Ukifanikiwa kufanya
ziara katika kambi za klabu nyingi za soka nchini, utakutana na vitu vingi vya
kuchekesha au kushangaza. Viongozi wengi wa klabu wanapanga na kueleza mipango
yao kwenye makaratasi, suala la vitendo linakuwa ngumu kutekelezwa.
Klabu ya Coastal
Union ya Tanga imepiga hatua katika suala la kambi kutokana na kutengeneza
mazingira ambayo kwa soka la Tanzania ni mazuri na yanamfanya mchezaji kuhisi
kuthaminika. Kambi yao ipo Raskazone
mkoani humo.
Mtaa huo ambao
kambi hiyo ya Coastal ipo, umetawaliwa na hali ya utulivu, huku wenyeji wake
wengi wakionekana kutumia baiskeli kwa ajili ya usafiri kama walivyo wakazi
wengi wa mji huo ambao msemo wa ‘Waja leo waondoka leo’ ni maarufu.
Championi Ijumaa
lilitua kambini hapo na kupokelewa na mlinzi wa kambi hiyo ambaye alilipeleka
moja kwa moja kwa mkuu wa kambi hiyo, Ally Salim Mohamed, maarufu kwa jina la King
Mswati, jina ambalo amepewa na wachezaji wa kikosi hicho.
Akielezea juu ya
kambi hiyo, King Mswati anasema: “Kikubwa ni kutokana na uongozi wa Coastal
Union kutaka kuona kila kitu kinakuwa sawa katika kuwapatia wachezaji sehemu
nzuri, hali ya utulivu na kuwa mbali na katikati ya mji kunawafanya wachezaji
kutumia muda mwingi wakiwa pamoja.
“Hiyo inawasaidia
kupeana elimu ya hapa na pale ya ndani na nje ya uwanja. Kazi yangu kubwa hapa
ni kuhakikisha vijana wanakuwa sawa kwa kupata kila kinachotakiwa wapewe kwa
wakati unaotakiwa, kuanzia wanapoamka mpaka jua linapozama.
“Kila siku kuanzia
saa tatu na nusu asubuhi natakiwa kuhakikisha chai ipo tayari, wanapata chai
safi, chapati mbili na mayai mawili ya kuchemsha au kukaanga, inategemea na
anachopenda mchezaji.
“Mchana kuanzia saa
sita na nusu ni muda wa chakula cha mchana, hapo wanaweza kupata wali au ugali inategemea
na ushauri wa daktari wa timu ambaye pia anazingatia ratiba ya mlo wa jioni. Wali
au ugali vinaongozana na nyama ya ng’ombe au samaki, mboga za majani, maharage
na matunda mbalimbali.
“Aidha, hivi
karibuni tunatarajia kuanza kuwapatia juisi, hayo yote yanafanyika ili
kuhakikisha wanakuwa na afya bora.”
Kuhusu ulinzi
anasema: “Hapa kama ulivyoona ukifika unakutana na mlinzi getini na baada ya
hapo unajieleza juu ya kile kilichokuleta, lakini kuhusu wachezaji wapo salama
hakuna anayeruhusiwa kuvuka geti bila taarifa za msingi.
“Kuna wakati
tunawaweka huru kidogo kama hakuna ratiba muhimu ya michezo ya ligi, lakini wanapokuwa
hapa hakuna mchezaji anayeruhusiwa kuwa nje ya geti kuanzia nne usiku labda
wawe katika mapumziko marefu.”
Gazeti hili liliwakuta wanawake wawili
waliojitambulisha kwa majina ya Halima Alawi (Mama Chanji) na Halima Jumaa ambao
ndiyo waliokuwa na kazi ya upishi, nao walisema kuwa walianza kazi hiyo miezi
mwili iliyopita.
Naye
Mkurugenzi wa Ufundi wa Coastal Union, Nassoro Bin Slum anasema: “Jengo hilo
tumepangisha kwa muda wa mwaka mmoja, awali ilikuwa ni Hoteli ya Raskazone.”
Akizungumzia juu ya kambi ya timu hiyo, nahodha
wa Coastal, Jerry Santo, anasema: “Kambi ni nzuri na tunashukuru vitu vingi
tunapata kwa wakati, kila mchezaji ana furaha ya kuwa hapa, uongozi umeonyesha
kujipanga katika hili, hivyo sisi wachezaji ni jukumu yetu kuonyesha uwezo.”
Mshambuliaji wa Coastal, Lutimba Yayo raia wa
Uganda anasema: “Hili ni jambo geni kwangu kwa kuwa kule nyumbani (Uganda) timu
hazikai kambini, wachezaji wanakutana na kwenda makwao, lakini hili ni jambo
nzuri kwa kuwa linawaweka wachezaji pamoja na tunapata nafasi ya kuzungumza kama timu.”
0 COMMENTS:
Post a Comment