February 3, 2014




Na Saleh Ally

ASILIMIA kubwa ya wachambuzi na hata hisia za mashabiki wa soka kuanzia nyumbani Tanzania na kwingineko England na duniani kote, wanaamini Manchester City itashinda mechi ya leo ya Ligi Kuu England dhidi ya Chelsea.


Mechi ya leo kwenye Uwanja wa Etihad ni ngumu na kila upande una hofu, maana hapakaliki.

Soka linakwenda kwa takwimu, lakini kuna wakati mambo yanakuwa tofauti na zinashindwa. Hivyo bado Chelsea pia ina nafasi ya kushinda mechi hiyo ya ugenini, lakini kweli kazi wanayo.

Kuonyesha kuwa mechi hiyo itakayopigwa kwenye Uwanja wa Etihad si laini kwa timu zote, ni nafasi ya timu zote tatu kwenye ligi.
Baada ya kushuka dimbani mara 23, Manchester City inaongoza ikiwa pointi 53 halafu Chelsea iko katika nafasi tatu ikiwa na pointi 50, ikiwa imecheza mechi sawa na za wenyeji wake.

Maana yake ni timu ambazo uwezo wao haupishani sana na inawezekana kila moja ikawa ina nafasi ya kushinda ingawa asilimia 60 zinakwenda kwa Manchester City na 40 zinabaki kwa wageni Chelsea.

Mechi nane:
Bado Manchester City wanapewa nafasi kutokana na kuwa mechi zao nane zilizopita zote wameshinda.
Katika mechi nane zilizopita upande wa Chelsea, pia hawajapoteza lakini wana sare mbili ikiwemo mechi iliyopita ambayo walikipiga na West Ham United, pamoja na kushambulia lakini bado walimaliza dakika 90 kwa suluhu.

Inaonyesha timu zote zina uwezo wa kufunga mabao zaidi ya mawili katika mechi moja lakini Manchester City inapewa nafasi kubwa kutokana na uwezo wake wa kufunga mabao mengi katika mechi moja.

Vikosi:
Vikosi vya timu hizo havitakuwa na tofauti kubwa sana, lakini majeraha ya baadhi ya wachezaji ndiyo yatawalazimisha makocha Manuel Pellegrini na Jose Mourinho kubadilisha mambo kadhaa.

Manchester City itamkosa Kun Aguero ambaye ni majeruhi, sawa na Chelsea ambayo inalazimika kucheza bila Fernando Torres ambaye amekuwa mwiba kwenye mechi kubwa kama hizo.
Tayari Mourinho ambaye ameonyesha imani kubwa kwa Mcameroon, Samuel Eto’o, ameishasema ndiye atakayempa nafasi ya kuongoza kikosi cha mashambulizi.

Mfumo wa timu zote mbili umekuwa ni 4-2-3-1, maana yake kila timu itabaki na mshambuliaji mmoja lakini kila zinapopanda lazima zinabaki na watu wanne nyuma.

Ufungaji & kufungwa:
Kwa mujibu wa msimamo wa ligi hiyo, Manchester City ndiyo timu ambayo imefunga mabao mengi kuliko nyingine yoyote, imetikisa nyavu za wapinzani mara 68, ndiyo timu iliyofunga mabao mengi kuliko timu nyingine zote zinazoshiriki ligi kubwa barani Ulaya.

Chelsea imefunga mabao 43, ni ya nne baada ya Liverpool yenye 57 na Arsenal iliyotikisa nyavu za wapinzani mara 45.

Lakini katika ugumu wa nyavu, inaonekana Chelsea ndiyo wataalamu zaidi kwa kuwa katika mechi 23 wamefungwa mabao 20 na ndiyo wana ngome ngumu kuliko nyingine yoyote. Manchester City wao wamefungwa mabao 26, wanaingia katika tano bora ya ngome ngumu bora England.

Kwa tathmini hiyo, maana yake mechi ya leo ni kati ya ngome ngumu dhidi ya safu kali ya ushambuliaji katika Ligi Kuu England, subiri majibu.

Wachungwe:
Manchester City:-ina watu hatari sana kwenye safu ya kiungo na ushambuliaji, Wahispania wawili hawa ni tatizo, Jesus Navas na David Silva. Wote ni wapishi lakini ni wafungaji wazuri wakipata nafasi.

Kiungo mwingine ni mchezaji bora Afrika kwa miaka mitatu mfululizo, Yaya Toure, anayechezesha timu, anayetoa pasi za mwisho na anayefunga pia, maana yake ni shughuli pevu.

Watu wawili wenye maumbo makubwa pia ni tatizo kwa Chelsea, Nagredo na Dzeko, mipira ya juu, lakini pia uwezo wa kupasua ngome bila ya woga. Kazi hii waachiwe Cahill na Terry.

Chelsea:-Usiwadharau hata kidogo, wana wasumbufu wengi katikati, Ramires, Lampard au Mikel kama akianza, ingawa sasa Mourinho amekuwa akimuingiza kumalizia kazi kama wanaongoza au kurekebisha mambo kama wamezidiwa.

Lakini Oscar, Hazzard na William, hawa ni tatizo kwa wilinzi wa Man City kwa kuwa wakizubaa kidogo tu wataumia.

Wote watatu wana uwezo wa kuwapita hata mabeki wanne, lakini mwisho wana uwezo wa kupiga mashuti na kufunga lakini wanaweza kutoa pasi nzuri za mwisho.

Mbele yao anakuwepo mtu mzima Eto’o, maarufu kama shemeji hapa Tanzania na akipata nafasi, basi ni mara chache sana kufanya makosa.

Vikosi vinavyotarajiwa kuwa:
.
Man City (Fomesheni 4-2-3-1): Hart; Zabaleta, Clichy; Demichelis, Kompany, Fernandinho, Silva,Touré Jovetic, Negredo na Navas.
Hawatakuwepo: Agüero (nyama ya paja), Milner (nyonga), Nasri (goti), Javi Garcia (haijaelezwa).

Chelsea (Fomesheni, 4-2-3-1): Cech; Ivanovic, Azpilicueta Cahill, Terry, Ramires, Lampard; Willian, Oscar, Eto'o na Hazard.
Hawatakuwepo: Torres, Van Ginkel (wote goti).
Mwamuzi: Mike Dean.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic