Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na
Klabu ya Yanga zimeendelea kuvurugana kuhusu kama Yanga ni halali kumtumia
mshambuliaji Emmanuel Okwi katika mchezo wa Klabu Bingwa Afrika dhidi ya
Comoronize utakaopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar wikiendi ijayo.
Okwi yupo katika wakati mgumu baada ya
TFF kusimamisha usajili wake huku ikitaka kupata ufafanuzi kutoka Shirikisho la
Soka la Kimataifa (Fifa) kama ni halali Wanajangwani hao kumtumia au la.
Okwi awali alikuwa mchezaji wa Simba
aliyeuzwa kwenye kikosi cha Etoile du Sahel lakini baadaye aligoma kwa kuwa
hajalipwa mshahara na kusajiliwa kwa mkopo na SC Villa ambayo ilimuuza kwa
Yanga.
Akizungumza na Championi Jumatano,
Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Seif Magari, alisema kuwa tayari
wameshamuandaa mchezaji huyo kwa ajili ya kumtumia katika mchezo wa Jumamosi
dhidi ya Comoronize, lakini bado hawajapata barua kutoka TFF hadi sasa.
“Tumemuandaa vyema Emmanuel Okwi kwa
ajili ya mchezo wetu dhidi ya Comoronize tutakaocheza Jumamosi kwani yupo safi
na amejiunga na wenziye na kiwango chake kinaonekana kipo juu.
“Tunawasubiri TFF waweze kututaarifu kwa
barua kama tunaweza kumtumia Jumamosi lakini hadi sasa hakuna barua yoyote
tuliyoipata ambapo tunasubiri jibu lao,” alisema Magari.
Aidha kwa upande wa TFF kupitia kwa
Ofisa Habari wake, Boniface Wambura, amefunguka kuwa: “Okwi tumemfungia leseni
ya kucheza ligi kuu hivyo iwapo mchezaji hana leseni ya kucheza ligi ya ndani
haruhusiwi kucheza mechi za kimataifa na kwa sasa tunasubiri barua kutoka Fifa
ambayo itatoa maamuzi.”
Yanga wana matumaini kuwa wanaweza
kupewa ruhusa ya kumtumia mshambuliaji huyo kwenye mchezo wa wikiendi ijayo.
0 COMMENTS:
Post a Comment