Na Saleh Ally
UKIAMBIWA kazi ya ukocha wa soka katika nchi za Afrika inaweza kuwa
moja kati ya kazi ngumu zaidi duniani, usikatae. Kuna mengi sana ya
kuthibitisha hilo.
Hata kocha kama atakuwa na ujuzi kiasi gani, asilimia kubwa ya nchi za
Afrika Mashariki, makocha wake wanafanya kazi bila ya kuwa na vifaa, makazi
wala malipo mazuri.
FERGUSON |
Wanaokuwa na ahueni ni makocha wa kigeni kwa kuwa tu, ugeni wao
huwafanya wapate huduma kadhaa ambazo makocha wazalendo wamekuwa hawazipati
hata kidogo.
Kuna kocha raia wa Brazil, Nielsen Elias alitua nchini kuinoa Simba
miaka takribani sita iliyopita, mara baada ya kuonyeshwa uwanja wa mazoezi,
akasisitiza kuwa kama hautabadilishwa ataondoka zake. Siku chache baadaye
akasema wazi, Simba haikuwa hadhi yake, akaondoka.
Kocha Ernie Brandts hadi anaondoka alikuwa hajatimiziwa ombi lake la
kupewa magoli madogo aliyokuwa ameyaomba kwa uongozi wa Yanga ili kutoa mafunzo
maalum. Lakini mwisho alionekana ameshindwa kuipandisha timu yake kiwango.
Tatizo kwa viongozi wa soka nchini wanaonekana wanajua zaidi kuliko
makocha, ndiyo maana timu kubwa kama Yanga na Simba, leo zaidi ya miaka 40,
hazina hata viwanja vya mazoezi vyenye ubora.
Vitu vinavyoonekana ni vidogo, ndiyo vikubwa na timu nyingi kubwa
maarufu duniani zinavithamini zikiwa njiani kupata maendeleo na zimefanikiwa.
PELLEGRINI |
Malipo duni ya makocha, kutokuwa na makazi mazuri hadi wanapokuwa
wageni au Wazungu lakini umewahi kusikia kuna klabu hapa nchini imetenga ofisi
kwa ajili ya kocha wake?
Kila mmoja anaamini kocha kazi yake ni uwanjani pekee, lakini klabu
zote kubwa duniani makocha wao wana ofisi zao.
Unaweza kusema Manchester United, Manchester City, Arsenal, Real
Madrid na Barcelona ni kubwa sana. Je, timu za madaraja ya nchini katika nchi
nyingine za Ulaya, makocha wao wanaofisi?
Ndiyo, mfano mzuri ni Gefle IF aliyowahi kuichezea Haruna Moshi
‘Boban’. Inashiriki daraja la kwanza na kocha wake, Perre Olsson ana ofisi
yenye ubora ambao unaweza kulinganisha au zaidi ya ile ya meneja mkuu wa benki.
Hapa nyumbani inaweza kuonekana ni sawa na kichekesho cha karne kocha
kuwa na ofisi kwa kuwa tu, hata makatibu au watendaji wa klabu na timu
nyingine, angalau wamepata ofisi miaka michache iliyopita. Lakini kabla ya hapo
mambo yaliendeshwa mfukoni au kwenye briefcase.
Kocha hana uwanja, hana vifaa na hana ofisi, makazi yake ni ya
kubangaiza au ya kiwango duni lakini bado uongozi unachotaka ni ubingwa.
Akishindwa, lawama zote na mwisho anatimuliwa, tena malipo yanakuwa shida.
Aliyekuwa Kocha Mkuu wa Manchester United, Alex Ferguson alikuwa akitumia
muda wake kwa zaidi ya saa tano kila siku akiwa katika ofisi yake akipanga
namna ya kufanya mikakati ya uendeshaji wa timu. Bado anakuwa na saa nyingine
tatu hadi nne za mazoezi, mara mbili kwa siku.
Maana yake, Ferguson alikuwa akifanya kazi takribani saa 10 kwa siku
kwa ajili ya Manchester United. Lazima atafanikiwa kwa kuwa anaipa nafasi kubwa
zaidi kazi yake.
Kuna kiongozi yeyote wa Simba amewahi kufanya utafiti kwa nini makocha
wawe na ofisini? Au nini umuhimu wake? Kazi ya soka inahitaji utulivu na
utunzaji kumbukumbu kwa mpangilio.
Inawezekana akawa na mambo mengi sana ya kupanga kuliko Hans van Der
Pluijm na Zdravko Logarusic wa Simba, lakini siku ya mwisho anachotaka ni
mafanikio na hasa vikombe kama wanavyotaka makocha wa Yanga na Simba.
Kuiga maendeleo si vibaya, iko haja sasa timu za hapa nchini
zikamuangalia kocha kama mwajiriwa anayeweza kufanya kazi zake klabuni na
kupanga mambo mengi. Kuanzia watoto, vijana na timu kubwa.
Lakini si kocha kufanya kazi kipindi cha mazoezi pekee, haitoshi.
Memba wa benchi la ufundi wanakutana wakati wa mazoezi pekee. Tofauti na Arsene
Wenger anavyofanya na wenzake wa Arsenal au Manuel Pellegrini na wafanyakazi
wenzake wa Manchester City.
Klabu za hapa nchini zinaweza kujifunza na zinaweza kubadilika, lakini
hazipaswi kuwa na viongozi wanaozifanya ni ziada, njia ya kupita wapate majina
au kujulikana zaidi au njia ya kulahisisha mambo ili wawanie ubunge kwenye
majimbo yao!
Kujifunza ni sehemu ya hatua za maendeleo, ukikubali sehemu uliyokosea
utaweza kupiga hatua. Makocha kuwa na ofisi ni sehemu ya mabadiliko na hatua za
maendeleo.
Lakini bado ni muhimu kuwa klabu zetu ziwe na viwanja vya mazoezi, la
sivyo ni sawa na kuwa na mtaji wa kuuza duka lakini hauna sehemu maalum ya
kuuzia. “umachinga wa soka.”
0 COMMENTS:
Post a Comment