Na Saleh Ally
Beki wa Simba, Shomari Kapombe, jana alitarajia kuanza kuichezea
AS Cannes ya Ufaransa ambayo imekubali kumpa mkataba wa miaka miwili.
Habari za uhakika kutoka Ufaransa ambazo zimethibitishwa na wakala
wake, Dennis Kadito, zimeeleza kuwa, baada ya kujadiliana na AS Cannes, timu
hiyo imekubali kumpa Kapombe mkataba huo wa miaka miwili.
“Jamaa walikuwa na mjadala, unajua kabla ilibidi wajadili kwa kuwa
kulikuwa na wachezaji zaidi ya kumi ambao walikuwa wanahitaji kusajiliwa na
timu hiyo.
“Timu nyingi kubwa za Ulaya zimeifanya kama soko au sehemu ya
‘shopping’, huwa zinakwenda pale na kununua wachezaji. Hivyo baada ya kujadili,
kwanza wamemsainisha kiungo mmoja kutoka Senegal na Kapombe atakuwa mchezaji wa
pili.
“Ninachojua kuwa Kapombe atatumiwa mkataba, unajua alishaondoka
hapa Ufaransa na sasa yuko Uholanzi na wakala wake. Lakini AS Cannes watamtumia
mkataba leo (jana) naye atausoma kwa msaada wa wakala wake na kuusaini,”
kilieleza chanzo cha uhakika kutoka Ufaransa.
Salehjembe lilimtafuta wakala wake, Denis Kadito mmoja wa mawakala
vijana wanaofanya kazi zao kwa kujituma ambaye alisema: “Kweli wale jamaa
wametuma mkataba na utapitiwa kwanza kabla ya uamuzi mwingine, hivyo ninaona
acha tusubiri kwanza ili nizungumze kwa uhakika.
“Unajua Kapombe amerudi hapa Uholanzi, hivyo kama leo atasaini
basi ataondoka kesho kwenda Ufaransa kwa ajili ya kujiunga na timu yake hiyo
mpya. Acha tusubiri halafu ndiyo nitazungumza.”
Kama hiyo jana atakuwa amesaini mkataba, Kapombe ataungana na
wachezaji wengine kutoka Afrika ambao wanacheza katika timu hiyo, nao ni;
Paulin Voavy (Madagascar), Elias Uzamukunda (Rwanda), Biliaminou Tidjani
(Togo), Sylvain N'Diaye (Senegal) na Adama Soumare (Burundi).
Aidha, wakala huyo aliishukuru Simba kwa kuonyesha kuelewa
kuhusiana na suala la Kapombe ambaye atakuwa kati ya Watanzania wachache
wanaocheza Ulaya.
Kapombe alifanikiwa kufanya vizuri katika majaribio hayo na
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Pope akasema
wamekubaliana kumuachia kwa mkopo katika klabu hiyo ya daraja la nne.
Pamoja na kucheza daraja la chini, klabu hiyo ina jina kubwa na
iliporomoka kutokana na kuingia katika migogoro lakini kabla ilifanikiwa
kuwatoa wachezaji nyota kama Zinedine Zidane, Patrick Vieira, Gael Clichy na wengine kibao.
Isee babukubwa endelea kutupa feedback mzee big up
ReplyDelete