Na Saleh Ally
Sakata la Yanga kuweka ngumu kuhusiana na mkataba wa
Azam TV kuonyesha live mechi za Ligi Kuu Bara limekuwa likiendelea kupasua
vichwa.
Baadhi ya wasomaji wengi wamekuwa wakihoji baada ya
kuandika makala iliyoelezea kuhusiana na namna Yanga walivyokuwa na haki ya
kuhoji kuhusiana na mkataba huo.
Hali hiyo imenishawishi huenda uchambuzi huo wa kwanza
haukujitosheleza vilivyo na huenda sikugusa sehemu kadhaa, ndiyo maana pamoja
na pongezi, maswali yamekuwa pamoja.
Leo, nataka kusisitiza zaidi kwamba Yanga walikuwa na
kila sababu ya kuhoji kwa kuwa suala hilo la mgawo wa kinachotolewa baada ya
mdhamini kutoa fedha zake za kuonyesha ligi moja kwa moja.
Azam TV imetoa fedha na bodi ya ligi imeamua kila timu
itapata Sh milioni 100 kwa msimu, Yanga wanahoji kuhusiana na hilo wakiamini
wao ni tofauti na timu nyingine, wanaamini wanastahili kupata nyingi.
Hakika wana haki, sababu zao ni za msingi na hata
katika ligi kubwa duniani kama England, Hispania na Italia kumekuwa na mifumo
tofauti ambayo huenda bodi ya ligi hapa nyumbani ilipaswa kuiangalia.
Katika mkutano kati ya watu wa bodi na Yanga,
nilichoelezwa wawakilishi wa Yanga mwisho walishindwa kugeuza mfumo na utabaki
uleule wa kila klabu kupata Sh milioni 100. Lakini huenda hawakujenga hoja
vizuri au kujimbua mambo zaidi.
Watu wa bodi walitolea mfano Ligi Kuu England maarufu
kama Premiership kuwa timu zote zina mgawo sawa. Nilipoamua kuchimba nilikuta
mambo ni tofauti na hata ufafanuzi wa Seria A na La Liga, bado unaonyesha Yanga
ilikuwa na hoja ya msingi.
Premiership:
Mgawo wa Ligi Kuu England bado hauko sawa kwa sawa
kama ilivyoeleza awali, badala yake mambo yako hivi, mgawo hufanyika katika
makundi matatu.
Kundi la kwanza ni fedha zinagawanywa asilimia 50
katika zote zilizopo na kila klabu kati ya 20 zinapewa sawa. Kundi la pili ni
asilimia 25 ni malipo ambayo hutolewa kwa klabu kutegemeana mara ngapi
ilionekana kwenye runinga ‘live’.
Asilimia 25 za mwisho, pia zinagawanywa kutegemeana na
timu imeshika nafasi ya ngapi katika msimamo wa ligi hadi ilipofikia tamati (merit payment).
Maana yake kama ni bingwa, mshindi wa pili, tatu
watapata zaidi na aliye mkiani atapata kidogo.
Mfano katika msimu wa 2011-12, mabingwa Man City
walipata mgawo wa pauni milioni 60.6 wakati Wolves waliokuwa mkiani wakapata
pauni milioni 39.1.
La Liga:
Real Madrid na Barcelona mara nyingi hawana tofauti
kubwa ya kipato wanachopata, lakini mfumo wao ni tofauti na England, huku kila
timu inaruhusiwa kujitafutia wadhamini au watangazaji ambao watawalipa.
Ingawa kuna lawama kuhusu mfumo huo na unatakiwa
kubadilishwa maana timu hizo mbili kubwa zinapata mara 14 ya nyingine.
Kigezo chao ni kilekile, kwamba ndiyo timu kubwa,
zenye mashabiki wengi na ikiwezekana watazamaji wengi.
Seria A:
Katika
msimu wa 2009-10 klabu kubwa ttau za Italia, Inter Milan, AC Milan na Juventus,
kila moja iliingia mkataba na kampuni ya Mediaset kuonyesha mechi zao na kwa
msimu ikalipa euro milioni 100 kwa kila moja.
Kutokana
na malipo hayo kwa klabu hizo kubwa tatu, asilimia 20 ilibaki kwa ajili ya
klabu nyingine 17 za Seria A na hapa bado kigezo ni ukubwa kwa maana ya
mashabiki na jina.
Mifano
hii michache inaonyesha kiasi gani Yanga walistahili kuhoji na namna gani klabu
nyingine kubwa zilishindwa kutaka kufanya uchunguzi angalau kidogo na kutaka
majadiliano kwanza.
Haki
za runinga zinakuwa ni za shirikisho, lakini timu kwa kuwa ndiyo inayoonekana,
tumeona inapewa hadi ya kupata fedha kulingana na inavyoweza kuingiza.
Ndiyo
maana hata katika makala yaliyopita, nilihoji kama Azam FC itategemea kupata
watangazaji kupitia mechi kati ya Ruvu Shooting na Rhino. Hakika watakuwa ni
watazamaji wachache na hata wadhamini watakaotoa fedha nyingi watasubiri
kuingiza fedha zao katika mechi zitakazoihusu Yanga au Simba, hata Azam FC
wanalijua hili ndiyo maana kuna tofauti wakicheza na timu nyingine wanachezea
Chamazi, wakikutana na kati ya timu hizo mbili, mechi lazima iwe Uwanja wa
Taifa.
Inavyoonekana
kama suala halijaisha, huenda Yanga na Azam TV watafikia mwafaka, lakini
ninaasa kuwa kuwe na hali ya uhuru wa kuhoji badala ya mambo kupelekwa kibabe.
Klabu
13 zilizobaki zilikubaliana na suala hilo, sawa. Kwanza mimi nasema ni klabu 11
tu, maana Azam FC iko na Azam TV, halafu Simba tayari ina mkataba na kampuni
hiyo, automatically hawa hawana jeuri ya kupinga.
Lakini
hizo 11, pia zina kila sababu ya kufurahia Sh milioni 100 kwa msimu, pili
zitaonekana kwenye runinga. Lakini Yanga, wanaonyesha kujitambua hata kama
walikuwa hawana pa kuipata hiyo fedha, lakini isiwe kigezo cha kuwafunga mdogo,
badala ya hoja zao zisizo na msingi zitupwe kule, zile zenye msingi,
zisikilizwe na kufanyiwa kazi.
Bado
bodi inapaswa kuheshimu ukubwa wa timu hiyo na ilichonacho, kutaka usawa ni
kitu kizuri, lakini iwe sehemu sahihi. England wanajali usawa, lakini angalia
katika mgawo wao wamegawanya makundi matatu, kundi la mwisho la asilimia 25,
linaangalia klabu imeshika nafasi ya ngapi.
Hii
inaonyesha bado Yanga walikuwa na mengi ya kudai, ukiachana na ukubwa wao, lakini pia
wanaona si sahihi kugawana sawa na timu iliyoshika mkia. Siamini kama Yanga
hawana hoja, au jambo lenyewe linapelekwa kishabiki sana, hali inayosababisha
kupoteza mwelekeo na uzushi kutawala.
Keshokutwa
Ijumaa nitawafafanulia zaidi kuhusiana na uonyeshwaji wa mechi katika Ligi Kuu
England, namna wanavyoweza kudhibiti na kujali mapato ya klabu husika.
FIN.
0 COMMENTS:
Post a Comment