Na Saleh
Ally
Vipigo mfululizo vya timu ya taifa, Taifa Stars, vimeonyesha kuwakera mashabiki wengi
ambao wanaona kuna haja ya kufanya mabadiliko katika kikosi au hata kocha.
Stars
imepoteza mechi nne mfululizo za mashindano ya aina mbili tofauti, kuwania
kucheza Chan na mechi za awali za kuwania kucheza Kombe la Dunia mwakani huko
Brazil.
Ivory
Coast ilianza kutibua raha ya Stars kwa kuifunga mabao 4-2, mechi mbili za
Uganda kuwania kucheza Chan, Stars ikapoteza 1-0 nyumbani na 3-1 ugenini.
Uvumilivu wa wengi ukaisha baada ya Stars kupoteza mechi ya mwisho ya kukamilisha
ratiba.
Mechi
hiyo dhidi ya Gambia, Stars ilifungwa mabao 2-0 ikiwa ugenini. Umuhimu wa mechi
hiyo ulikuwa hivi, Stars ingeshinda ingemaliza ya pili katika kundi na
kujiwekea uhakika wa kuanzia mbele itakapopangwa ratiba nyingine ya michuano
hiyo ya awali. Lakini sasa italazimika kuanzia katika mechi za awali kabisa
baada ya kushika nafasi ya tatu.
Watanzania
ambao furaha kubwa mara ya mwisho ni pale Stars ‘ilipoitoa shoo’ Morocco kwa
kuichapa mabao 3-1, wamepoteza imani na wengine wanashauri kikosi kibadilishwe
au Kocha Kim Poulsen aondoke zake.
Tatizo
ni lipi hasa Stars inaonekana kuporomoka kwa kasi?
“Tatizo
kubwa katika soka liko hivi, ukipoteza mchezo na ukajaribu kuelezea utaonekana
unajitetea, lakini hali halisi ni kwamba kuna ugumu wa mambo mengi na yanapaswa
kufanyiwa kazi.”
Mambo
yapi, unaweza kuyafafanua?
“Utakubaliana
nami, Tanzania ni nchi inayochipukia kisoka. Tuna wachezaji wachache sana
wanaocheza nje na tunawahitaji kila mechi tunayocheza lakini mambo yamekuwa
tofauti na ugumu unatokea kila ninapokuwa nimechagua kikosi.”
Mfano,
mechi dhidi ya Gambia ulimkosa nani?
“Mechi
dhidi ya Gambia nilikosa wachezaji kumi ambao ninaamini ninawahitaji kwa ajili
ya kikosi cha kwanza. Juma Kaseja ni kipa niliyekuwa ninamhitaji, nilikuwa
naye. Shomari Kapombe (beki wa kulia), alishindwa kuja na Shaabani Nditi wa
Chelsea, kwangu ingekuwa bora kucheza namba tatu.
“Sikuwa
na watu wote wa kati, Kelvin Yondani na Aggrey Morris. Kiungo wa kukaba
Athumani Idd na kiungo wa juu, Sure Boy (Salum Abubakari). Washambuliaji wawili,
Mwinyi Kazimoto na Thomas Ulimwengu au John Bocco. Namba 11, Mbwana Samatta
lakini kiungo wa kulia ningependa kumtumia Ismail Ferouz ambaye yuko Chelsea
pia.
“Inawezekana
ningewachezesha wengine kama Amri Kiemba, Mrisho Ngassa na Frank Domayo lakini
hao wote niliowataja wangekuwa msaada kwetu. Lakini haikuwa hivyo.”
Unafikiri
unapaswa kubadili kikosi au uondoke na Tanzania ipate kocha mwingine?
“Maoni
kila mtu ana yake, mimi ni mwajiriwa wa TFF. Kama itafikia hivyo, sitakuwa na
kipingamizi, lakini nitashauri kwanza matatizo ya kuhakikisha wachezaji
wanaotakiwa na kocha wanapatikana kuliko kuamini kocha ndiyo mwenye tatizo.
