October 21, 2013




Wakati Ligi Kuu England, sasa maarufu kama Premiership ilipoanza rasmi mwaka 1992, kulikuwa na mchezaji mmoja tu Mwislamu, Nayim, aliyekuwa kiungo wa Tottenham, raia wa Hispania.


Lakini katika msimu huu, kuna takribani wachezaji 40 Waislamu wanaoshiriki ligi hiyo wakiwa na timu mbalimbali kati ya 20 zilizopo.

Wastani wa wachezaji wawili Waislamu katika kila timu ya Premiership na nguvu ya dini hiyo, umeanza kubadili mambo kadhaa.
Wachezaji wenye imani ya dini hiyo, wamekuwa imara na mambo kadhaa yamekuwa yakilazimika kubadilishwa kutokana na wanachoamini.

Demba Ba aliyetoka Newcastle kwenda Chelsea na Demba Cisse aliyebaki, wote raia wa Senegal, wamekuwa maarufu kutokana na misimamo yao ya kupinga mambo kadhaa katika ligi hiyo yanayopingana na maelekezo ya Uislamu.

Mara kadhaa, kila wanapofunga, wamekuwa wakikimbia kwenye kibendera na kuinama kusali.

Kutokana na kurudia kwao mara kwa mara, watoto kadhaa katika timu za vijana za Newcastle, wamekuwa wakiinama na kusali kila wanapofunga mabao, bila ya kujali imani zao.

Pamoja na juhudi za makocha wao kujaribu kuwazuia, lakini vijana hao wamekuwa wakiendelea kufanya, baadhi wakiamini kushukuru kwa kusujudu, kunasaidia kufunga mabao mengine.
Zawadi ya mwezi:

Kila mchezaji anaposhinda tuzo ya kuwa bora kwa mwezi katika Premiership, amekuwa akipewa chupa kubwa ya mvinyo. Lakini aliposhinda kiungo wa Manchester City, Yaya Toure, aligoma kuichukua zawadi hiyo, akisisitiza pombe ni haramu katika Uislamu.

Hali hiyo ilizua taharuki na baada ya mjadala, Bodi ya Premiership iliamua kubadili zawadi na sasa mshindi wa mwezi amekuwa akipewa tuzo maalum kuonyesha ameshinda, bila ya mvinyo.

Wapo waliokerwa na hilo, lakini hakuna ubishi ili kuheshimu imani za wote, uamuzi huo ukapitishwa.

Kitu kingine ambacho kimekuwa na mabadiliko ni wachezaji Waislamu kutengenezewa sehemu maalum kwa ajili ya chakula.
Kila timu inapokuwa kambini, Wazungu ni watu wanaokula nguruwe kwa wingi. Hivyo hulazimika kuwawekea Waislamu sehemu yao maalum hata kama wako wawili au mmoja, lengo ni kuonyesha wanaheshimu dini yao kwa kiasi gani.

Ramadhani:
Ugomvi mkubwa umekuwa kwenye mfungo mtukufu wa Ramadhani, makocha wengi wa Premiership wamekuwa wakichukizwa nao kwa madai wachezaji hawali chakula kwa saa 18, hivyo kushindwa kufanya vizuri.

Abou Diaby aliwahi kuzozana na kocha wake, Arsene Wenger na akasisitiza lazima afunge kama ilivyowahi kumtokea Ba wakati akiwa Newcastle.

Msimu uliopita, wakati Ba akiwa katika mzozo na kocha wake, Alan Pardew, mashabiki walitunga wimbo maalum na waliimba kila alipofunga na kusisitiza kwamba mabao hayakuwa yakitosha, aongeze.

Lakini mshambuliaji wa zamani wa Stoke City, Mamady Sidibe aliwahi kumueleza kocha wake achague kumpanga au kumuweka benchi lakini lazima afunge, huku akisisitiza wako wenye swaumu na wanafanya vizuri uwanjani.

Kushangilia:
Utamaduni wa Premiership ni wa Kizungu, hilo halina ubishi, ndiyo maana hata timu inapobeba ubingwa hushangilia kwa kutumia mvinyo wakimwagiana na kunywa kwa furaha.
Baada ya Swansea kushinda Kombe la Carling 2013 baada ya kuichapa Bradford kwa mabao 5-0, ushangiliaji wao ulikuwa wa umakini mkubwa na walitaarifiwa kuepuka kuwamwagia pombe wenzao ambao ni Waislamu.

Wadhamini:
Vita hii iliendeshwa na Ba na Cisse ambao wamekuwa mstari wa mbele kupinga kuvaa nembo za wadhamini ambao bidhaa zao zinakiuka maagizo ya Uislamu.

Cisse aligoma kuvaa jezi ya Newcastle inayowatangaza Wonga ambayo ni kampuni ya kamari. Baadaye alilegeza msimamo baada ya mazungumzo ya kipindi kirefu.

Lakini wapo wachezaji Waislamu, hasa waliozaliwa na kukulia Ulaya ambao wamekuwa hawana misimamo mikali sana kama Hatem Ben Arfa ambaye aliendelea kuvaa Wonga bila ya matatizo.
Kipa wa Wigan, Ali Al-Habsi kabla haijateremka daraja, aliwahi kusema wachezaji Waislamu wana wakati mgumu sana katika ligi hiyo au Ulaya kote.

Alichosisitiza kwake anaupenda mpira, lakini asingependa kutangaza vitu vinavyokiuka Uislamu. Hata hivyo, akawapongeza Waingereza kwa kuwa wakati fulani wamekuwa hawana matatizo kuonyesha heshimu kwa Uislamu.

@@@@@@@@@

BAADHI YA WACHEZAJI NYOTA WAISLAMU PREMIERSHIP:
Mesut Ozil (Arsenal-Ujerumani)
Adnan Januzaj (Man United-Ubelgiji)
Abou Diaby (Arsenal-Ufaransa)
Adel Taarabt (QPR- Morocco)
Ahmed Elmohamady (Sunderland-Misri)
Armad Traore (QPR-Ufaransa)
Bacary Sagna (Arsenal-Ufaransa)
Demba Ba (Chelsea-Senegal)
Leo Osman (Everton-Uingereza)
Kolo Toure (Liverpool-Ivory Coast)
Yaya Toure (Man City-Ivory Coast)
Mamady Sidibe (Stoke City-Mali)
Marouane Chamakh (Palace-Morocco)
Marouane Fellaini (Man United-Ubelgiji)
Mousa Dembele (Spurs-Ubelgiji)
Papiss Cisse (Newcastle-Senegal)
Samir Nasri (Man City-Ufaransa)
Youaness Kaboul (Spurs-Ufaransa)
Hatem Ben Arfa (Newcastle-Ufaransa).
FIN.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic