Kocha Mkuu wa Yanga, Ernie Brandts
amesema kikosi chake kipo tayari kwa ajili ya mchezo wa kesho Jumamosi dhidi ya
Mbeya City, kwenye Uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya, lakini tatizo kubwa ni afya
ya kiungo wake mkongwe, Athuman Idd ‘Chuji.’
Hatua hiyo inakuja kufuatia Chuji
kuumia goti la kulia katika mchezo wa ufunguzi wa Ligi Kuu Bara, dhidi ya
Ashanti United ambao timu yake ilishinda kwa mabao 5-1, ambapo tangu apatwe na
maumivu hayo, alishindwa kuitumikia klabu hiyo.
Brandts amesema kikosi chake kimetua
salama Mbeya, tayari kwa mchezo huo wa kesho, lakini hana uhakika kama ataweza
kumtumia Chuji au la katika mchezo huo.
“Daktari wetu (Nassoro Matuzya)
anaendelea kufuatilia kwa ukaribu afya yake, maana nilizungumza na Chuji, akaniambia
bado anasikia maumivu kwa mbali katika ile sehemu aliyoumia,” alisema Brandts.
Wakati huohuo, beki wa kati wa timu
hiyo, Kelvin Yondani amepona na yupo fiti kwa ajili ya mchezo huo.
Yondani ambaye aliumia katika mechi ya
Ngao ya Jamii dhidi ya Azam, alisema: “Nimepona majeraha ya misuli ya paja
baada ya kukaa nje ya uwanja wiki moja. Nipo fiti kucheza mechi ya Jumamosi
(kesho).” Yanga ina pointi nne sawa na Mbeya City ambapo timu zote zimecheza
mechi mbili mpaka sasa.
0 COMMENTS:
Post a Comment