PAMOJA na umaarufu mkubwa
zilionao katika mchezo wa soka, klabu za Tanzania ndizo zinaongoza kwa
kuendeshwa ‘kihuruma’ zaidi.
Nasema kihuruma kwa kuwa
ndiyo klabu ambazo zinakwenda zaidi kwa kutegemea mapenzi ya dhati ya wanachama
wao ambao wanakuwa wapo tayari kutoa au kufanya lolote ili zisiyumbe.
Wanachama wengi wa Yanga
na Simba wamezigeuza klabu hizo kama furaha ya mioyo yao, huenda wana mapenzi
nazo makubwa hata kuzidi familia zao!
Hivyo wanakuwa tayari
kufanya lolote ili mradi wasizione zinaangamia, kuharibu mwelekeo au kupoteza
heshima ambayo wao wanaona inastahili sana.
Hivyo wapo wanachama ambao
wamekuwa wakitoa fedha kwa ajili ya kuhakikisha wachezaji fulani maarufu au
bora wanasajiliwa na klabu hizo kwa maana ya msaada au sifa.
Lakini pia wapo wanachama
ambao wamekuwa wakijitolea kuwalipa mishahara wachezaji ambao wanakuwa
wamesajiliwa na timu zao ili kuhakikisha wanafanya kazi vizuri.
Kutokana na mwenendo huo,
timu nyingi ukianza na Yanga na Simba, zimekuwa hazina mahesabu kamili, tena ya
uhakika ili kujua kwa mwaka zimetumia kiasi gani na zimeingiza kiasi gani.
Mfano mzuri ni katika
mkutano wa wanachama wa Simba uliofanyika hivi karibuni kwenye Ukumbi wa
Maofisa wa Polisi Oysterbay jijini Dar es Salaam.
Utaona kila kitu
kilikwenda haraka na hata katika usomaji wa matumizi na mapato, mambo yakaenda
kwa kulipua na ajabu zaidi hata wanachama wenyewe waliona ni jambo la kawaida
na hakuna waliokuwa tayari kutaka kujua mapato na matumizi kwa umakini zaidi.
Wanachama wengi walikuwa
wanataka kwenda kuona mechi ya kirafiki kati ya Simba dhidi ya URA na wakati
huo walishapewa tiketi za bure. Maana yake hakukuwa na umuhimu wa matumizi na
mapato kwao, ambacho mimi naona ni kitu cha ajabu sana.
Huenda viongozi wa klabu
nao wamekuwa wakifanya mambo kwa kulipua kwa kuwa hawana wanachama ambao ni
makini na wanaotaka kupata uhakika wa mambo badala ya kuyaacha yaende kwa kulipua.
Viongozi wanapaswa kuwa
makini na hilo na hasa wanapozungumzia suala la maendeleo ya klabu. Kweli
wanataka ziendelee lakini kama hakuna mpangilio mzuri na wa uhakika kuhusiana
na mapato na matumizi, bado itakuwa ni kupoteza muda.
Labda kama viongozi pia
wanafanya hivyo kwa makusudi kwa kuwa lengo lao linakuwa ni kutaka kufanya
mambo katika hali ya vurugu ili nao waweze kufaidisha matumbo yao.
Hata kama wanachama
watakuwa wanatoa misaada, basi si kitu kizuri kupotezea matumizi ya fedha, badala
yake wanapaswa kuonyeshwa kuwa, fedha zilizotolewa ni sehemu ya mapato, halafu
zimetumika vipi.
Hii itazisaidia klabu hata
siku zisiposaidiwa, zitakuwa zinatambua zinahitaji kiasi gani cha fedha kwa
ajili ya matumizi yake. Hivyo zijipange vipi na kufanya ubunifu kwa ajili ya
kuingiza fedha nyingi na za kutosha.
Klabu haziwezi kuendeshwa
kisayansi uwanjani tu, wakati uendeshaji wa uongozi umezorota na mambo hayaendi
kwa mpangilio wala hakuna juhudi za kitaalamu zinazofanyika kuongeza masoko na
mwisho kuongeza kipato cha klabu.
Fedha ya kutosha inafanya
kila kitu kwenda katika mstari. Kuanzia kwa Yanga na Simba kama klabu kubwa,
zina nafasi ya kuingiza fedha nyingi kama kuna ubunifu wa utanuzi wa masoko na
viongozi kweli wanakuwa na nia ya kufanya hivyo.
Lakini kujua kiasi gani
kimepatikana, kiasi gani kilitumika, itakuwa ni rahisi kung’amua wapi kulikuwa
na upungufu, nini kinatakiwa na kipi kifanyike kufanikisha na hiyo ndiyo
itakuwa dira ya kwenda kwenye mafanikio.
Hivyo, klabu lazima
zifanye kila linalowezekana kuhakikisha mambo yanakwenda namna hiyo,
ninamaanisha kitaalamu.
0 COMMENTS:
Post a Comment