Straika mpya wa Yanga, Lusajo Renatusi, amejiunga na Yanga juzi na
kuanza mazoezi moja kwa moja kwenye Uwanja wa Loyola jijini Dar es Salaam.
Straika huyo aliyesajiliwa na mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara katika
kipindi hiki cha usajili akitokea Machava FC ya Moshi, alikuwa hajatua klabuni
hapo kwa kuwa alikuwa anamalizia masomo yake katika Chuo Kikuu cha Ushirika na
Biashara (MUCCOBS) kilichopo Moshi.
Katika mazoezi yake ya kwanza akiwa na Yanga juzi, mshambuliaji
huyo alionyesha uwezo wa hali ya juu uliomtisha Kocha Mkuu, Ernie Brandts.
Akizungumza na Championi Jumatano, Brandts alisema ameridhishwa na
kiwango cha mshambuliaji huyo na kwamba ataongeza changamoto kwenye safu ya
ushambuliaji ya timu hiyo ambayo tayari ina wakali wengine kama Didier
Kavumbagu, Jerry Tegete, Said Bahanuzi na Hussein Javu.
Kocha huyo raia wa Uholanzi, alisema Lusajo ana kasi, anajua
kufunga mabao na kukaba kwa wakati mmoja, hivyo anaamini ataisaidia timu kwenye
msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.
“Nimeridhishwa na kiwango cha Lusajo ndani ya uwanja, ni mchezaji
mwenye kasi na uwezo wa kufunga mabao. Kitu kingine ni kwamba anajua kukaba.
“Ujio wake katika kikosi changu utaongeza changamoto ya namba
kwenye nafasi hiyo anayocheza,” alisema Brandts.
0 COMMENTS:
Post a Comment