*Yanga,
Simba zamvutia lakini ashindwa kuchagua aipende ipi
*Asisitiza
kama vipi, bora ziwe zinatoka sare kila mechi
Na Saleh Ally
DUNIA ina maajabu yake ndiyo maana
wakasema, “tembea uone”. Katikati ya Jiji la Dar es Salaam, binadamu ameamua
kuishi ndani ya handaki kwa miaka saba sasa.
Chacha Makenge (36), ameishi katika
handaki lililo katika eneo la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwa kipindi
chote hicho na hana hofu na maisha yake ni mazuri tu.
Makenge ambaye alikuwa anajulikana
kama Kadogo Charles wakati akiwa mtoto, aliamua kubadili jina hilo kwa madai
sasa ni mtu mzima. Makala yake ya kwanza kuhusiana na maisha yake hayo,
yaliandikwa na gazeti kongwe la Uwazi.
Pamoja na mfumo huo wa maisha,
Makenge baba wa mtoto mmoja ni shabiki mkubwa wa timu ya Chelsea ya England
ambayo inanolewa na Kocha Jose Mourinho.
TUKIWA NDANI YA HANDAKI |
AKINIONYESHA KISANDUKU CHA HUDUMA YA KWANZA |
VYAKULA, ULEZI, UFUTA NA KARANGA |
Ushabiki wake wa soka ulitokana na kushawishiwa
na rafiki yake aliyekuwa akiitwa Benny, baada ya hapo ameamua kuishabikia timu
hiyo pekee.
“Naifutilia Chelsea pekee yake,
napenda kuwaona wanacheza. Uchezaji wao ni tofauti kidogo, naweza kusema
wanalingana na wachezaji wengine wa Ulaya. Hata kama wanakuwa hawana mpira
lakini bado utaona wako karibu na wanafuatilia kinachofanyika.
“Hakuna anayesimama na kubaki sehemu
moja tu akisubiri hadi mpira umfikie. Ingawa nilishawishiwa na rafiki yangu,
baadaye nikajikuta naipenda timu hiyo. Sijawahi kuwa shabiki wa wachezaji
fulani badala yake napendelea zaidi uchezaji na mafanikio ya timu.
“Kila ninapoangalia mpira lazima
nifaidike na kujifunza, mfano kinachonivutia katika mchezo wa soka zaidi ni
suala la ushirikiano katika timu. Watu wanapiga pasi, zinafika. Maisha
yanatakiwa yawe hivyo, watu wapasiane mambo ili kutengeneza kitu kimoja kwa
faida ya wote.
“Soka ndiyo mchezo ninaoupenda zaidi
kama nitaamua kuzungumzia michezo. Ingawa mpira wa hapa nyumbani huwa
haunivutii sana,” anasema Chacha.
Alipoulizwa kuhusiana na Yanga na
Simba, anasema: “Kwanza nikuambie sijawahi kwenda kuangalia mpira Uwanja wa Taifa,
sitaki kuwa mshabiki wa upande mmoja lakini napenda kufuatilia nani amefungwa
zinapokutana. Mfano nilisikia Simba imeifunga Yanga mabao 3-1, bahati mbaya
nikawa sijauangalia.
“Siwezi kuuchambua kwa kuwa sikuuona.
Lakini bado ningependa timu hizo ziwe zinatoka sare kuepusha tafrani na
ikitokea sare basi wawe wameifanyia kazi kweli. Wacheze mpira unaoonekana na
atakayezembea, basi afungwe.”
Lawama:
“Mimi sina mchezaji anayenivutia
sana, napenda kuwaona watu wakiwa sawa, siangalii jina la mtu, naangalia
aliyefanya kazi. Ingawa naweza kushauri kwa wale wanaolaumu sana ikitokea timu
zao zimefungwa basi wajaribu kuangalia kwanza mazingira.
“Inawezekana maandalizi hayakuwa ya
kutosha, hakukuwa na nidhamu katika maandalizi na hili ni tatizo kubwa. Unajua
mwili ukiutumia vibaya pia ni tatizo, hauwezi kuwa katika hali nzuri na kukupa
matokeo mazuri,” anasema Chacha.
Makazi yake:
Makazi yake yako kando ya barabara ya
Sam Nujoma upande wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na anaishi mwenyewe tu
kwa kuwa alishatengana na mkewe.
Chacha anasema mkewe amekuwa akishangaa
kila anapokwenda katika eneo analoishi na wakati mwingine anadhani
amechanganyikiwa.
“Kwa kuwa niliwahi kuzushiwa
nimechanganyikiwa, nikafikia hadi kulazwa kwa nguvu hadi nilipoweka mgomo wa kula,
basi mkewe wangu hudhani kweli bado naumwa kitu ambacho si sahihi. Mimi ni
mzima wa afya kabisa,” anasema.
Eneo analoshi lina ukubwa wa
takribani mita 500. Ametengeneza barabara nzuri kwenda kwake na ameigawa mara
mbili kama ilivyo Sam Nujoma Road. Maana ina upande wa kushoto na kulia na
katikati kuna majani ambayo yametenganisha.
“Ukiwa hapa upande huu ni wa kwenda
na huu ni wa kurudi, ni kama zilivyo barabara nyingine tu,” anasema.
Msikiti&Kanisa:
Kuna sehemu ambayo amekwangua majani na inatumika kama msikiti na nyingine kama kanisa.
"Natembelewa na watu wa imani tofauti, hivyo atakayetaka kuabudu atachagua kwenda msikitini au kanisani," anasema akizionyesha sehemu hizo.
Ulinzi:
Kabla ya kuifikia barabara hiyo,
unalazimika kuyapita majani yaliyotengenezwa vizuri kama geti na ukivuka tu
unakuta kiti kilichotengenezwa kwa ubunifu kwa kutumia majani.
“Hii ni sehemu ya ulinzi shirikishi,
wakati mwingine nalazimika kukaa hapa na kulinda. Ninafanya ulinzi shirikishi.”
TUNATOKA NJE YA HANDAKI.. |
TUNASHIRIKIANA KUFUNGA MLANGO.. |
Ujenzi:
“Niliijenga kwa miezi saba, ilikuwa
ni taratibu na nimekuwa nikiliboresha eneo hili kila kukicha hadi kufikia hapa.
Hakukuwa na ramani badala yake ni ubunifu wangu tu. Kabla ya kuchimba handaki
nilikuwa nikilala nje tu (anaonyesha sehemu).”
Kitabu:
Unapofika kwake kuna kitabu kwa ajili
ya wageni kama ilivyo katika sehemu mbalimbali maarufu ambayo wageni hulazimika
kusaini wanapotembelea.
“Nimekuwa na wageni wakiwemo watu
maarufu. Hivyo nimeandaa kitabu ili wasaini kwa ajili ya kumbukumbu hapo
baadaye,” anasema.
NIKIMZAWADIA MPIRA HUKU MAKONGORO OGING AKISHUHUDIA.. |
TUKITOKA NJE YA GETI LA ENEO HILO |
Ndani:
Ndani ya handaki kuna kitanda kimoja
kidogo usawa wa urefu wa futi nne na upana futi moja na nusu. Sehemu maalum ya
kuhifadhi vitamu, mafaili, magazeti, vyakula na kopo la huduma ya kwanza.
Wanaweza kuingia hadi watu kumi na
kukaa kwenye ngazi. Lakini kuna nyuki wa aina zaidi ya nne ambao wanazunguka
mule ndani.
“Mimi nimewazoea na hawawezi kuniuma,
unajua nao ni viumbe na hawana matatizo kabisa na mimi na tumekuwa tukiishi
pamoja,” anasema Chacha.
Lakini anapolala, kawaida hafungi
mlango na siku zote hana hofu na wanyama hata kidogo kwa kuwa ameishi miaka
saba bila tatizo hilo.
“Kufunga kwangu labda kuwe na mvua au
nikiwa natoka,” anasema na baadaye kuonyesha mlango wa majani na miti ambao
hutumika kufunga.
Kwake hakuna taa ya aina yoyote na
wala hataki kibatari, hivyo ikifika usiku ni kiza kinatawala naye anaona sawa.
“Macho yanafanya kazi mchana kutwa
kwenye mwanga, unapofika usiku vizuri kuyaacha kwenye giza yajijenge upya. Kama
kuona nafanya hivyo kwa hisia,” anasisitiza.
Chakula:
Anakula vyakula kadhaa kama ulezi,
ufuta na vinginevyo. Lakini mara moja moja anaweza kwenda kununua vyakula
katika maduka yaliyo kwenye jengo la kibiashara la Mlimani City ambalo liko
karibu kabisa na anapoishi.
“Ninapokwenda Mlimani City kununua
vitu, kodi inanikera sana. Maji ya shilingi mia tisa, nalipa kodi zaidi ya
shilingi 150. Swali langu hawa jamaa nao wanalipa kodi, au wao wanasubiri
waniuzie mimi ndiyo inakuwa kodi waliyolipa.
“Kama wanalipa, vipi kwenye lisiti
inaonyesha kodi niliyolipa mimi tu. Wao wamelipa wapi na kwa nini isionyeshwe.
Nimesikia kodi ya simu imefutwa lakini maji bado tunalipishwaa kodi kubwa sana.
Hii ni ajabu!”
Uamuzi wa Chacha kukaa katika eneo
hilo ulitokana naye kuchomewa nyumba yake na rafiki yake aliyekuwa amempa eneo
kwa ajili ya kujenga.
Rafiki yake huyo kwa mujibu wa Chacha
alichoma nyumba yake wakati akiwa mahabusu katika kituo cha Polisi cha
Sitakishari.
Baadaye akafikishiwa mahakamani kwa madai ya kuwashambulia watu
waliomvamia usiku na akahukumiwa jela miezi tisa hadi alipotoka kwa msamaha we Rais
Kikwete Desemba 10, 2009.
“Nikaamua kuepuka majungu na tafrani
za wanadamu, baada ya kutoka jela niliendelea na kazi zangu za sanaa za mikono
lakini nikatafuta sehemu yenye utulivu ikiwa ni pamoja na kuchimba handaki kama
nyumba yangu, sasa naishi kwa amani,” anasema Chacha.
0 COMMENTS:
Post a Comment