March 23, 2014





Na Saleh Ally
JIJI la Madrid ndilo litakuwa mwenyeji wa mechi kubwa ya watani wa jadi kuliko nyingine zote duniani inayopigwa leo Jumapili kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu.

Real Madrid dhidi ya wageni wao, Barcelona, kila timu itakuwa inacheza mechi yake ya 29 ya Ligi ya Hispania maarufu kama La Liga. Kila upande utakuwa unataka kuibuka na ushindi.


Ushindi ni muhimu kwa kila timu kwa mambo mawili makubwa, kwanza ni mechi ya watani wa jadi na hakuna timu itakubali kushindwa bila ya kujali ni ugenini au nyumbani. Ushindi kwa timu yoyote utakuwa ni heshima kubwa kwa sababu ya kuendelea kuweka rekodi, kwamba wamekutana mara ngapi na yupi ameshinda mara nyingi.
 
ANCELOTTI
Pili, nafasi katika msimamo wa La Liga, kwani ushindi ni pointi tatu na hakuna ambaye atataka kupoteza au kugawana, badala yake azipate zote kwa wakati mmoja.

Timu zote zimecheza mechi 28, Real Madrid inaongoza La Liga kwa kuwa na pointi 70, inafuatiwa na Atletico Madrid yenye pointi 67 na Barcelona ni watatu wana 66. Hii inaonyesha kiasi gani kila upande utakuwa unataka kushinda leo.

Iwapo Madrid watashinda, maana yake watajipa nafasi nzuri ya kuongeza pengo la pointi saba dhidi ya wapinzani wao hao, lakini Barcelona wakishinda maana yake watakuwa wamesonga na kupunguza pengo ambalo litabaki pointi moja tu.

Lakini Madrid ambao wanaonekana kuwa na kikosi bora kipindi hiki chini ya Carlo Ancelotti, watakuwa na hamu ya kulipa kisasi cha kufungwa mabao 2-1 katika mechi ya mzunguko wa kwanza ambayo ilichezwa ugenini Camp Nou.

Lakini ukiachana na hayo, kuna mambo mengi ambayo yanaifanya dunia ‘isimame’ inapofikia siku ya El Clasico, yaani mechi ya watani, gumzo kuliko zote katika ulimwengu wa soka.

Kati ya mambo hayo ni kila timu ina wachezaji gani maarufu, zimewahi kukutana mara ngapi na ipi imeshinda nyingi, ipi imepoteza sana na kuna sare ngapi. Wachezaji gani ambao wamecheza mechi nyingi za La Liga na imekuwa vipi.

Ronaldo & Messi:
Cristiano Ronaldo wa Real Madrid ndiye mwanasoka bora dunia kwa sasa akiwa amechukua taji lililokuwa linashikiliwa na mpinzani wake mkubwa Lionel Messi. Lakini rekodi nyingine kesho, Ronaldo atacheza dhidi ya Barcelona, kwa mara ya kwanza akiwa mwanasoka bora duniani.

Aliwahi kutwaa taji hilo mwaka 2008 akiwa Manchester United, lakini tokea ametua Madrid amekuwa akipambana kulipata bila ya mafanikio na Messi amekuwa akilichukua kama anavyotaka.
TATA

Swali, leo ni zamu ya Ronaldo? Lakini bado Messi ambaye amekuwa akisumbuka kutoka kwenye majeruhi atakuwa anataka kuonyesha kuwa hata kama hana taji hilo, yeye ni bora na ndiye mchezaji ambaye amekuwa ‘akiionea’ Real Madrid, anavyotaka.

Bale & Neymar:
Wachezaji wengine wawili ambao wameongeza utamu wa La Liga ni Gareth Bale ambaye sasa ndiye mchezaji ghali zaidi duniani kwa maana ya uhamisho. Lakini pia kuna Neymar wa Barcelona ambaye pia ni mchezaji ghali na kinda ambaye ana kipaji cha aina yake.
Hawa wanaonekana kama wasaidizi wa Ronaldo na Messi, lakini wana uwezo mkubwa na inawezekana kabisa wanaweza wakafanya mambo makubwa zaidi hata ya hao nyota wawili na ‘kuuiba’ mchezo na wao ndiyo wakawa gumzo zaidi.
Kipaji cha Neymar ni hatari, tayari Madrid wanajua madhara yake kwa kuwa amewahi kuwaadhibu. Ni hata kwa mabeki kwa kuwa pamoja na kuwa na uwezo wa kufunga lakini ni mjanja katika kutoa pasi za mwisho zinazozaa mabao.

