Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF) limeanza mchakato wa kuendeleza uwanja wake uliopo eneo la Mnyanjani
jijini Tanga.
Kwa Mujibu wa taarifa kutoka TFF, uwanja huo ambao ulinunuliwa wakati wa uongozi chini ya Leodeger Tenga, sasa shughuli inayoendelea kwa sasa ni
kupima udongo (soil test) na kuandaa michoro kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha
michezo (Sports Complex) ukiwemo uwanja wa mpira wa miguu na majukwaa yake.
TFF imetuma maombi rasmi kwa Mkuu wa
Mkoa wa Kilimanjaro kuomba eneo la kujenga kituo cha michezo ikiwemo uwanja wa
mipira wa miguu na majukwaa yake.
Pia Mkuu wa mkoa ameombwa kuingilia
kati kuwaondoa wafanyabiashara waliovamia uwanja wa mpira wa miguu wa Jamhuri
(King George Memorial ground) mjini Moshi.
TFF inawakumbusha viongozi wa vyama
vya mikoa ambao hawajaomba maeneo ya kujenga vituo vya michezo vikiwemo viwanja
vya mpira wa miguu, waongeze jitihada za kufanya hivyo, TFF itawaunga mkono.
TFF inachukua fursa hii kuvipongeza
vyama vya mpira wa miguu ambavyo ama tayari vimeshachukua hatua au viko mbioni
kuchukua hatua kutafuta na kuendeleza maeneo kwa ajili ya matumizi ya mpira wa
miguu.
TFF inaahidi kuunga mkono juhudi hizi
na pale itakapohitajika kuongeza nguvu haitasita kufanya hivyo.
Wakati huo huo, TFF inalishukuru
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kwa kukubali kugharamia
uwekaji nyasi za bandia kwenye Uwanja wa Kaitaba, na pia kusaidia uendelezaji
wa uwanja wa TFF wa Tanga.
0 COMMENTS:
Post a Comment