Marehemu Omari Changa
aliyefariki dunia Jumapili iliyopita ambapo gazeti hili lilikuwa la kwanza
kuripoti, imeelezwa kuwa mwili wake uligundulika tangu asubuhi ya siku hiyo na
muokota chupa za plastiki (makopo), lakini taarifa ilichelewa kuwafikia kwa kuwaogopa
polisi.
Imeelezwa kuwa, Changa,
straika wa zamani wa Yanga, alionekana Jumapili asubuhi, kabla ya taarifa za
kuonekana kwa mwili wake kuanza kusambaa majira ya saa 7 mchana na taarifa
kuwafikia wazazi wake saa 9 alasiri.
Inadaiwa kuwa, muuza makopo
huyo hakuwa mwepesi wa kuondoka eneo hilo ambalo lilikuwa karibu kabisa na
nyumba ya baba yake mzazi Changa, Mzee Changa Idd akisubiri watu wengine
wanaomfahamu wapite na kumgundua Changa ili iwe rahisi ujumbe kuifikia familia
ya mzee Idd.
Lakini baadaye mzee Idd
alitambua mazingira yote juu ya mwili wa mtoto wake, tangu asubuhi muuza makopo
alipomuona kwa mara ya kwanza.
“Taarifa zilichelewa
kunifikia, lakini watu waliugundua mwili wake (Changa), mapema tangu asubuhi
ila walisita kuja kututaarifu kwa kuhofia kuwa mashahidi namba moja endapo
uchunguzi ungefanyika.
“Ila hakuna uchunguzi unaoendelea
mpaka sasa kwa sababu tumeshamzika mtoto wetu, ila labda kama ni ripoti ya
hospitali anayo baba yake mdogo Omari,” alisema Idd.
Alipozungumza na SALEHJEMBE, baba huyo mdogo wa Changa, Abou Mirambo, alisema kuwa ripoti
iliyotolewa na hospitali juu ya mwili wa marehemu, inasema alipigwa na kitu
kizito usoni kilichopelekea upande wa kushoto wa uso kubonyea na upande wa
kulia wa paji la uso kuvimba.
Aidha, kwenye mkono wa
kushoto, aligundulika kuchubuka ngozi yake yote ya juu kuanzia kwenye kiwiko
mpaka kiganjani.
“Mimi pekee ndiye
niliyefuatilia hizo ripoti za hospitali na ndiye niliyekabidhiwa mwili na
madaktari na watu wa usalama, imebainika amepigwa na kitu kizito usoni na
mchubuko wa ngozi yote ya juu kwenye mkono wake wa kushoto,” alisema
Mirambo.
0 COMMENTS:
Post a Comment