Bale, alikuwa akisumbuka na majeraha kila mara. Sasa ameinuka na yuko safi na ana vitu vingi ambavyo mabeki wa Barcelona vitawapa wakati mgumu. Kwanza uwezo wa kuwachambua hata mabeki watatu, kasi, krosi zenye ‘macho’ lakini mashuti makali.

WACHUNGWE:
Ingawa wanaozungumziwa ni wachezaji nyota kama Ronaldo, Angel Di Maria na wengine, lakini kuna wachezaji makinda wanapaswa kuchungwa na hasa upande wa Real Madrid. Kwanza mkongwe Xabi Alonso na pasi zake murua kwa mashambulizi ya kushitukiza, noma. 

Usisahau, Madrid itamkosa Jesse ambaye ameumia, lakini ina makinda hawa watatu, Álvaro Morata, Isco na Asier Illarramendi na kama kweli watapata nafasi kesho kwa kuwa Ancelotti anaamini vijana, basi wana kila sababu ya kuweka ulinzi maradufu kwa kuwa vipaji vyao ni vya juu sana.

Hata iwe vipi, mkongwe Xavi Harnandez atakuwa tatizo, lakini wachezaji watatu, Andres Iniesta, Alexis Sanchez na Pedro Rodriguez wana bahati sana ya kutingisha nyavu za Madrid, wachungwe lakini kuna vijana hawa; Jonathan dos Santos, Cristian Tello na Ibrahim Afellay. Kama Tata atawapa nafasi, basi Madrid wachunge sana.

Katika timu hizo, hakuna ya kuidharau. Hisia za kuwa Barcelona wamekwisha chini ya Tata Martino si sahihi, kila timu ina uwezo mkubwa na kiwango cha juu. Lakini Madrid wanaonekana kuwa na kiwango cha juu zaidi.

TAKWIMU:
Mechi tano:
Madrid:- Katika mechi zao tano za mwisho wameshinda nne na kutoka sare moja. Kati ya hizo, zote  mbili  za mwisho wamefanikiwa kuibuka na ushindi.
Barcelona:-Katika mechi zao tano za mwisho kabla ya kesho kuivaa Madrid, Barcelona wameshinda tatu na kupoteza mbili. Bado rekodi yao si nzuri ukilinganisha na wapinzani wao ingawa si kigezo cha wao kupoteza.

WALIOCHEZA NYINGI EL CLASICO:
MCHEZAJI                             MECHI
Manuel Sanchís-Madrid       43
Francisco Gento-Madrid       42
Xavi Hernández-Barca        38
Fernando Hierro-Madrid         37
Raul Gonzalez-Madrid            37
Carles Puyol-Barca               32  


WALIOPACHIKA MABAO MENGI:
(Ni mabao kila zilipokutana, hawa waliofunga mengi na bado wanacheza):
MCHEZAJI                        IDADI           TOKEA
Messi-Barca                          18                   2004
Ronaldo-Madrid                   12                    2009
Pedro-Barca                           5                     2008
Xavi-Barca                               5                    1998
Benzema-Madrid                   4                 2009

VIPIGO VIKUBWA TOKEA 1943:
Juni 13, 1943
Real Madrid 11-1 Barcelona- Copa del Rey
Feb 3, 1935
Real Madrid 8-2 Barcelona-La Liga
Sept 18, 1949
Real Madrid 6–1 Barcelona-La Liga
Aprili 21, 1935
Barcelona 5–0 Real Madrid
Machi 25, 1945
Barcelona 5–0 Real Madrid
Sept 24, 1950
Barcelona 7–2 Real Madrid-La Liga
Okt 25, 1953
Real Madrid 5–0 Barcelona
Feb 17, 1974
Real Madrid 0–5 Barcelona
Jan 8, 1994
Barcelona 5–0 Real Madrid
Jan 7, 1995
Real Madrid 5–0 Barcelona
Nov 9, 2010
Barcelona 5–0 Real Madrid



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic