Mshambuliaji wa Yanga, Said Bahanuzi,
juzi Jumamosi aliwaomba radhi mashabiki wa soka waliofurika kwenye Uwanja wa
Jamhuri mjini hapa kwa kitendo cha kukosa penalti katika mchezo wa Ligi ya
Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly nchini Misri, wiki iliyopita.
Bahanuzi ambaye alikuwa hajawahi
kukutana na mashabiki kwenye umati mkubwa tangu warudi nchini Misri, alitumia
nafasi hiyo baada ya kufanya mazoezi mepesi kabla ya mechi ya Ligi Kuu Bara
kati ya Mtibwa na Yanga kuanza.
Wakati wachezaji hao wakiingia vyumbani
kujiandaa na mechi hiyo, aliwaacha wenzake na kwenda kusimama mbele ya jukwaa
la mashabiki wa Yanga na kuwanyooshea mikono kama ishara ya kuwasalimia, kisha
akajishika kifuani na kuwainamia, ishara ambayo hutumiwa na waungwana kuomba
msamaha.
Baada ya kitendo hicho, mashabiki hao
walimpigia makofi ndipo akaenda kujichanganya na wenzake kuelekea vyumbani.
Wakati tukio hilo likiendelea, kundi la mashabiki wanaodhaniwa kuwa ni wa
Simba, lilikuwa likipiga mayowe ya kumzomea.
Championi Jumatatu lilijaribu kuongea na
mchezaji huyo kutaka kujua sababu za kitendo hicho, lakini alikataa kuzungumza
chochote akidai hawaruhusiwi kuzungumza na wanahabari.
0 COMMENTS:
Post a Comment