Na Saleh Ally
Kibarua cha Ligi Kuu Bara kinaanza leo, kwa
wenye kumbukumbu katika mechi saba za ufunguzi wa ligi hiyo msimu uliopita
mabao kumi yalitikisa nyavu katika siku hiyo moja.
Simba ndiyo ilikuwa timu ya kwanza kupata
ushindi mkubwa baada ya kuichapa African Lyon mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Taifa,
Dar. Mganda Emmanuel Okwi akafunga bao la kwanza la ligi katika dakika ya 32,
baadaye Nassor Said ‘Chollo’ katika dakika ya 36 na Mghana, Daniel Akuffor
akafunga la tatu katika dakika ya 56.
Siku hiyo Yanga ilishikiliwa kwa sare ya
bila bao jijini Mbeya, Abdulhalim Humud akaifungia Azam FC bao pekee la ushindi
dhidi ya Kagera FC na Jerry Santo akaibeba Coastal Union kwa bao pekee la ushindi
dhidi ya Mgambo, ikiwa ni ‘vita’ ya watoto wa Tanga.
Wakati msimu mpya unaanza, kuna mambo mengi
sana ya kujadili, kwamba timu ipi itafunga mabao mengi, yatafungwa na nani na
ikiwezekana mchezaji yupi atakuwa wa kwanza kufunga bao la kwanza msimu huu.
Kwa usajili ulivyofanyika, ni yapi maandalizi
ya timu husika na ipi inaonekana inaweza kuwa bingwa, nafasi ya pili na tatu?
Au zipi zitaingia tano bora na ipi itakuwa bingwa?
Maswali yanaweza kuwa mengi, pia inawezekana
ikawa vigumu kwa majibu kupatikana kesho, lakini mwendo wa jahazi hilo la Ligi
Kuu Bara unaweza ukawa umeanza kuonekana leo na picha halisi ikajichora,
ingawa inawezekana kukawa na mabadiliko kama ambavyo msimu uliopita namna Yanga
ilivyoanza kwa kusuasua na kumaliza bingwa.
Kaseja:
Wengi watakuwa wanataka kupata majibu, Simba
kwa zaidi ya misimu minne, kwa mara nyingine itashiriki ligi hiyo bila ya kuwa
na aliyekuwa kipa wake, Juma Kaseja.
Kipa huyo ambaye huenda ndiye mchezaji
aliyecheza mechi nyingi zaidi za ligi kuu, tokea ianzishwe, si kuikosa Simba
tu, badala yake hataonekana kabisa katika mechi za ligi hiyo kwa kuwa
hakusajiliwa na timu yoyote.
Wengi watataka kujua, Mganda Abel Dhaira
ambaye ni kipa namba moja wa Simba kwa sasa ataweza vipi kuliziba pengo la kipa
huyo ambaye ni kati ya makipa bora kuwahi kutokea nchini!
Wapya
dimbani:
Wachezaji wapya ambao wanatokea katika ligi
za chini, pia ni kati ya wale ambao huibuka kila msimu. Ni wachezaji wapya ambao walikuwa katika
timu nyingine na sasa wamejiunga na timu kubwa kama Yanga au Simba.
Mfano mshambuliaji Hussein Javu, msimu uliopita
alizitesa Yanga na Simba na sasa yuko Jangwani. Ataweza kasi ya ligi akiwa
katika kikosi hicho cha mabingwa na kuendeleza cheche zake? Pia ni hivyo kwa upande
wa Simba ambayo imewasajili wachezaji kadhaa akiwemo Sino Agustino kutoka Prisons.
Kung’ara kwa wachezaji hao kunategemea
nafasi, maana yake lazima waanze kuitafuta kwa nguvu ili kuwapita waliokuwa
wameishaipata.
Wageni 15:
Wageni 15 katika timu tatu za Yanga, Simba,
Coastal Union na Azam FC ndiyo watakuwa gumzo zaidi na wataweza kuwa vipi kimsaada
kwa timu zao na changamoto kwa soka ya Tanzania.
