Straika wa
Simba, Amissi Tambwe, amesema mpira wake aliopewa baada ya kufunga mabao matatu
‘hat trick’ katika mchezo dhidi ya
Oljoro ni kumbukumbu ya kipekee kwake na ameahidi kuupeleka kuutunza kwao Burundi
kama kumbukumbu.
Tambwe,
alipiga hat trick, Jumamosi iliyopita wakati timu yake ikiwasambaratisha
maafande wa JKT Oljoro kwa mabao 4-0, bao lingine likiwekwa kimiani na Jonas
Mkude.
Nyota huyo wa zamani wa Vital ‘O ya Burundi, alisema
ataupeleka kwao ili mke wake na mtoto wawe wamkumbuke kupitia mpira huo na
kuthamini kazi yake huku Tanzania.
“Ilikuwa ni
mara ya kwanza kupewa haki yangu kihalali, kwangu ni kumbukumbu na ninataka mke
na mtoto wangu Flory kila watakapouangalia wanikumbuke na kuthamini
ninachofanya huku Tanzania,” alisema Tambwe.
Hat trick
hiyo ni ya pili kwake baada ya mabao manne aliyofunga dhidi ya Mgambo Shooting
katika ushindi wa mabao 6-0 raundi ya kwanza, lakini hakupewa haki yake baada
ya mchezo.
Aliongeza
kuwa iwapo atafanikiwa kufunga hat trick nyingine iwe kwenye mchezo wa leo
dhidi ya Mtibwa au siku nyingine, mpira huo atautoa kama zawadi kwa marehemu
mama yake.
“Huu siwezi
kuutoa kama ‘dedication’ (zawadi), ni kumbukumbu muhimu kwangu, mara ya kwanza
walininyima haki yangu, lakini iwapo nitabahatika kufunga tena, hiyo itakuwa ni
zawadi kwa mama yangu. Nilimpenda sana, najua bila yeye nisingekuwa hapa wala
kuwa na mafanikio haya, bahati mbaya hayupo duniani,” aliongea kwa unyonge.
0 COMMENTS:
Post a Comment