Mshambuliaji Omary Changa aliyefariki dunia
Jumapili iliyopita na Championi likawa gazeti la kwanza kuandika, amezikwa juzi
kwenye makaburi ya Mwinyi Mkuu yaliyopo Magomeni, Dar, katika msiba
uliohudhuriwa na mamia ya wadau wa soka nchini.
Kifo cha mchezaji huyo wa zamani wa
Yanga na JKT Ruvu ambaye mara ya mwisho alikuwa akiichezea Moro United ya Ligi
Daraja la Pili, kimepokelewa kwa huzuni na masikitiko makubwa na baadhi ya
wadau waliojitokeza kwenye msiba huo.
Baadhi ya watu maarufu waliojitokeza
msibani hapo ni pamoja na nahodha wa zamani wa Yanga, Ally Mayay, aliyeonekana
kusikitishwa na msiba huo ambapo alieleza huzuni aliyokuwa nayo kwa marehemu.
“Kwa kweli tumehuzunika sana sisi
familia ya soka ukizingatia ni mmoja kati ya watu wachache waliokuwa wana uwezo
mkubwa wa kucheza mpira hapa nchini, yaani pengo lake halitaweza kuzibika
milele, alikuwa ni mtu wa pekee sana kwenye safu ya ushambuliaji,” alisema
Mayay.
Kocha Mkuu wa Moro United, Salum
Kumbala, naye pia alionyesha kusikitishwa: “Alikuwa msaada mkubwa kwa timu yetu
akiwa uwanjani lakini pia alikuwa akiwapa sana ushauri wenzake jinsi ya
kufanikiwa katika mpira, tumeondokewa na mtu muhimu sana.”
Kwa upande wake beki wa Azam FC, Aggrey
Morris, ambaye alikuwa msibani hapo, alisema: “Huyu ni mmoja wa wachezaji
niliokuwa nawakubali sana ili ndiyo hivyo ametutoka na hakuna atakayekuja
kufanya alivyokuwa anavifanya Changa na hiki ni moja kati ya mapengo makubwa
kuwahi kutokea kwenye soka hapa Tanzania.”
Pamoja na hayo, kiungo wa Yanga, Nizar
Khalfan, pia alielezea hisia zake: “Tumeumia sisi kama wachezaji kwa kumpoteza
mwenzetu aliyekuwa na kipaji chenye kuleta dira nzuri tu kwa soka la Tanzania,
tutammisi sana.”
Mashabiki, wadau, wachezaji na makocha walijitokeza kwa wingi kwenye
msiba wa mchezaji huyo ambaye mwili wake ulikutwa umetupwa Jangwani jijini Dar
es Salaam, wikiendi iliyopita.
0 COMMENTS:
Post a Comment