Yanga ina Hamis Kiiza (ameenda majaribio
Lebanon), Haruna Niyonzima, Mbuyu Twite na Didier Kavumbagu ambao wote hawana
ugeni na ligi hiyo kwa kuwa kila mmoja ni msimu wa pili na tatu. Maana yake
wanaweza kupambana na hakuna tofauti kubwa na wale watano wa Azam FC ambao ni
Bryan Umonyi, Jockins Atudo, Humfrey Mieno, Kipre Bolou na Kipre Tchetche.
Simba ina wachezaji wanne wa kigeni, kati ya
hao wawili ni wageni ambao ni Kaze Patrick ‘Demunga’ na Amis Tambwe ambao
watakuwa na kazi ya kuonyesha uwezo wa kiwango chao.
Dhaira utakuwa msimu wa pili, safari hii
akiwa kipa namba moja wakati Joseph Owino amerejea Simba na ana uzoefu na ligi
hiyo ingawa hofu ya Wanasimba imekuwa ni hii; kama kweli yuko fiti hasa.
Coastal Union ina kifaa, nahodha wake Jerry
Santo, ambaye ana uzoefu wa kutosha wa
ligi hiyo katika kiungo na beki, lakini kinda mpya, Crispian Odula kutoka
Bandari ya Mombasa anategemewa kuwa chachu ya ushindi kwa timu yake na
changamoto kwa soka nchini.
Lakini Coastal ina kifaa kingine, Yayo
Lutimba, Mganda ambaye ametokea URA ya Kampala na alionyesha tayari ubabe kwa
kuzifunga Yanga na Simba katika mechi za kirafiki, kazi ipo!
Makocha
wageni:
Ingawa kutakuwa na ushindani mkubwa kutoka
kwa makocha wazalendo, msimu uliopita bingwa hadi nafasi ya tatu ilishindwa na
vikosi vinavyoongozwa na makocha wageni, Ernie Brandts (Yanga), Stewart Hall
(Azam FC) na Patrick Liewig (Simba).
Safari hii Simba ina makocha wazalendo,
Abdallah Kibadeni na Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ ambao wana kazi ya kuonyesha
wanaweza kufanya kazi yao kwa ubora zaidi ya wageni, hii maana yake lazima
wachukue ubingwa au nafasi ya pili.
Lakini wageni hasa Brandts na Hall wana
nafasi ya kuonyesha walichofanya msimu uliopita haikuwa bahati, pia wana
kibarua kigumu cha ushindani kutoka kwa makocha wazalendo kama Mecky Maxime
(Mtibwa Sugar), Ahmed Morocco (Coastal), Charles Boniface (Ruvu Shooting), Juma
Mwambusi (Mbeya City) na wengine.
Kagera Sugar ni washindani kama ilivyokuwa
msimu uliopita lakini safari hii watakuwa chini ya Mganda, Jackson Mayanga,
ambaye ana kibarua cha kubakisha ubora na kuupandisha.
Ligi itakuwa ngumu, ushindani utakuwa juu
lakini lazima timu zote zijue, wakiwemo wachezaji wageni, kuwa watakutana na
ushindani mkali kutoka kwa timu zisizokuwa na wachezaji wenye majina makubwa.
Timu kama Ruvu JKT, Ruvu Shooting lakini pia
kutoka Mtibwa Sugar, Kagera Sugar zina wachezaji wengi wenye uzoefu mkubwa na
Ligi Kuu Bara, hivyo wanajua wafanye nini.
MSIMAMO
WA 2012-13
P W D L GF GA Pts
1. Yanga 26 18 6 2 47 14 60
2. Azam 26 16 6 4 46 20 54
3. Simba 26 12 9 5 38 25 45
4. Kagera 26 12 8 6 28 20 44
5. Mtibwa 26 10 9 7 29 25 39
6. Coastal 26 8 11 7 25 24 35
WAFUNGAJI BORA 2012-13
Kipre Tchetche, Azam 17
Didier Kavumbagu, Yanga 10
Paul Nonga, JKT Oljoro 9
MECHI ZA
UFUNGUZI LEO:
Agosti 24,
2013
Yanga v Ashanti
Taifa
Mtibwa v Azam Manungu
Oljoro v Coastal Abeid
Mgambo v JKT Ruvu Mkwakwani
Rhino v Simba A.H. Mwinyi
Mbeya City v Kagera Sokoine
Ruvu v Prisons Mabatini
0 COMMENTS:
Post a Comment