Na Saleh Ally
JOSE Mourinho aliwaambia mashabiki wa Chelsea kuwa kikosi chake kitaibuka na ushindi katika mechi dhidi ya Manchester City, usiku wa kuamkia jana kwenye Uwanja wa Etihad jijini Manchester.
Kweli ameweza hilo, tena huku Chelsea ikionyesha kiwango kikubwa na kuwashangaza wengi walioamini tofauti hapo awali.
Chelsea imeifunga Man City na kuvunja rekodi ya kutofungwa nyumbani msimu huu, kwani ilikuwa imeshinda mechi 11 ndani ya Etihad, dhidi ya Chelsea ilikuwa ya 12, mambo yakawa magumu.
Kabla ya mechi hiyo, mvuto ulikuwa kwa wachezaji, nani atacheza na yupi ni hatari. Lakini wako waliamini Man City haifungiki huku wakiwa wamesahau kwamba ililala kwa mabao 2-1 ndani ya Stamford Bridge jijini London.
Chelsea iliyocheza kwa mfumo wa ushirikiano wa pamoja kama mbwa mwitu iliingia uwanjani ikiwa tayari inaongoza kwa pointi tatu dhidi ya Man City na ujuzi wa Mourinho ukamuondoa kwenye reli Manuel Pellegrini raia wa Chile.
Pellegrini na Mourinho wamekuwa na upinzani mkubwa, chanzo ni maneno ya Mourinho wakati alipotua Real Madrid. Waandishi walipomuuliza kwamba hahofii presha ya timu hiyo, jibu lake lilimlenga Pellegrini ambaye alikuwa ametoka Madrid na kutua Malaga.
“Presha ipo kila sehemu, lakini siku nikifukuzwa hapa, sitakwenda Malaga. Nitajiunga na timu nyingine kubwa,” Mourinho alijibu ikionekana dongo kwa Pellegrini na uadui ukaanzia hapo.
Wakati Malaga ailipoifunga Madrid, Pellegrini naye aliponda na kusema walistahili kushinda kwa kuwa wapinzani wao wanacheza vururu tu.
Mourinho alipoingoza Chelsea kuifunga Man City 2-1, pale Stamford Bridge, Pellegrini alisusa kumpa mkono Mourinho na kuingia zake vyumbani, baadaye ilielezwa kuwa alikerwa na maneno yake kabla ya mchezo.
Lakini jana Mourinho naye amelipa, baada ya mechi aliruka juu kushangilia, akapongezana na watu wake wa benchi la ufundi na baadhi ya wachezaji, halafu huyoo akaingia zake vyumbani.
Rekodi ya Pellegrini wakati akiwa Real Madrid inaonyesha aliwahi kufikisha pointi 96 kwa msimu, lakini pointi nyingi zaidi za Mourinho ni 100.
Hii inaonyesha vita ya mechi hiyo ilikuwa kali zaidi kwa makocha hata kuliko kwa wachezaji na bado Mourinho. Kingine ambacho Mourinho amewahi kumtambia Pellegrini kuwa wakati akiwa Real Madrid alishindwa kuzima utawala wa Barcelona kama alivyofanya yeye.
Pellegrini aliwahi kukanusha kuwa hana matatizo na Mourinho, lakini hilo halifuti hali halisi kati ya makocha hao wawili ambao kila mmoja alipania kumfunga mwenzake na alitaka kuonyesha ubora kwa wenzake.
Kiufundi Mourinho alikuwa bora zaidi, kitu ambacho amethihirisha tokea Real Madrid kama utalinganisha makocha hao.
Lakini usiku wa kuamkia jana alijua madhara mafowadi Edin Dzeko na Álvaro Negredo kuwa ni wakubwa na wenye uwezo wa kufunga mabao ya vichwa.
Fanya tathmini ya mchezo huo, vichwa vingi wamepiga mabeki John Terry, Gary Cahill na David Luiz ambao Mourinho alijua ni warefu, wana maumbo makubwa na wanaweza kupambana nao.
Lakini akampanga kiungo mgeni Nemanja Matic ambaye alijua ana uwezo mkubwa wa kuwavuruga na ndiye alitoa pasi nyingi za ‘counter attack’ kwa akina William na Hazard na kama Chelsea wangekuwa makini zaidi, basi wangepata hata mabao matatu.
Kiuchezaji, Pellegrini alibadilisha mfumo na kutumia 4-4-2 badala ya 4-3-2-1 huku Mourinho akibaki na mfumo huo ambao uliwapa ugumu Man City na walipobadili, tayari walikuwa wamechelewa.
Yaya Toure ndiye alijitutumua zaidi kwa viungo, lakini bado wingi wa viungo wa Chelsea waliokuwa wakicheza kama mbwa mwitu kutokana na ushirikiano wao, ukawa ni ugumu kwake.
Utaona walivyokuwa wanamgombea kumkaba kama mbwa mwitu wanapambana na Simba aliyegoma kukaa ili aliwe nyama.
Mechi hiyo ilikuwa burudani kubwa, ilitazamwa na mashabiki wengi wa soka hata hapa nyumbani, ingawa ilikuwa saa tano usiku, watu hawakukubali kulala na kuikosa na ilikuwa burudani ya kweli yenye mafunzo.
0 COMMENTS:
Post a Comment