Katika siku za karibuni, kumekuwapo na mjadala kuhusiana na hatua ya klabu ya Yanga
kupinga udhamini wa Ligi Kuu ya Tanzania unaotarajiwa kufanywa na Azam Media.
Tumeona
ni vema tukatoa msimamo wetu wa pamoja kuhusiana na hatua hiyo ya wenzetu kwa
lengo la kuweka rekodi sawa.
Tunataraji
hatua hii ya vilabu hivi 13 itafunga mjadala huu na tungependa wana habari,
kama mtaamua kuuendeleza, basi muundeleze katika mrengo ambao wadau, yaani sisi
vilabu vinavyoshiriki mashindano hayo, zimeamua kuufuata.
Tunapenda
kukumbusha kwamba kwa muda mrefu, kilio cha vilabu vya Ligi Kuu ya Tanzania
vilikuwa ni ukosefu wa wadhamini na kwa bahati nzuri kuna dalili kwamba Mungu
ameanza kukisikia kilio hicho msimu huu.
Kwa faida
ya umma, tungependa kutoa takwimu za nchi jirani zinazotuzunguka. Kenya, kila
klabu hupata Sh milioni saba za Kenya (sawa na Sh milioni 125 za Kitanzania)
kwa mwaka -fedha ambazo zimeifanya ligi ya Kenya kuwa na uwiano na ushindani wa
kweli (fedha hizo ni mjumuisho wa gharama za matangazo ya televisheni na
udhamini wa bia ya Tusker).
Tanzania
leo tunajivunia kuwazidi Kenya kutokana na udhamini wa Azam ambapo kwa mwaka
huu, kila klabu itapata zaidi ya Sh milioni 170 (Jumla kutoka milioni 100 za
Azam na milioni 70 za Vodacom).
Hatuna
sababu ya kutaja viwango vya udhamini kwa nchi nyingine jirani kama Uganda,
Burundi, Rwanda, Zambia nk kwa vile zote zina udhamini wa chini kuliko Kenya.
SuperSport,
ambao wanaliliwa na baadhi yetu, udhamini wao kwa ligi ya Uganda ni dola
350,000 ambazo ni pungufu kulinganisha na dola milioni moja zilizotolewa na
Azam Media hapa nchini.
Ni imani
yetu kwamba udhamini huu utaifanya ligi ya Tanzania kuwa bora kuliko zote za
Afrika Mashariki. Hili litasaidia kutengeneza timu bora ya Taifa ya Tanzania.
Tungependa
kutoa ufafanuzi wa masuala machache ambayo yaliongelewa na wenzetu wa Yanga
kama sababu za kupinga udhamini huu.
BODI YA TPL
Kwa
mujibu wa Katiba za FIFA, CAF na TFF, Haki za Televisheni zipo chini ya FA ya
nchi husika. TFF iliamua kukasimu shughuli ya majadiliano kwa Kamati ya Ligi
ambayo ilishirikisha vilabu vyote 14, ikiwamo Yanga na wawakilishi wake
walihudhuria mchakato mzima hadi mwisho.
Hoja ya Yanga kuwa bodi haina
nguvu/Mamlaka kisheria kwa kuwa ni ya mpito inakosa mashiko kwa sababu kimsingi
ni TFF ndiyo iliyoingia mkataba kwa sababu ndiyo iliyopewa mrejesho na Kamati
ya Ligi kwamba mchakato umekwenda sawasawa.
Hoya ya kuwa Bodi ya TPL iliyoko sasa
hivi haina mjumbe hata mmoja aliyeteuliwa kutoka YANGA. Hili si kweli hata
kidogo. Mmoja wa wajumbe wa TPL ni Seif Ahmed almaarufu Seif Magari; ambaye
vyeo vyake ndani ya Yanga vinajulikana.
Kama alikuwa hahudhurii vikao vya TPL,
hilo ni suala la Wanayanga wenyewe kumuhoji kwanini alikuwa hahudhurii hivyo na
hivyo kuinyima klabu yake ushiriki katika mijadala muhimu kwa maslahi ya soka
hapa nchini.
Ifahamike pia kwamba TPL haikuhodhi
mchakato huu bali ilitoa fursa kwa vilabu vyote vya Ligi Kuu kushiriki ambapo
Yanga ilikuwa ikiwakilishwa na Makamu Mwenyekiti wake, Clement Sanga na Katibu
Mkuu, Lawrance Mwalusako.
Hii maana yake ni kwamba hoja kuwa
Yanga haikushirikishwa ni mfu.
Yanga walitumia neno UTARATIBU WA DUNIA
NZIMA wakisema eti hakuna mahala duniani ambapo kampuni yenye klabu inayocheza
ligi husika kupewa mkataba wa udhamini au urushwaji wa matangazo.
Inaonekana Yanga hawakufanya utafiti
kwani ligi ya Afrika ya kusini ina timu inayoitwa Super Sports United na
inarushwa na kituo cha TV chaSupersports.
Pia majirani zetu Kenya wana timu
inayoitwa Tusker FC huku ligi hiyo ikidhaminiwa na bia ya Tusker.
Tunawashauri Yanga kuwa ni vema kufanya
utafiti kabla ya kuibuka na hoja za namna hii ili kuepuka kuwapotosha wanachama
wao.
Yanga pia
katika hoja zao wamepinga utaratibu wa kugawana mapato sawa. Hoja hii ni ya
msingi na majadiliano yetu yalilitazama hili kwa kina lakini tukaona kwa
mazingira ya Tanzania na uchanga wa ligi yenyewe kwa sasa ni heri kugawana sawa
ili pesa kwa usawa ili itoke kwa wakati na kusaidia vilabu kujiendesha. Yanga
wanakosea wanaposema eti wao wanastahili kupewa zaidi kwa sababu ni klabu kubwa
na yenye mashabiki wengi kwa kuwa sababu hii haitumiki sehemu yoyote duniani.
Tuchukulie
mfano wa nchi ya England ambako ingawa Liverpool ina washabiki wengi kuliko
Manchester City na Chelsea, imezidiwa kwenye mapato ya televisheni na timu
hizo.
Hii ni
sababu kinachoamu mapato mwisho wa siku ni kiasi cha mechi za timu ambazo
zimeonyeshwa na televisheni kwenye msimu husika na nafasi ya timu kwenye
msimamo wa ligi.
Hata
hivyo, ikumbukwe kwamba nchini England, malipo haya hufanyika baada ya msimu kumalizika
na hapo ndipo watu hukaa chini na kupigiana hesabu za nini kilipatikana. Sasa
ukitumia mfumo huu, ina maada timu zitalazimika kusubiri ligi iishe ili
kuangalia msimamo ya ligi kisha kugawana mapato. Sote tunajua jinsi timu
zinavyoteseka kwa kukosa nauli, posho, mishahara, pesa za kambi nk.
Kwa
mazingira yetu ya Tanzania kwa sasa, mfumo kama huu haufai. Hii ni kwa sababu
timu zinahitaji fedha kuanzia kwenye maandalizi ya mechi ya kwanza na
hazikopesheki fedha kwenye mabenki.
Tanzania
inachohitaji kwa sasa ni ligi yenye ushindani tofauti na sasa ambapo ushindani
uko kwa timu chache zenye uwezo wa kifedha.
Tukizijengea
uwezo timu zote taifa litakuwa na ligi nzuri na hatimaye timu nzuri ya taifa.
Pia itawezesha wadhamini wengi zaidi kuingia kwenye mpira na hivyo timu nyingi
zaidi kufaidika.
Tukifikia
huko, tunaweza kukaa chini na kutazama mfumo wa kugawana mapato utakaokuwa bora
zaidi wakati huo.
Mambo ya
Kuzingatia.Tangu ligi ianze hapa nchini takribani miaka 50 iliyopita, hakuna
timu iliyowahi kulalamikia mfumo wa kugawana mapato sawa kwa kila mechi ambao
umekuwa ukitumika. Mfano mapato ya mlangoni tumekuwa tukigawana sawa na Yanga
haijawahi kulalamika, Pesa za udhamini wa Vodacom tangia ilipokuwa ikidhaminiwa
na TBL hadi leo hii tumekuwa tukigawana sawa na Yanga haijawahi
kulalamika kutaka kupata zaidi kwa kuwa eti ina mashabiki wengi, pia hata pesa
za haki ya matangazo ya Televisheni zilizowahi kutolewa huko nyuma nailiyokuwa
ikiitwa GTV, na Star TV kwa nyakati tofauti pesa ziligawiwa sawa kwa kila timu.
