Mshambuliaji wa
zamani wa Simba na timu ya taifa, Taifa Stars, Joseph Kaniki amepandishwa
kizimbani jijini Addis Ababa, Ethiopia kutokana na tuhuma za kukamatwa na
madawa ya kulevya.
Iwapo Kaniki
pamoja na mwenzake Mkwanda Matumla ambaye ni bondia watapatikana na hatia, basi
watafungwa nchini Ethiopia hadi watakapomaliza kifungo chao, Serikali ya
Tanzania imethibitisha hilo.
Kaimu Balozi
wa Tanzania nchini Ethiopia, Samuel Shelukindo ameliambia Championi Ijumaa,
jana kutoka Addis Ababa kuwa, Kaniki na Mkwanda walipandishwa kizimbani kwa
mara ya kwanza mwanzoni mwa wiki na
huenda ikawa hivyo tena wiki ijayo.
“Jana (juzi)
tulikwenda kuwaona na tumekuwa tukifuatilia kwa karibu, huku kidogo kuna
utaratibu tofauti, hivyo hatujajua lini watapandishwa tena kizimbani kwa mara
ya pili.
“Iwapo
watapatikana na hatia, kama ni kifungo cha jela, basi watatumikia hapa
Ethiopia. Maana tunabanwa kutokana na kutokuwa na mkataba wa kupeana
washitakiwa au wafungwa kama ambavyo nilieleza awali,” alisema Shelukindo.
“Hii juzi tu,
kuna Watanzania wengine walikuwa wamefungwa hapa na tayari wameshamaliza
vifungo vyao, wameondoka kurejea nyumbani.
“Lakini
tumekuwa tukifuatilia kwa karibu, lengo ni kuhakikisha hata kama watuhumiwa au
wakihukumiwa, basi haki yao inapatikana. Uingereza, Marekani na nchi nyingine
wamekuwa wakifanya hivyo.”
Lakini
taarifa nyingine ambazo gazeti hili limezipata kutoka kwa Mtanzania anayeishi
Addis Ababa, zinaeleza Kaniki amekuwa akilia gerezani usiku kucha.
“Kuna
Watanzania wenzetu wamefungwa katika gereza ambalo Kaniki yumo, tulienda
kuwaona juzi, yeye hatukumuona. Ila wanasema amekuwa akilia usiku kucha, tena
wakati mwingine kwa sauti ya juu akionekana kulijutia suala hilo,” alisema
Mtanzania huyo ambaye hakupenda kutajwa jina lake gazetini.
Kaniki na
Mkwanda walikamatwa siku kadhaa zilizopita kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa
wa Bole, Addis Ababa nchini humo wakiwa njiani kwenda barani Ulaya na taarifa
zinaeleza wangetua Italia, nyingine Hispania lakini wawili hao wanaishi Sweden.
Kaniki
amewahi kuzichezea Simba, Mtibwa Sugar na Rayon Sports ya Rwanda, alikwenda
kufanya majaribio Sweden ambako alifeli lakini baadaye akasajiliwa na timu ya
daraja la pili ya Konya ambayo hata hivyo, hakudumu nayo na kazi yake ya mwisho
ilikuwa ni ufagizi katika kampuni ya usajili mjini Norrkoping.
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment