Na
Saleh Ally
Kumekuwa
na maswali mengi sana kuhusiana na timu zetu za taifa, kwani kila mashindano
tumekuwa tunajivunia suala la afadhali na inaonekana wengi tumeridhika nalo.
Wakati
timu ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars, inakwenda Kenya kushiriki Michuano ya
Kombe la Chalenji, hakika nilikuwa nina asilimia 90 kwamba ndiyo yenye nafasi
ya kutwaa kombe hilo, nitakupa sababu.
Katika
timu zote zilizoshiriki michuano hiyo ambayo imefikia tamati jijini Nairobi,
Kili Stars ndiyo ilikuwa na kikosi bora zaidi kuliko nyingine, takwimu zinasema
hivyo kwa maana ya vikosi.
Zambia
ambao walikuwa wageni, kikosi chao ambacho hushiriki michuano iliyo chini ya
Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) na lile la Afrika (Caf), kilikuwa kimevunjwavunjwa.
Yaani waliotumika, wengi ni wageni.
Sudan
pia ilifanya hivyo na hata wenyeji Kenya pia ilikuwa hivyo. Mfano ingekuwa ni
michuano ya kuwania kufuzu kucheza Kombe la Dunia au Mataifa Afrika, basi
asilimia 80 ya wachezaji walioshiriki Kombe la Chalenji isingekuwepo.
Badala
yake wachezaji kama akina McDonald Mariga, Victor Wanyama, Denis Oliech, Jamal
Mohamed na wengine wanaocheza nje ya Kenya, ndiyo wangechukua nafasi.
Kadhalika
Uganda, kocha wao, Sredojevic Milutin ‘Micho’, aliamua kuwaita wachezaji
wanaocheza Uganda tu huku akichukua wawili kutoka nje ambao ni Hamis Kiiza wa
Yanga na Dan Sserunkuma wa Gor Mahia ya Kenya.
Micho
aliacha rundo la wachezaji wa nje kwa kuwa anataka kuboresha kikosi cha Chan
mwakani huko Afrika Kusini. Ethiopia pia waliamua kuchukua wachezaji wengi
vijana kwa lengo la kutengeneza kikosi chao upya. Waliokwenda na vikosi vyao
kamili ni Somalia, Kili Stars na Zanzibar Heroes.
Hapa
kitu cha kujiuliza ni hiki, kama Kili Stars ilikwenda na kikosi kwa asilimia 95
ambacho kinaunda timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, vipi kimeshindwa
kufurukuta dhidi ya vikosi vya pili au vya vijana vya wenzetu?
Taifa
Stars imekuwa ikizitoa jasho na ikiwezekana kuzifunga Zambia, Uganda, Kenya
tena zikiwa na wachezaji wake wa kikosi cha kwanza ambao wengi hawakuwepo
Nairobi.
Kama
ni tathmini, kikosi cha Kili Stars ndiyo kilikuwa bora zaidi kuliko vingine,
lakini mwisho kimeishia nusu fainali na kufungwa na wenyeji ambao walikuwa na
wachezaji wengi ambao hawana nafasi kama akina Mariga wakiwa wameitwa kujiunga
na timu hiyo.
Hata
ukiangalia au ukapima mchezaji mmoja-mmoja na rekodi za mashindano makubwa,
yaani yale ya klabu na timu za taifa chini ya Caf, basi hakuna timu iliyokuwa
na wachezaji wenye uwezo kama wale wa Kili Stars.
Ninaona
kuna tatizo na linaweza likatokea katika moja ya pande hizi mbili, kwa
wachezaji au Kocha Kim Poulsen ambaye nafikiri huu ndiyo ulikuwa wakati mwafaka
kwake kufunguka, maana Tanzania kuendelea kubahatisha sasa imekuwa ‘too much’.
Najua
Poulsen na wenzake wanalipwa kwa ajili ya kuitumikia Taifa Stars, hakuna kati
yao anayeweza kusema anafanya kazi ya kujitolea. Kikubwa kinachotakiwa ni
mafanikio na hakuna zaidi ya makombe au kufuzu kucheza michuano mikubwa kama
Kombe la Dunia au Mataifa Afrika, ikiwezekana hata Chan.
“Mambo
ya ilibaki kidogo tu”, sasa basi. Kama itaendelea basi wakati wa kufunguka na
kumhoji Poulsen bila ya woga utafika na hakutakuwa na breki wala woga, muhimu
zaidi, maslahi ya taifa mbele.
Ndiyo
maana nasema umefika wakati kwa Poulsen kufunguka, kama anaona kuna tatizo,
kuna wachezaji wavivu, wasiomsikia, wasiotaka kujituma kwa ajili ya taifa lao,
basi awe wazi na afunguke mara moja.
Inawezekana
kuna mambo yanaendelea chinichini, labda kuna mgomo baridi, au kuna wachezaji
viburi waliovimba vichwa, basi Poulsen aseme na mara moja washughulikiwe ili
wajue maana ya utaifa na umuhimu wa kuichezea timu ya taifa.
Lakini
kama atathibitisha hakuna tatizo, basi yeye ndiye atakuwa na tatizo na kama
ameshindwa kulitatua, basi mara moja Mtanzania mimi nitaanza kulitatua na
kutaka mabadiliko.
Kama
wapo wanaoona ni sahihi timu kila siku kubakiza kidogo tu kufuzu au kuchukua
kombe na wanaacha mambo hayo yaendelee, basi sasa wakati umebadilika na
umekwisha, maneno na visingizio sasa basi, tunataka mafanikio.
FIN.







0 COMMENTS:
Post a Comment