November 25, 2013


Na Saleh Ally
Sakata la kamati ya utendaji limeendelea kuchukua sura mpya kila kukicha na jana mwenyekiti aliyesimamishwa, Ismail Aden Rage amejitangaza upya kuendelea na nafasi yake.


Lakini wajumbe wa kamati ya utendaji wameendelea kushikilia msimamo wao kutokana na kikao walichokaa kwamba wao wamemsimamisha mwenyekiti huyo.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lililomtaka Rage kuitisha mkutano ndani ya siku 14 na yeye jana akatangaza kukaidi, limesema litasubiri barua yake halafu liifikishe kwenye kamati ya utendaji.

Kwa kifupi, Simba bado hakujatulia na Rahma Al Kharusi ambaye alikuwa mjumbe wa kamati ya utendaji na kuamua kujondoa anasema amekubali kuitumikia nafasi yake mpya aliyoteuliwa.
Lakini anasisitiza iwapo hali ya migongano isiyokwisha ndani ya klabu hiyo itaendelea, basi yeye atajiondoa kabisa.

“Niko mbali na ninabanwa na kazi zangu za kibiashara, lakini nimekuwa nikikerwa sana kutokana na mambo yanayotokea ndani ya Simba.

“Mambo haya ya migogoro si kitu cha kuendelea kukipa nafasi halafu tukaona ni mambo ya kawaida, badala yake tuyakemee.

“Mimi niliamua kujiondoa Simba kabisa, nilifanya hivyo kwa kuwa ninaona kama tunapoteza muda na ugomvi na malumbano yanachukua nafasi yetu ya maendeleo. Niliamua kujiondoa lakini nimezungumza na Rage kwa mara nyingine kaniomba tena nibaki na kuisaidia Simba.

“Nabaki kwa kuwa nina mapenzi na klabu na watu wake, sasa nimeteuliwa kuwa mjumbe wa bodi ya wadhamini. Hii itanisaidia kutoingia katika mikutano mingi na badala yake zaidi nitafanya kazi ya kulinda maslahi na mali za Simba.

“Lakini kama bado migogoro itaendelea, kweli nitaondoka mara moja na kuendelea na biashara zangu kwa kuwa hata zenyewe bado zinahitaji muda wangu,” anasema milionea huyo mwanamke ambaye ni mmiliki wa makampuni ya RPB Group.

Alipoulizwa kama anaunga mkono upande upi kati ya ule wa Rage na kamati ya utendaji, Malkia wa Nyuki anasema:

“Mimi nabaki kuwa kiongozi wa Simba nisiyekuwa na upande, siwezi kujua hata tatizo hasa ni nini kwa kuwa niko mbali kama nilivyokueleza. Lakini jambo la muhimu ni kuangalia maendeleo ya klabu.

“Yoyote anayetaka maendeleo ya klabu ndiye tunafanya naye kazi, angalia suala la Sunderland tumelishughulikia na limefikia pazuri, lakini inaonekana halipewi kipaumbele kwa kuwa halina maslahi binafsi.

“Wako wanaoangalia maslahi yao binafsi na si klabu, hawa wanakosea na lazima tukubali Simba ni ya watu wengi na tunaopewa nafasi ya kuongoza ni dhamana tu. Lazima tuitumikie klabu na kuwasaidia Wanasimba badala ya kuiangamiza.

“Kweli naipenda Simba, lakini nasisitiza malumbano yasiyokuwa na msingi yakiendelea, mara moja nitaondoka kwa kuwa hakuna faida ya kubaki hapo,” anasema Malkia wa Nyuki.
Mwanamama huyo aliwahi kumwaga zaidi ya Sh milioni 80 kuisaidia Simba kuweka kambi nchini Oman kwa siku 15, baada ya hapo akatoa zaidi ya Sh milioni 36 kuisaidia Simba kulipa deni la Kocha Milovan Cirkovic ambaye uongozi wa Rage ulikuwa umeshindwa kumlipa.
Kama hiyo haitoshi, alilipa deni la Simba iliyokuwa inadaiwa mjini Arusha. Malkia wa Nyuki alitoa Sh milioni 15 kwa mmiliki wa hoteli ambaye alikuwa amezuia basi la Simba.
Halafu siku hiyohiyo akatoa zaidi ya Sh milioni 15 na kupunguza deni kwa wachezaji waliokuwa wanaidai klabu hiyo chini ya uongozi wa Rage.
Lakini siku chache baadaye aliamua kukaa kimya hadi alipofanya mahojiano, jana na Championi Jumatatu akisisitiza suala hilo la migogoro kumalizwa, la sivyo atajiondoa zake.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic