Na Saleh Ally
HAKUNA ubishi, umaarufu wa Ligi Kuu England
unatokana na namna ushindani unavyokua kuanzia mwanzo hadi mwisho wa ligi hiyo
bila kujali timu ni zipi.
Vipigo vya ‘kufa mtu’ vya juzi huku vikihusisha
vigogo kama Arsenal, vimeonyesha kuwa Ligi Kuu England, maarufu kama
Premiership, haitaki lelemama na wala si ligi ya kubahatisha.
Timu zilizo kileleni au zinazopambana kuwania
ubingwa, yaani Chelsea, Liverpool na Manchester City kila moja imeshinda
kuanzia mabao matano kwenda mbele.
Chelsea iliishindilia Arsenal kwa mabao 6-0 na
kuacha gumzo ambalo litaendelea kudumu kwa siku kadhaa, Manchester City
wakawaminya Fulham na kuzidi kuwadidimiza kwa mabao 5-0 huku Liverpool
wakiwatanguliza SAS (Suarez na Sturridge) wakailipua Cardiff kwa 6-3.
Arsenal ndiyo timu pekee iliyo katika nne bora
katika msimamo wa ligi hiyo ambayo ilikutana na kipigo cha mabao hayo sita.
Hiyo ni dalili tosha kuwa timu hizo hazina
mchezo katika mechi hizo za mwisho, pia ni dalili tosha kwamba kadiri ligi
inavyokwenda ukingoni, basi kutakuwa na mambo mengi sana ya kushangaza.
Pamoja na yote hayo, timu tatu tu tayari
zimejichuja kuwa ndiyo zinazowania ubingwa wa Ligi Kuu England ambazo ni
Chelsea, Liverpool na Manchester City.
Kimahesabu inaonekana Manchester City inaongoza
kutokana na asilimia kubwa, ikifuatiwa na Chelsea, Liverpool na Arsenal ambao
hata hivyo wamezidi kupoteza mwelekeo tofauti na walivyoanza.
Mchezo wa soka unapendwa kuliko yote duniani kwa
kuwa hautabiriki, ukiamini vile wenyewe unaibuka na matokeo tofauti kabisa.
Lakini kuna wakati unafikia, lazima mambo yawe hivyo.
Pamoja na kwamba hesabu zinaonyesha Manchester
City ina nafasi kubwa zaidi lakini lazima ishinde, hali kadhalika kwa Chelsea
na Liverpool, atakayeteleza basi ajue amekwenda na maji.
Kingine ambacho kina ugumu ni hivi, kwamba
katika baadhi ya mechi, timu hizo nne zinazowania ubingwa, zitakutana zenyewe
kwa zenyewe. Maana yake ugumu wa hesabu utakuwa katika mechi hizo,
atakayepoteza, basi anapotea zaidi.
Man City:
Hawa wana nafasi zaidi kutokana na kuwa na
michezo mingi zaidi mkononi, wanayo kumi, maana yake inategemea watazicheza
vipi karata zao kuhakikisha wanapasi au la.
Hadi sasa wamecheza mechi 28, wamekusanya pointi
63 na wako kwenye nafasi ya tatu. Iwapo watashinda zote kumi, watafikisha
pointi 93 ambazo zitakuwa ni za juu zaidi na haziwezi kufikiwa na timu nyingine
yoyote.
Kwa pointi hizo, hakutakuwa na timu ya kuwazuia
kuwa mabingwa wa England kwa mara ya pili katika kipindi cha misimu mitatu.
Ugumu kwao ni mechi mbili; watakutana na timu
mbili kati ya hizo zilizo katika nafasi nne za juu katika msimamo huo; Machi 29
watawavaa Arsenal wakiwa ugenini na Aprili 13 watakaribishwa kwenye Dimba la
Anfield kwao Liverpool. Wakivuka hapo, basi wao wanaume wa shoka.
Chelsea:
Kimahesabu wana nafasi ya pili kwa kutwaa
ubingwa maana wamecheza mechi 31, wana pointi 69 kileleni mwa ligi,
wanachojivunia ni kuwa na pointi nyingi na si michezo mingi.
Wamebakiza mechi saba, wakishinda zote watakuwa
na pointi 90 ambazo ni za pili kwa wingi ukilinganisha na Man City wakishinda
zote.
Mechi ya vigogo walio katika nne bora, itakuwa
Aprili 7 dhidi ya Liverpool kwenye Uwanja wa Afield, wakipita hapo wana nafasi
kubwa. Wakipoteza, kutakuwa na walakini na ugumu kwao.
Liverpool:
Wana pointi 65 baada ya kucheza mechi 30 za Ligi
Kuu England na wako katika nafasi ya pili kwenye msimamo. Lakini kama ni kutwaa
ubingwa, inaonekana wanaweza kufanya hivyo bado.
Unaweza kuwapa nafasi ya ubingwa kwa kuwa katika
mechi 30 walizocheza, maana yake wamebakiza nane na wakishinda zote, tayari
wana uwezo wa kufikisha pointi 89.
Lakini wana ugumu zaidi kwa kuwa wana mechi
mbili dhidi ya vigogo wanaowania ubingwa. Aprili 13 watakuwa nyumbani dhidi ya
Man City, hicho ni kimbembe. Halafu Aprili 27 wana Chelsea na ndiyo zinazopewa
nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa.
Inawezekana Liverpool ikajitengenezea nafasi
bora kwa kuwa iko nyumbani na ikizifunga timu hizo mbili, itatibua hesabu zao
na asilimia zao za ubingwa, kujitengenezea nafasi bora zaidi badala ya
kuonekana kucheza nao ni tatizo kwao.
Arsenal:
Tofauti na ilivyoanza, kasi yake kama kawaida
inapungua mwishoni na taratibu wanaanza kupiga ‘rivasi’. Tayari wameyumba
ingawa ndiyo timu inayopewa nafasi ya nne kati ya nne zinazowania ubingwa.
Imecheza mechi 30 na kukusanya pointi 62 ikiwa
katika nafasi ya nne kwenye msimamo na iwapo itashinda zote nane zilizobaki
itakusanya pointi 86.
Ugumu kwake katika mechi nane zilizobaki, moja
ni tatizo kwa kuwa watakutana na Man City, Aprili 29. Ndiyo watakuwa nyumbani,
lakini wanalazimika kufanya kazi ya kweli kupunguza kasi ya ‘mziki’ wa jamaa
hao wa Jiji la Manchester.
Timu yoyote katika ya hizo, ukianza na yenye
nafasi ya kwanza hadi ya nne kutwaa ubingwa huo inaweza kuwa bingwa,
kinachotegemewa ni umakini na hesabu za uhakika za kumaliza mechi zilizobaki.
Karibu kila timu itakutana na timu nyingine
zinazoonekana ni ndogo lakini pia zitakuwa zinapambana kuepuka kushuka daraja.
Hivyo, ugumu utakuwa mwanzo mwisho na timu ikifungwa mechi mbili kati ya
ilizobakiza, ubingwa isahau.
MSIMAMO WA NAFASI YA UBINGWA:
MECHI POINTI WAKISHINDA ZOTE POINTI
Chelsea
31
69 (mechi 7) +21
90
Liverpool 30
65
(mechi 8) +24 89
Man
City 28
63
(mechi 10) +30 93
Arsenal
30
62
(mechi 8) +24
86
Premier
P W D L GF GA Pts
1.
Chelsea 31 21 6 4 62 23 69
2.
Liverpool 30 20 5 5 82 38 65
3.
Man City 28 20 3 5 76 27 63
4.
Arsenal 30 19 5 6 53 34 62
0 COMMENTS:
Post a Comment