Na Saleh
Ally
HATIMAYE
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage, ametangaza rasmi kwamba hatagombea
nafasi hiyo mara baada ya muda wake kwisha, haya si maneno yangu, amesema mbele
ya wanachama wakati wa mkutano wa marekebisho ya katiba.
Huenda hili
likawa wazo zuri na msaada mkubwa kwa Simba lakini kutakuwa na mambo mengi ya
kujifunza kwa wanachama na njia walizopita hadi kufikia hapa walipo na uongozi
wao utamaliza muda ukiwa umewaacha wapi katika kipindi hiki cha miezi miwili.
Nilisikia
walitaka kumchapa Rage kwa kuwatolea maneno ya shombo lakini askari polisi
waliokuwa eneo la mkutano wakamuokoa. Nimpe pole Rage, lakini bado nasisitiza,
kiburi si maungwana. Bora kujali utu kuliko vitu.
Yote hayo
ninaweza nikawa ninapita katika kupitia yale yaliyotokea katika mkutano huo wa
marekebisho ya katiba uliofanyika Jumapili iliyopita kwenye Ukumbi wa Bwalo la
Maofisa wa Polisi jijini Dar es Salaam. Lakini ninacholenga hasa ni kuhusu
fedha za mshambuliaji Emmanuel Okwi.
Kawaida nimekuwa
nikipata rundo la maoni kutoka kwa mashabiki wa soka kuhusiana na namna ambavyo
Simba inaweza kupata malipo yake ili kuepuka hasara kubwa ya kumuuza Okwi bure
kwa Etoile du Sahel.
Najua
kabisa kwamba kila nikiligusa suala la Okwi, Rage amekuwa mkali sana na ndiyo
kipindi pekee ambacho amekuwa akisema ninamsakama au kutoa vitisho vyake.
Lakini kwa kuwa najua yote anayoyasema si sahihi na ninachohoji ni kingine,
basi naendelea kuuliza na kuchambua tu.
Katika
kauli alizowahi kuzitoa Rage, alisisitiza Etoile wangewalipa dola 300,000 (Sh
milioni 480) hata kabla yeye hajaondoka madarakani, lakini juzi ametangaza kwa
mara ya pili kuwa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) limewahakikishia kuwa
watalipwa fedha zao, hata kama yeye Rage hatakuwa madarakani.
Miezi
miwili kabla, Rage alisema amepokea barua kutoka Fifa ikionyesha namna Etoile
walivyoomba kusogezewa muda wa kulipa fedha hizo za Okwi. Hofu yangu iko hapo,
kwamba pamoja na kauli hizo za Rage, hakuna hata mwanachama mmoja aliyehoji
zilipo barua hizo.
Ilikuwa
vizuri kuwaonyesha wanachama barua hizo ili kupata uthibitisho wa anachokisema,
lakini Rage hakufanya hicho, kitu ambacho kinanipa hofu kwamba huenda mambo
yako ndivyo sivyo, lakini anajaribu kuwapoza wanachama hao kwa mgongo wa chupa.
Kama
alivyosema Rage kwamba hana njaa, kweli hilo linawezekana kabisa. Lakini kwenye
suala la fedha hakuna anayeridhika, ndiyo maana hadi leo bilionea Mtanzania,
Bakhresa anaendelea kufanya biashara. Hiyo maana yake anasaka noti, sasa
itakuwa kwa Rage?
Kauli mbili
alizowahi kuzisema Rage ambazo zinathibitisha kwamba hata alichokisema
kuhusiana na hizo barua kinaweza kisiwe kweli ni hizi; moja, fedha zitalipwa
kabla ya mwaka jana kwisha, pili, kamwe Okwi hatacheza Yanga.
Hadi mwaka
umeisha, hakukuwa na fedha zilizolipwa hata senti, ndiyo maana nimekuwa
nikisisitiza hili kuwa Okwi aliuzwa bure kwa Etoile du Sahel. Pili hilo la
kusema kamwe hatacheza Yanga, sasa Okwi anacheza tena michuano ya nyumbani na
kimataifa!
Tangu Okwi
aanze kucheza tena kwa ufafanuzi wa Fifa, Rage hakuwahi kuzungumza lolote na
ajabu hakuna wanachama wa Simba waliohoji. Kama ambavyo nimekuwa nikisisitiza,
Simba hawana sababu ya kuzungumzia suala la Okwi kucheza Yanga au la, badala
yake waulizie fedha zao. Lakini mwenyekiti wao aliendelea kupambana na hilo.
Baadaye
ilionekana kweli hakuwa sahihi, badala yake alitakiwa kuelekeza nguvu kwenye
malipo ya Sh milioni 480. Sasa hilo limefanyika, lakini hadi leo hakuna lolote
na hadithi ndiyo zinaonekana kuzidi kukolea, kama ingekuwa ni filamu, basi
labda wakati huu ndiyo jambazi limekutana uso kwa uso na stelingi, tena kwa
mara ya kwanza.
Filamu ya
Okwi inakwenda ukingoni, lakini hadi leo Simba haijalipwa na matumaini ya
kulipwa yako chini sana. Kuna kila sababu ya kusema hivyo kwa kuwa sababu za
msingi ziko lukuki, nitakupa chache.
Etoile
inayotakiwa kulipa fedha hizo kibao, haina faida yoyote na Okwi na Fifa
hiyohiyo ndiyo ilimuidhinisha kwenda SC Villa na baadaye ikakubali acheze Yanga
kwa mujibu wa TFF. Sasa jiulize, itakuwa vipi kulipa kitu ambacho hakina faida
kwao?
Dola
300,000 si fedha kidogo. Timu kama Etoile inaweza vipi kufanya mchezo wa
kijinga kama huo? Usisahau Waarabu hao wana uzoefu mkubwa katika masuala ya
kuuza na kununua wachezaji, hivyo wanajua wafanye nini.
Lakini
jiulize, kama Rage akiwa madarakani, alishindwa kurekebisha kosa lake la
kumuuza bure Okwi, je, akiwa nje ya uongozi, ataweza vipi kuifanya kazi hiyo
kwa ufasaha ili Simba ilipwe? Au siku ya mwisho atawahoji viongozi walio
madarakani kushindwa kulishughulikia suala hilo ili waweze kulipwa!
0 COMMENTS:
Post a Comment