Chelsea imeonyesha mpira uko tofauti
siku zote na wengi wanavyoamini kwa kuichapa Man City kwa bao 1-0 ikiwa kwao
Etihad jijini Manchester.
Bao la Chelsea katika mchezo huo
lilifungwa na beki wake wa kulia Branislav Ivanovic ambaye aliukuta mpira
unaelea baada ya Ramirez kupiga shuti lililowababatiza mabeki wa Man City, naye
akautupia kambani kiufundi utafikiri mshambuliaji.
Katika mechi hiyo ya Ligi Kuu England iliyomalizika punde,
kocha Jose Mourinho wa Chelsea ameingia vyumbani haraka hata bila ya kumsalimia
Pellegrini hali iliyoonyesha kuwa amechanganyikiwa na furaha ya ushindi wa
mechi hiyo.
Pamoja na ushindi huo, Chelsea
imeendelea kubaki katika nafasi ya tatu, ikiwa na pointi 53 sawa na Man City
lakini tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa yanawabakiza vijana hao wa
Manuel Pellegrini katika nafasi ya pili.
Arsenal ambayo jana iliichapa Crystal
Palace inabaki katika nafasi ya kwanza ikiwa na pointi 55, hivyo kufanya
ushindani kuwa mkubwa zaidi kwa timu tatu hizo ingawa Liverpool yenye pointi 47
si ya kuidharau.
Katika mechi ya leo, Chelsea ndiyo
ilipoteza nafasi nyingi huku ikionyesha soka tofauti la kushambulia kwa ‘kaunta
atak’ tofauti na wengi walivyotarajia kuwa itapaki basi ili kuzuia kasi ya
upigaji mabao ya Man City.
Kama washambuliaji wa Chelsea wangetulia
kidogo tu, basi wangekuwa na uwezo wa kufunga hata mabao mengine angalau mawili
na kupata ushindi mzuri zaidi ya huo wa 1-0.
0 COMMENTS:
Post a Comment