“Mnaweza
kuweka kocha mwingine lakini kama matatizo ni haya anaweza asifanikiwe pia, hivyo
mkaendelea kubadili makocha bila ya mafanikio na mwisho mambo yakaendelea kuwa
mabaya.”
Sasa
nini kifanyike kuweka mambo sawa kabla Watanzania hawajahamia kwako?
“Kuhakikisha
wachezaji ninaowachagua wanapatikana, kazi yangu ni kuchagua ninaowataka na TFF
inahakikisha wanafika. Timu kama TP Mazembe wamekuwa tatizo kubwa kuwaachia
wachezaji bila sababu za msingi, TFF wanalijua hili.
“Wangejitahidi
kubadilika na kuwa wakali hasa katika tarehe ambazo ziko chini ya Fifa maana
timu ya taifa inakuwa na haki. Lakini TP Mazembe wamekuwa wakiamua na wakati
mwingine kusema ni wagonjwa lakini hali halisi sivyo.”
Mechi za
Chan, Samatta na Ulimwengu wasingeruhusiwa. Timu ikacheza vibaya, kiwango cha
chini. Kisingizio ni nini?
“Nitakachosema
ni kisingizio, si najitetea ila ninafafanua, tafadhali nieleweke. Maandalizi
yalianza katika kipindi cha Mwezi Mtufuku wa Ramadhani, ninaheshimu sana imani
ya wenzangu. Lakini nusu ya timu walikuwa wanafunga.
“Jiulize,
vipi unampa mazoezi makali mchezaji. Lakini hata siku ya mechi ilikuwa hivyo na
kweli tulicheza vibaya. Nilisikia uchungu sana kwa kuwa Uganda walikuwa chini
ya uwezo wetu, sasa nifanyaje? Siwezi kuingilia imani ya mtu mwingine.”
Kuhusu
kuita wachezaji wa nje, unafikiri huwezi kufanya vizuri bila ya wao?
“Wao
ndiyo Tanzania, utaona wengi wao wamepata timu nje kwa kuwa walicheza vizuri
kwenye kikosi cha Taifa Stars. Kapombe na Kazimoto ni mfano mzuri, kumbuka nchi
yetu ni ndogo na ina watu wachache ambao wanafanya vizuri.
“Wachezaji
wanaocheza nje wana mafunzo na uimara zaidi, wanaweza kuwa msaada zaidi kwa
kuwa tunapokwenda kucheza na timu kama Morocco, Ivory Coast tunakutana na
wachezaji wenye mafunzo ya kisasa na uzoefu mkubwa.
“Lazima
kuwe na uchungu na timu ya taifa, wachezaji lazima wakubali inachangia kuwatangaza
kila inapofanya vizuri. Hivyo wafike mara moja kila wanapoitwa na kulitetea
taifa lao ambalo linawafaidisha.
“Leo
mchezaji akitaka kusajiliwa Ulaya, basi wanaangalia katika viwango vya Fifa
taifa lenu liko namba ngapi. Mkiwa katika kiwango kizuri ni sehemu ya soko
zuri, hivyo lazima waithamini na kujua inawatangaza.”
Vipi
kuhusu kutafuta wachezaji hapa nyumbani?
“Kuna
ile timu ya vijana, tutaipa nafasi lakini bado nitafanya ziara katika mikoa
kadhaa na kutafuta wachezaji.”
Ubovu wa
viwanja vya mikoani hauwezi kuwa tatizo kwako kugundua vipaji sahihi?
“Swali
zuri, kujua mchezaji bora, kwa kiwanja bora inakuwa sahihi zaidi. Lakini ndiyo
hali halisi, kwa kocha mzoefu kama mimi naweza kuangalia mambo mengine na ubora
mwingine utapatikana nitakapomchukua na akatumia kiwanja kizuri.”
0 COMMENTS:
Post a Comment