Mabingwa wa soka Tanzania Bara, Yanga wanatarajia kushuka dimbani
leo kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Altay SK ya Uturuki.
Yanga ipo Uturuki ambapo imeweka kambi
ya wiki mbili kwa ajili ya kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania
Bara pamoja na michuano ya Klabu Bingwa Afrika.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Abdalah Bin Kleb, alisema kikosi cha
timu hiyo kinaendelea vizuri nchini Uturuki na kesho (leo) kinashuka dimbani
kucheza mechi ya kirafiki ikiwa ni muendelezo wa kujipima nguvu.
“Kikosi kipo vizuri kwa jinsi
nilivyowasiliana nao na kesho Jumatano wanatarajia kucheza mechi moja ya
kirafiki na Altay SK ili kuangalia upungufu kwenye timu yetu.
“Tunaamini kikosi kitakuwa bora zaidi
pindi kitakapowasili nchini mara baada ya kurejea kutokana na mechi
wanazotafutiwa kujipima nazo na wachezaji wanaonyesha kujituma zaidi katika
mazoezi,” alisema Bin Kleb.
Yanga inatarajia kucheza mechi tatu za
kirafiki ikiwa nchini humo. Katika mechi ya kwanza, Yanga ilishinda mabao 3-1
dhidi ya Akara Sekerspor.
Yanga inatakiwa kurejea nchini kabla ya
Januari 25 ambapo itafungua pazia la mzunguko wa pili kwa kucheza dhidi ya
Ashanti.
0 COMMENTS:
Post a Comment