Kocha Mkuu wa Ashanti United, Abdallah
Kibadeni, amezitaja wazi mechi rahisi kwake zilizobaki kwenye mzunguko wa pili
wa ligi zinazoweza kumpa ushindi ambazo ni dhidi ya Simba SC, Azam FC na
Coastal Union.
Kibadeni alisema kuwa anapokutana na
timu hizo inakuwa rahisi zaidi kuwa na matumaini ya ushindi kutokana na timu
hizo kucheza kwa kujiamini zaidi.
“Unajua mechi ambazo zinaweza kutupa
ushindi ni zile tutakazokutana na Simba, Azam au Coastal, Yanga alikuwemo
kwenye kundi hili lakini kwa bahati mbaya tulipoteza kwenye ule mchezo
tuliokutana nao.
“Timu hizi nne nilizokutajia mechi zake
huwa nyepesi kuliko hizi nyingine zilizobaki ila watu huwa hawajui tu,
unapokutana nao mchezo huwa rahisi, hawakamii mechi na hucheza kiufundi zaidi,
kitu ambacho ni tofauti na unapokutana na hawa wengine kwa sababu hukamia na
kufanya mambo yawe magumu zaidi.
“Angalia tulipocheza na Yanga tukafungwa
2-1, tulicheza vizuri kuliko mechi ya Mgambo tuliyofungwa 2-0 ambapo mpira
haukuwa mzuri kutokana na timu pinzani kukamia zaidi.
“Timu kubwa zinacheza kwa kujiamini
zaidi lakini hizi ndogo ni matatizo, kupata pointi kwao ni kazi ngumu sana,”
alisema Kibadeni.
Aidha, Kibadeni aliongeza kwa kusema hizi timu
nyingine zinapotaka kushuka daraja ndiyo huamua kufanya hivyo ili zipate wa
kushuka naye lakini Azam, Coastal, Simba na Yanga hazina sababu ya kufanya
hivyo kwa kuwa zenyewe huangalia zicheze vipi kiufundi ziweze kutwaa ubingwa.
0 COMMENTS:
Post a Comment