Kumekuwa na tabia ya makocha wengi kuwa
rafiki wa kila mmoja, kuanzia wachezaji, viongozi na hata waandishi wa habari
kila wanapokuwa katika kazi zao.
Nasema kazi zao nikimaanisha wakati
akiwa ndiye kocha, tena anajulikana au kukubalika na watu wote mfano wa watu
hao niliowataja.
Lakini ikitokea kocha huyo akaondolewa
au kufutwa kazi, basi anapoteza watu wengi sana kwa muda mfupi na wanakuwa
hawamjali kabisa!
Soka ni mchezo wa watu wengi wenye tabia
ya kuwajali watu pale wanapoamini wanaweza kuwapa furaha tu lakini inapokuwa
vingine, basi hawajali kwa lolote lile.
Mifano iko mingi, tumeona wachezaji
wanapoumia, viongozi wa timu nyingi wamekuwa wakiwakimbia na kuonyesha
kutowajali bila ya hofu hata kidogo. Ilimradi wanajua hawawezi kutimiza raha
yao ya kuwaona wanacheza katika kipindi hicho.
Hiyo haitoshi, tumeona inapotokea
wachezaji au makocha wanapokuwa wamelazwa, ni watu wachache sana wamekuwa
wakionyesha upendo na ubinadamu kwao. Wengi wamekaa kando na kuamini hawahusiki
hata kidogo.
Maana yake watu wanaopenda mpira au wale
wanaojiita watu wa mpira, wanawapenda wale wanaowapa raha yao ya kuisaidia timu
wanayoipenda ishinde tu, wakiugua au kufukuzwa basi urafiki unakufa.
Huu unaweza kuwa ni mfano, lakini mifano
niliyoeleza inaweza kuwa msingi wa kumkumusha na kumsuta kila anayeona
anahusika na anaweza kubadilika, ikishindikana, basi sawa, kila mtu ana haki ya
kuchagua.
Tuachane na mifano, tukumbushane
kuhusiana na makocha. Yanga imetangaza kumuacha Ernie Brandts, lakini taarifa
zilizopo amekuwa akihaha huku na kule na imeelezwa anabembeleza ikiwezekana
alipwe fedha zake ili aondoke.
Yanga imekubali kumlipa lakini baada ya
siku 30, kweli inafuata mkataba lakini kama itamlipa halafu aondoke, maana yake
itakuwa imepunguza bugudha, pia itampa nafasi ya kuondoka na heshima yake.
Mambo ya kuonekana anaranda kwenye mitaa
ya jiji, mara akitakiwa kwenda mazoezini, au achague mwenyewe nafikiri si
sahihi.
Kuna taarifa pia amekuwa akiranda kwenye
ofisi za Yanga akitaka mkataba wake alionao usainiwe ili aweze kuwadai Yanga
vizuri na kila akienda hapati ushirikiano na anaondoka zake, pia si sahihi.
Tuliona wakati huo makocha wa Simba kama
Milovan Cirkovic kutoka Serbia na Patrick Liewig raia we Ufaransa
walivyosumbuka wakiendelea kubaki Dar es Salaam kudai fedha zao.
Yanga inaweza kujitofautisha katika hilo
na kufanya mambo yaende tofauti kwa kuwa ni vizuri sana kukumbuka kwamba
Brandts anastahili heshima kwa aliyoyafanya Yanga.
Hata siku moja hakuwahi kulaumiwa kwa
uzembe, badala yake kila kukicha aliifanya kazi yake kwa juhudi na aliweza
kuipa timu hiyo kombe.
Kama tatizo ni kuifunga Simba, pia
aliwahi kufanya hivyo na atabaki kuwa mmoja wa makocha walioifundisha Yanga kwa
mafanikio na kujenga kikosi bora kilichokuwa kinapiga soka safi, hilo
halikwepeki.
Hivyo ni vizuri sana kuonyesha pamoja na
kuonekana kwamba ameshindwa kwa sasa, basi heshima na thamani yake isishuke
kutokana na kufungwa mechi moja tu.
Kama uongozi we Yanga umeona ni sahihi
kuachana naye, vizuri ukamalizana naye mapema, pia ukatofautisha uvunjani wa
mikataba wa makocha na watu wa ofisini. Hivyo umlindie heshima ili aondoke
salama.
Heshima mara nyingi inasimama kwenye
thamani au kukumbuka mazuri ya kitu au mtu. Yanga bado wanapaswa kukumbuka kazi
kubwa ya kocha huyo, basi wamalizane naye vizuri, mapema na aende zake salama
salimini.
Fin.
0 COMMENTS:
Post a Comment