Na Saleh
Ally
UTAONA katika mechi ya jana dhidi ya Osasuna namna Lionel Messi alivyokuwa akicheza kwa juhudi. Lazima afanye hivyo kurudi kwenye chati.
Katika mechi hiyo ya La Liga, Barcelona ilishinda kwa mabao 7-0, Messi akapiga hat trick lakini pia akatoa pasi za mabao.
Kukaa nje kumemuathiri, lakini ni wakati mwafaka kwake kuonyesha ni muhimu kama awali au zaidi. Tegemeo na mwenye msaada mkubwa. Unajua kwa sababu zipi?
RONALDO |
Mkataba mpya wa Real Madrid na Cristiano Ronaldo ambao unailazimu klabu hiyo kulipa
euro milioni 18 (Sh bilioni 39) kwa mwaka, unaonyesha umesababisha mpasuko wa
chinichini kati ya Barcelona na Messi.
Mkataba
huo mpya kati ya Ronaldo na Real Madrid walioingia miezi michache iliyopita,
unaifanya klabu hiyo tajiri kuwa inamiliki wachezaji wawili maarufu
wanaohusiana na suala la fedha nyingi.
Ronaldo
ndiye mchezaji anayelipwa zaidi kuliko wengine wote duniani, lakini Gareth Bale
ambaye amenunuliwa na Madrid akitokea Tottenham kwa pauni milioni 80 (Sh
bilioni 208), ndiye mchezaji ghali zaidi kwa maana ya uhamisho.
Kutokana
na hali hiyo, lazima Messi atahoji, ingawa amekuwa kwa kipindi kirefu, tayari kuna
taarifa ya kuanza mjadala wa mkataba mpya.
Bado
Barcelona na Messi hawajakubaliana katika mambo kadhaa ingawa Messi ameshindwa
kudai fedha nyingi kama za Ronaldo kwa kuwa anataka apate euro milioni 9 (Sh
bilioni 20) kwa mwaka ambazo ni nusu ya zile anazolipwa Ronaldo.
Messi
ameonekana hana wasi katika hilo kwa sababu kadhaa, moja ni kuhusiana na fedha
anazopata kutoka kwa wadhamini wake pembeni na Barcleona.
Kwa
mwaka, Messi anaingiza hadi euro milioni 23 (Sh bilioni 52) kutoka kwa wadhamini
wake nane na wadhamini wakuu wamekuwa ni Adidas ambao katika kila miezi 12, wao
hutoa euro milioni 8 (Sh bilioni 18).
Messi
amekuwa akionekana ni kama mtoto wa Adidas, juhudi za Nike kumsaka zimekuwa
zikigonga mwamba kwa kuwa yeye ameonyesha mapenzi makubwa na Adidas na suala
hilo linatokana na historia kati yake na makampuni hayo mawili makubwa ya vifaa
vya michezo.
Messi
aliwahi kuomba apate udhamini wa Nike wakati akiwa bado hajajulikana sana, Nike
wakakataa kwa kuona hakuwa na hadhi yao. Lakini Adidas walijitokeza na
kumchukua, ndiyo maana anazidi kuwaonyesha fadhila.
Tukirudi
kwenye mkataba mpya na Barcelona, euro milioni 9 kwa mwaka kwake ni sawa,
lakini Barcelona nao wanasema wanahitaji kumiliki haki ya picha za Messi, kitu
ambacho yeye na msimamizi wa masuala yake ya kimaslahi, Jorge Messi ambaye ni
baba yake mzazi wanapinga.
Messi
na Jorge, wanachotaka pamoja na kutolewa euro milioni 9 kwa mwaka, basi kitu
muhimu kwao ni kuachiwa haki za picha hizo ambazo pia zina nafasi ya
kuwaingizia mamilioni ya fedha.
Barca
inahitajika kukusanya euro milioni 45 (Sh bilioni 101) ili kuanzisha mkataba
mpya wa miaka mitano na Messi. Ingawa tayari ina mkataba naye hadi mwaka 2018,
maana yake kama wataingia huo mpya itakuwa ndiyo uthibitisho wa Messi kuzeekea
Barca.
Inaonekana
wazi kuwa Barcelona haikuwa tayari kutengeneza mkataba mpya na Messi lakini
hali ilivyo na presha kutoka Madrid namna inavyowahudumia Bale na Ronaldo,
Barcelona wanaingia kwenye presha.
Ronaldo
ndiye amekuwa presha kubwa kwa Messi, lakini presha zaidi kwa Barcelona. Ingawa
wamekuwa wanakataa lakini kuanza kujadili mkataba mpya wa Messi katika kipindi
hiki kunadhihirisha hilo.
Messi
bado hajawa katika kiwango kizuri, anajaribu kuinuka lakini hakuna ubishi kuwa
atakaa sawa na kuanza kufanya vizuri kama hataumia na kukaa nje kwa muda mrefu
kwa kuwa ana uwezo mkubwa.
Ushindi
wa Ronaldo kuwa mchezaji bora pia ni sehemu ya presha nyingine kwa Messi ambaye
anatambua analazimika kufanya vizuri ili kushindana naye katika tuzo zijazo.
Awali
ilionekana kuwa Messi alikuwa presha kubwa kwa Ronaldo, hiyo ilikuwa ni hali
halisi. Ilionekana kama alikosea kuhamia nchini Hispania, wengine wakashauri
angeweza kubaki England na kuichezea Manchester United na ingekuwa rahisi kwake
kupambana na Muargentina huyo.
Wakati
Ronaldo anatua Real Madrid akitokea Manchester, tayari Messi alikuwa ni mfalme
wa soka la Hispania na duniani kote, hivyo ikaonekana kama vile Ronaldo
alikosea.
Utaona
mara ya mwisho Ronaldo alichukua uchezaji bora wa dunia mwaka 2008, baada ya
hapo hakuwahi kupata nafasi hiyo huku Messi akishinda zaidi ya mara mbili.
Hali
hiyo ilisababisha presha kubwa kwa Ronaldo ambaye bado aliendelea kupambana
ikiwa ni pamoja na kuweka rekodi ya kufunga mabao mbele ya Messi.
Wachambuzi
wa soka walisema Ronaldo kwenda kwenye anga za Messi ni sawa na suala la kujipeleka
kwenye mdomo wa mamba. Lakini sasa inaonekana amefanikiwa kumthibiti mamba!
0 COMMENTS:
Post a Comment