Timu ya soka ya waandishi wa habari za
michezo nchini, Taswa FC kesho itapambana na timu inayoundwa na wanamuziki wa
bendi ya African Stars (Twanga FC) katika mechi malaum ya kukaribisha mwaka
mpya.
Mechi hiyo imepangwa kwenye viwanja vya
Leaders Club inatarajia kuwa na msisimko wa aina yake ambapo baada ya mechi
hiyo, bendi ya African Stars itatumbuiza jukwaani kwa mujibu wa Mwenyekiti wa
Taswa FC, Majuto Omary.
Majuto alisema kuwa mechi hiyo itaanza
saa 7.00 mchana ili kutoa nafasi kwa wanamuziki wa Twanga pepeta kupanda
jukwaani kutumbuiza nyimbo zao mbali mbali ikiwa pamoja na mpya mbali mbali
zitakazosikika kwa mara ya kwanza.
Alisema kuwa wameamua kucheza na Twanga
Pepeta kutokana na ushindani uliopo ambapo katika mechi ya mwisho, Taswa FC
ilishinda kwa mabao 3-1.
Alisema kuwa ushindani wa timu hizo mbili ndiyo
umepelekea kufanyika kwa mechi hiyo ambapo awali, timu ya kombaini ya Jogging
itapambana na timu ya makempu ya Twanga Pepeta.
Meneja wa Twanga Pepeta, Hassan Rehani
alisema kuwa kiburudani wamejiandaa vizuri na wanamuziki wake wamepania vilivyo
kuanza mwaka vyema ili kutoa burudani ya aina yake.
“Hii ni sehemu ya zawadi ya
mwaka mpya na wanamuziki wamepania kupiga nyimbo zote zilizotamba mwaka 2013 na
pia watakaribisha maombi maalum ya nyimbo kutoka kwa mashabiki.
“Tuna albamu nyingi na nyimbo kibao
zilizotamba, hivyo ni wakati wa mashabiki kufanya kile wanachokitaka kutoka
katika bendi yetu, wamepewa fursa hiyo nasi tupo kambili kutimiza maombi yao,”
alisema.
0 COMMENTS:
Post a Comment