipindi hiki kwa kuwa klabu hiyo haijatoa hata senti. Hapo maswali
yanaanza kujitokeza.
Kwamba Simba itafaidika vipi, kabla ya
Kapombe kusaini mkataba na AS Cannes, ameongeza mkataba na Simba hadi mwaka
2016. Katika mkataba huo mpya beki huyo pia hajalipwa lolote na klabu hiyo ya
Msimbazi.
Hapo ndiyo mpango wa biashara ulipo,
kwamba Kapombe ameingia mkataba na Simba hadi 2016, lakini mkataba wake na AS
Cannes ni wa miaka miwili. Utakapofikia mwisho kama atakuwa hajauzwa, basi
atarejea Simba ambao watalazimika kumlipa ada ya mkataba wake huo alioongeza
ambao sasa hawajamlipa.
Lakini katika miaka miwili hiyo akiwa na
AS Cannes, kama atauzwa, basi asilimia 40 (mfano) ya mauzo itakwenda kwa Simba.
Yaani kama atauzwa mfano dola milioni moja, basi Simba itapata dola 400,000 (Sh
milioni 653).
Samba ilichoangalia ni biashara ya
baadaye, lakini inawezekana kabisa naweza kusema ni uzalendo wa hali ya juu
ambao ulikosekana hapo awali tena kwa kipindi kirefu sana. Leo, Kapombe ameweka
rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza wa Tanzania kucheza soka nchini Ufaransa.
Kwangu inanipa imani, kwamba Simba kwa
mara ya kwanza naweza kusema imeona mbali. Niliposikia suala hili limefanyika,
nikashangazwa kidogo kwa kuwa ni nadra kwa timu za Tanzania kukubaliana na hilo
kwa kuwa mara nyingi zinaangalia biashara ya leo tu bila ya kujali kesho mambo
yatakuwaje?
Kati ya watu niliowahoji ndani ya Simba
wakanieleza Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Pope na
Katibu Mkuu, Evodius Mtawala ni kati ya waliotoa ushawishi wa jambo hilo
kufanyika, wao walilenga maslahi kama Kapombe akiuzwa lakini pia kuanzisha
uhusiano wa kibishara kati yao na AS Cannes, pia timu nyingine za Ulaya.
Hili ni jambo lisilojali sana busara,
badala yake hesabu za biashara ya baadaye na muono wake unahitaji darubini,
yaani lazima wahusika waangalie mbali ili kuchukua uamuzi sahihi katika wakati
sahihi kama ambavyo wamefanya Simba.
Inawezekana kabisa Simba leo wasione
kama mambo yanawezekana, au walilofanya si jambo zuri, lakini siku itafika
wakaeleweka ingawa bado watakuwa wakitegemea juhudi na maarifa ya Kapombe kwa
kuwa akifanikiwa, basi walichokiratajia kutatokea.
Lakini asipofanikiwa, bado kwa mfumo wa
mkataba waliotengeneza watakuwa na nafasi ya kumrudisha mikononi mwao baada ya
miaka miwili na inawezekana atakuwa amekomaa zaidi kiumri, maana sasa ana miaka
21. Lakini pia atakuwa amejifunza mengi katika soka la Ufaransa na akirejea,
akawa msaada mkubwa kwa Simba kama askari aliyekuwa mafunzoni.
Simba wamefanya mambo mawili makubwa
kabisa, kwanza ilikuwa ni ujasiri wa kukubali Lapombe aondoke katika kikosi
chao, pili ni hesabu katika mkataba wao na mchezo huyo na umakini wa mkataba
waliotaka aingie beki huyo na AS Cannes.
Mimi sijapata bahati ya kuona mtaba hata
mmoja, lakini kama kila kitu kitakuwa kimewekwa kama nilivyoelezwa na kueleza
hapa. Maana yake Simba watakuwa wako katika mstari sahihi na huenda
hawatajilaumu.
Natamani kuona Kapombe anafanikiwa ili
uwe ushawishi kwa timu nyingine kukubali au kujenga tabia ya uthubutu,
nakumbuka awali kuna baadhi ya timu ikiwemo Simba zilikataa, katakata kuwaachia
wachezaji wao kwa mikopo. Simba imepiga hatua moja mbele.
Hii itakuwa changamoto ya ushawishi kwa
klabu nyingine, lakini ninaamini nyingi zitasubiri kuona Kapombe anafikia wapi.
Uamuzi mgumu, mara nyingi ni njia sahihi
ya kupiga hatua mbele.
Kuwa mwoga unaweza kuwa salama zaidi, lakini ukaendelea
kubaki ulipo milele. Simba wamechagua njia ya kwanza ambayo inaweza kuwa
mapinduzi katika biashara ya wachezaji barani Ulaya.
Tayari wachezaji wake wawili katika
kipindi cha miaka kumi wamecheza Ulaya, Henry Joseph aliyekuwa Kongsvinger IF
ya Norway na Haruna Moshi ‘Boban’ aliyekuwa Gefle IF ya Sweden.
Kwa Kapombe, mambo ni tofauti. AS Cannes
imewatoa nyota wengi kama Zinedine Zidane na Patrick Vieira na inajulikana kama
“soko la wachezaji” kutokana na uwezo wake wa kuzalisha vipaji. Kapombe
akikomaa, maana ya Simba kuchukua uamuzi huo, itaonekana. Kila la kheri.
0 COMMENTS:
Post a Comment