Na Saleh Ally
KIPIGO cha mabao 2-1 walichokipata Real
Madrid kutoka kwa Sevilla, usiku wa kuamkia jana, ni jibu tosha kwamba
wameingia kwenye kipindi kigumu cha matatizo na wakizubaa kidogo, majanga!
Kwa mtazamo wa haraka kama baadhi ya
mashabiki wa Madrid walivyoandika kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba
mambo mazuri yanakuja na wasijute na kupoteza, inaweza kuonekana kama ni jambo
la kawaida.
Lakini mambo yakiwekwa kwenye mahesabu
inaonekana kuwa kuna kila dalili Barcelona inaweza kubeba ubingwa wa La Liga na
hasa kama Madrid watashindwa kuliona na kuliamini hilo kuwa linaweza kutokea.
Tofauti au balaa kwa Madrid limeanza
baada ya kupoteza pointi sita ndani ya siku tano tu, halafu Barcelona
wakaongeza idadi hiyo ya pointi kwa kipindi hicho.
Madrid wamepoteza mechi mbili mfululizo,
dhidi ya Barcelona kwa kufungwa mabao 4-3 wakiwa nyumbani kwao, halafu
wakafungwa 2-1 na Sevilla wakiwa ugenini. Barcelona wao wakaongeza pointi kuwa
sita kwa kuwaadhibu Celta Vigo 3-0.
Kutokana na matokeo hayo, Barcelona
wamepanda hadi nafasi ya pili wakiwa na pointi 72, wakati Madrid waliokuwa
vinara wameteremka hadi nafasi ya tatu wakiwa na pointi 72 na Atletico Madrid
ndiyo vinara wakiwa na 73.
Hesabu za kuangalia ni mwenendo wa timu
hizo, namna Madrid wanavyokwenda ni balaa kwa kuwa Barcelona wamewazidi kwenye
vitu vingi wakati ndiyo wako katika hatua za mwisho.
GD:
Kasi ya ufungaji mabao kwenye safu ya
Barcelona imezidi kuwa juu na hasa tangu kurejea kwa Messi na hiyo inafanya
tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa (GD) ya Barcelona kuwa juu. Barca
imefunga mabao 88 na kufungwa 25 tu, hivyo GD yake ni 63.
Madrid imefunga 81 na kufungwa 32, GD
yake ni 49. Hivyo ikitokea imelingana na Barcelona, basi itakuwa katika wakati
mgumu kuwa juu yake.
Kanuni:
Kanuni za La Liga kuhusu timu kuwa juu
ya msimamo, zinaonyesha kwanza timu inaangaliwa kuwa ina pointi ngapi, pili
zimewahi kukutana mara ngapi na nani alifanya vizuri (head-to-head). Halafu
vinafuata vigezo vingine.
Barcelona na Madrid zimekutana mara
mbili kwenye La Liga, Barca imeshinda zote. Hivyo yenyewe iko katika nafasi
nzuri zaidi.
Ushindi:
Ushindi mfululizo unazidi kujenga hali
ya kujiamini ya Barcelona ambayo awali ilionekana iko taabani. Lakini kupoteza
kunazidi kuidhoofisha Madrid ambayo ilijiona iko katika nafasi nzuri ya kutwaa
ubingwa kabla ya kuboronga mechi mbili mfululizo.
Messi:
Messi ndiye amekuwa chachu ya mabadiliko
ya Barcelona ambayo imekuwa na kiwango cha juu zaidi baada ya kurejea kwake.
Hali nzuri ya kuelewana kimchezo kati
yake na watu wawili, Iniesta na Neymar imeongeza makali ya Barcelona katika
kupata ushindi.
Mechi:
Baada ya mechi 30, kila timu imebakiza
mechi nane tu. Katika kila mechi nane zilizobaki kwa timu hizo, inaonyesha zina
ugumu wake kwa kuwa zitacheza na timu kama Espanyol, Getafe, Villareal na
Atletico Madrid ambazo bila ya kujali ziko nafasi ipi lakini zimekuwa na
upinzani mkubwa dhidi ya timu hizo.
Barcelona:
Espanyol, Real Betis, Granada,
Villareal, Getafe, Athletic Bilbao, Elche na Atletico Madrid.
Madrid:
Rayo Vallecano, Real Sociedad, Almeria,
Osasuna, Valencia, Valladolid, Celta Vigo na Espanyol.
0 COMMENTS:
Post a Comment