Mara kibao nimekuwa nikizungumzia
kuelezea namna ambavyo klabu kongwe nchini zilivyo na utajiri mkubwa wa watu lakini zimekuwa hazifanyi
lolote kuutumia kujipatia maendeleo.
Mechi ya jana iliyowakutanisha ndiyo
mechi kubwa kuliko zote katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na
inawezekana ikawa moja ya mechi tano kubwa kabisa barani Afrika.
Mechi ambayo ina uwezo wa kuiginza hata
Sh milioni 600, lakini fedha za mapato zimekuwa hazifikii hapo kwa kuwa wengi
wamekuwa wakifaidika na fedha nyingi kwenda mifukoni mwao.
Yanga na Simba, zina mashabiki zaidi
milioni 30 kwa hapa nchini, inawezekana kabisa kama zingekuwa na mipango
madhubuti kujenga timu kubwa na zenye ubunifu za masoko, basi zingekuwa
zinaingiza mamilioni ya fedha.
Hazifanyi hivyo kwa kuwa siasa inaizidi
hali halisi ya maisha ya klabu hizo, viongozi wengi wanaoongoza ni wale
wanaotaka kutengeneza majina yao, wanaozuia kwa makusudi maendeleo makubwa kwa
kuwa wanajua siku chache zijazo wataondoka, hivyo hawataki wengi wakute kuna
maendeleo badala yake, kila kiongozi anayeingia analazimika kuanza mwanzo.
Simba na Yanga, jana zinegeweza kupata
mapato makubwa kama ilivyokuwa kwa kuwa tiketi ziliisha ndani ya saa 10 tu. Na
bado ilionekana kuna watu walikuwa wakitaka wapate tiketi, lakini
ikashindikana.
Lakini kiongozi yupi ambaye alihakikisha
kunakuwa na wadhamini ambao wangeweka mabango ambayo yangewaingizia angalau Sh
milioni 150 kwa siku hiyo, hata kama wangetakiwa kugawana na bodi ya ligi.
Kama wangekuwa na timu bora ya masoko,
kwa miezi ingekuwa ikienda na kuzungumza na wadhamini kuwaeleza kwamba mechi
hiyo itaangaliwa na watu zaidi ya 60,000 pake uwanjani. Lakini kupitia Azam TV,
watu zaidi ya milioni tano wataangalia mechi hiyo.
Kwa wadhamini ambao wanataka kujitangaza
wangekuwa kutoa matangazo na kuweka pale uwanjani na kuyalipia. Lakini hakuna
mtu hata mmoja kutoka Simba au Yanga aliyejaribu kufanya hivyo ili kuongeza
kipato.
Hiyo ni fursa ambayo inaanchwa ipite
kimyakimya huku viongozi wa Yanga na Simba, zaidi wakiangalia ushindi pekee ili
wapate sifa na kukubalika kwa wanachama wao.
Klabu hizi zinaendeshwa kisiasa sana,
ndiyo maana timu zake mara kwa mara zimekuwa zikilalama kuhusiana na fedha iwe
ya kambi au vinginevyo, lakini mirija ya kupata fedha na kumaliza matatizo hayo
imefinywa na viongozi wenyewe.
Wiki mbili nzima, gumzo la Simba dhidi
ya Yanga lilikuwa juu, lakini hakuna hata kiongozi mmoja alifikiri namna timu
hizo zinaweza kuingiza fedha za ziada zaidi ya zile za mapato ya uwanjani.
Nawaambia lakini hamtaki kukubali,
kwamba viongozi wengi wamekuwa na mawazo yaleyale tokea akina Abdallah Kibadeni
na Gibson Sembuli wakicheza soka.
Kwamba vipi waende kwa waganga, kambi
ilindwe, nani atupiwe lawama kama mchawi iwapo atashindwa na kadhalika.
Aghalabu kwao kusikia wanazungumzia
kuhusiana na uingizaji wa fedha, mbaya zaidi wanataka kuwa kama Manchester
United, Real Madrid, Barcelona na timu kubwa nyingine za Ulaya.
Hakika ni ndoto za mchana, badala yake
viongozi wabadilike na vizuri waamini Yanga na Simba ni timu na zina uwezo wa
kutengeneza fedha nyingi zaidi kwa kuingiza kila moja zaidi ya Sh milioni 300
na hasa zinapokutana.
Mechi yao ni biashara kubwa, lakini
kutokana na walivyolala, kila Yanga na Simba zinapocheza, wako wanaotajirika na
kuingiza mamilioni. Umasikini unabaki umeziganda klabu hizo kubwa ambazo ukubwa
wao ni jina, ndani ya mfuko, hohehahe!
mimi ni msomaji wako maarufu tulikutana getini Taifa, nakupa moyo uendelee kutuhabarisha,
ReplyDelete