Hii ni
kwa sababu kikanuni, timu zote zinazoshiriki kwenye ligi ni sawa na zote
zinaweza kuwa bingwa au kushuka daraja.
Ni mdudu
gani huyu aliyeingia kwenye soka ya Tanzania na kuanza kuleta siasa za
kubaguana? Baba wa Taifa alipata kutuasa kwamba dhambi ya ubaguzi ni sawa na
kula nyama ya mtu. Ikianza, haitaishia kwenye ligi pekee na itakwenda hadi
mahali tusipotaka.
MGOGORO WA MASLAHI
Yanga
imekuwa ikilalamikia uwepo wa kiongozi mwandamizi wa makampuni ya Bakhresa
kwenye bodi ya Ligi na kusema inaleta mgongano wa maslahi.
Sisi
vilabu tunaamini kwamba uwepo wa kiongozi huyu ndiyo umesaidia makampuni yake
kuwekeza fedha kwenye mpira. Na mifano ipo hai tukianzia na michuano ya Vijana
ya Uhai Cup, ujenzi wa kituo cha michezo cha Chamazi ambacho kinatumiwa na timu
nyingi za Tanzania.
Na sasa
tunafaidika na udhamini huu mnono ambao haujapata kutokea katika historia ya
Tanzania.
Tungependa
viongozi wengi zaidi wa makampuni yanayoheshimika hapa nchini wakijitokeza
kuongoza mpira badala ya kuanza kuwapinga.
Kwa
mfano, tungependa kuona mkurugenzi wa benki ya CRDB akiwa kiongozi wa Ashanti,
bosi wa Barrick akiongoza Mbeya City na Mkurugenzi wa Tanga Cement akiongoza
Coastal Union.
Hivi
ndivyo namna mpira unavyoweza kuvutia wawekezaji. Ndiyo maana tulifurahi wakati
Yusuf Manji, alipoomba uongozi Yanga.
Bado
tunataraji kwamba naye atajitosa kuingiza fedha zake kwenye ligi ya Tanzania
(mpira) kama alivyofanya Bakhresa ambaye pamoja na kutumia fedha zake Azam FC,
bado ameamua kusaidia na timu nyingine kwa ujumla.
Tunapenda
kumuahidi Yusuf Manji kwamba iwapo naye atataka kudhamini Ligi Kuu iwe
kibiashara au kiufadhili, sisi tutamuunga mkono na hatutajali suala la mgongano
wa maslahi.
UPOTEVU WA MAPATO
Wenzetu
Yanga wamedai kwamba kwa kuonyesha mechi kwenye televisheni, mapato yake ya
mlangoni yatapungua.
Hili pia
halikufanyiwa utafiti wa kutosha. Katika siku za karibuni, mechi zilizoingiza
mapato makubwa zaidi ya milangoni ni zile ambazo zilionyeshwa Live kwenye
televisheni za ndani na nje ya nchi.
Mifano ni
mechi za watani wa jadi msimu uliopita zilizoonyeshwa Live na SuperSport na
mechi za Kombe la Kagame zilizoonyeshwa wakati huo.
Hata
mechi ya Taifa Stars na Ivory Coast iliyoonyeshwa Live pia, ilijaza uwanja.
Ulaya ambako karibu kila familia inamiliki televisheni na umeme wa uhakika,
bado watu wanajaa katika viwanja vya soka.
Mpira
kuonyeshwa kwenye televisheni unaufanya utangazike zaidi na watu watake kuona.
Kuna faida nyingi za mpira kuonyeshwa kwenye televisheni kuliko hasara moja ya
kufikirika ambayo Yanga wanaiona.
Ingekuwa
vema iwapo Yanga wangetoa takwimu za kuonyesha ni kwa namna gani mechi
kuonyeshwa kwenye televisheni kuliwahi kupunguza mapato ya milangoni.
Kwa faida
ya umma, mpira kuwa kwenye televisheni kuna faida zifuatazo; jezi kuongezeka
thamani na hivyo kuvutia makampuni makubwa kutaka kudhamini klabu wakitumia
fursa ya kutangaza bidhaa zao, matangazo ya viwanjani (touchline fence) kuwa na
thamani zaidi ambapo kwa sasa vilabu havipati chochote, kuchochea michezo ya
kubahatisha, kutabiri matokeo na kupata habari kupitia simu za mkononi na hivyo
vilabu vitaanza kutengeneza fedha za kutosha.
Ulaya
wamesonga mbele kutokana na televisheni. Anayekataa mpira kuonyeshwa kwenye
televisheni ni sawa na mtu anayegoma kutumia mfumo wa digitali katika ulimwengu
wa leo.
UWAZI
KWENYE MCHAKATO WA KUUZWA KWA HAKI ZA MATANGAZO
Yanga
wameandika kwenye taarifa yao rasmi eti hakukuwa na uwazi kwenye mchakato wa
kuipata kampuni ya kurusha matangazo ya Televisheni.
Sote
tunajua kuwa vituo vya televisheni vilivyopo nchini kama Star TV ambayo iliwahi
kurusha mechi kadhaa msimu uliopita vilikuwa vikijua kuwa kuna nafasi hiyo na
TFF mara kadhaa wamekuwa wakitangaza hilo kupitia idara ya Habari ya TFF.
TFF kwa
mfano walikwenda mbali kwa kuialika Supersports kuja kuonesha mechi bure kwa
kilichokuwa kikiitwa Super Week ili kuwashawishi waje kuwekeza na mara ya
mwisho ni Yanga hawa hawa walioongoza harakati za kuikataa Supersports kuonesha
mechi bure wakisema kuwa kama ni kuwavutia inatosha.
Katika
mazingira kama haya tunastaajabishwa na ukigeugeu wa Yanga leo kusema eti tenda
haikuwekwa wazi. Sote tunajua kuwa ni Super Sports pekee tuliokuwa
tukiwategemea na kuwashawishi ambao hawakuonesha kuhitaji kuja kuwekeza. Kwa
nini leo tuikatae Azam TV?
Yanga
wanaposema eti TFF/Kamati ya Ligi imeipa haki za matangazo kampuni ambayo haina
ofisi wala kituo cha televisheni kilicho hewani kwa sasa wanasahau kuwa huko
nyuma TFF iliwahi kuwapa haki za matangazo GTV ambao hawakuwa na ofisi wala
kituo cha TV na baada ya miezi michache walifungua ofisi zao na kuleta
vingamuzi na kuaza kurusha mechi zetu. Vilabu vilifaidi udhamini ule kabla ya
ile kampuni kufilisika. Kwa hiyo hii si mara ya kwanza kwa jambo hili kufanyika
na kama Azam TV hawataonesha mechi za ligi hiyo sisi kama vilabu haituhusu
kwani ni hasara yao.
Tunachowaomba
Azam Media sisi kama vilabu ni kuhakikisha wanatulipa pesa zetu kwa haraka ili
zitusaidie kwenye maandalizi,Tunawaomba Yanga wasichafue hali ya hewa kwa kuwa
wao hawana shida ya Pesa.
Sisi
Umoja wa Vilabu 13 vinavyoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania tunapinga, kwa nguvu
zote, madai ya Yanga kwamba hatukushirikishwa kama vilabu kwenye mchakato huu.
Mfumo wa
ugawanyaji wa mapato tuliouchagua, tuliuchagua wenyewe bila kushurutishwa na
yeyote na tunadhani ndiyo mfumo unaotufaa kwa sasa hadi hapo ligi yetu
itakapokuwa na nguvu maana kwa sasa inaruhusiwa klabu kupata fedha mwanzoni
kulingana na hali halisi ya vilabu vyetu.
Tunawashauri
wenzetu wa Yanga waanze kuamini kwenye kitu kinachoitwa Uwajibikaji wa Pamoja
(Collective Responsibility). Mambo yanayoamuliwa kwenye vikao hayapaswi
kupingwa nje ya vikao.
Kama hoja
ililetwa kwenye vikao na ikazidiwa nguvu na hoja nyingine, hakuna sababu ya
kuikataa kwa sababu tu hukubaliani nayo. Mfumo wa kidemokrasia una kanuni moja
kuu; Wengi Wape
Imetolewa
na
Vilabu 13
vya Ligi Kuu ya Tanzania
Simba SC,
Azam FC, Ashanti United, JKT Ruvu, Ruvu Shooting Stars, Mgambo JKT, JKT Oljoro,
Rhino Rangers, Mbeya City, Tanzania Prisons, Mtibwa Sugar, Coastal Union na
Kagera Sugar.
0 COMMENTS:
Post a Comment