Na Mwandishi Wetu
Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement
Sanga, ameweka rekodi kwenye klabu hiyo baada ya kurudisha kitita cha Sh
milioni 38 mara tu baada ya kutua akitokea Misri.
Inaelezwa Sanga alikabidhiwa kitita cha
dola 50,000 (Sh milioni 80) kwa ajili ya matumizi kama hoteli, posho na mengine
wakati Yanga ikiwa nchini Misri kupambana na mabingwa wa Afrika, Al Ahly ambako
ilitolewa kwa mikwaju ya penalti.
Baada ya timu hiyo kurejea nchini ikiwa
imetolewa kwa mikwaju 4-3 ya penalti, Sanga alikwenda klabuni na kukabidhi
fedha hizo ambazo zilichukuliwa haraka na kupelekwa benki, kitu ambacho
kiliwashangaza watu wengi ofisini hapo.
“Kweli hiyo si hali ya kawaida, unajua
fedha zile dola elfu hamsini zilitolewa kwa ajili ya bajeti ya timu ikiwa
Cairo, si unajua namna Al Ahly walivyokuwa wanaiwinda Yanga kuihujumu! Hivyo
kilichofanyika ni kuhakikisha kila kitu kinakuwa safi.
“Utaona namna mambo yalivyokwenda
vizuri, unaweza kusema uongozi ulifanya kila linalowezekana lakini mwisho
walioshindwa ni wachezaji. Si kwamba tunalaumu lakini ndiyo mambo ya mpira,
lakini Sanga amefanya kazi vizuri na karudisha zile fedha, katushangaza,”
kilieleza chanzo kutoka ndani ya Yanga.
Sanga ndiye alikuwa kiongozi wa
mapambano wakati Yanga ikiwa nchini Misri katika miji miwili tofauti, wa Cairo
ambao unaongoza kwa ukubwa nchini humo na ule unaofuatia kwa ukubwa wa
Alexandria ambako ndiyo mechi ilipigwa.
Yanga ikiwa huko ilikataa hoteli na
mabasi yote iliyopangiwa na Al Ahly na ikakodi kivyake. Lengo lilikuwa ni
kujiepusha na hujuma za Waarabu wa Misri ambao wana mbinu nyingi sana nje ya
uwanja.
0 COMMENTS:
Post a Comment