March 19, 2014


Na Saleh Ally
MWANZONI mwa miaka ya 1990, winga machachari wa timu ya Mkoa wa Shinyanga, Mwinyimvua Komba alicharuka na kuzichapa kavukavu na beki wa Mwanza Heroes, George Masatu hali iliyosababisha mchezo wa Kombe la Taifa kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga kusimama kwa zaidi ya dakika kumi.

Komba maarufu kama Masolwa na Masatu, walizichapa baada ya kila mmoja kumshutumu mwenzake alimshika makalio. Lakini mwamuzi alisisitiza kuwa hakuwa ameona lolote kuhusiana na madai yao.

Kila mmoja alishitaki kwa wakati wake, lakini mwamuzi hakuweza kuchukua hatua kwa kuwa hajaona kilichotokea. Hasira zao zisingemalizika, kwa kuwa kila mmoja alitaka kumuonyesha mwenzake kazi.
Achana na wachezaji hao wawili ambao wote sasa ni baba au wazazi, twende Ulaya. Mshambuliaji mahiri wa Liverpool, Luis Suarez ni baba wa watoto wawili wa kike ambao amezaa na mkewe, Sofia Balbi ambaye alikuwa mpenzi wake tangu wakiwa shule hadi alipofunga naye ndoa mwaka 2009.
Hali kadhalika, mshambuliaji mkali wa Bayern Munich, Arjen Robben, ni baba wa watoto watatu, kati yao wawili ni wa kiume na binti mmoja.
Inawezekana tabia zao wanapokuwa katika familia zao zinaweza kutofautiana sana, lakini wanaporudi uwanjani hata kama kuna tofauti kiuchezaji, wawili hao hawawezi kupishana sana na akina Masatu na Masolwa katika tabia za kitoto.
Kawaida watoto hutegemea kushitaki karibu kila kitu kwa wazazi wao, mfano ikitokea wamepigwa na wenzao, basi lazima mashitaka yatakwenda kwa wazazi.
Hali hiyo ndiyo imejitokeza zaidi kwa wachezaji hasa wa soka ambao wanaonekana kuwa na tabia zinazofanana na mwamuzi anapokuwa uwanjani anaonekana ni sawa na mzazi kwa kuwa kila mchezaji hutaka kushitaki, akiwa kasukumwa, kapigwa kibao, katemewa mate na vinginevyo.
Lakini kali zaidi ni madeko, hadi sasa Suarez ndiye mchezaji anayeongoza zaidi kwa tabia hiyo ya kudanganya kuwa amefanyiwa madhambi kumbe la.
Katika msimu wa 2012-13 wa Ligi Kuu England, Suarez alipewa cheo cha kuwa na tabia za kitoto zaidi baada ya kujiangusha mara 26 bila ya kufanyiwa madhambi na akafanikiwa kuwalaghai waamuzi mara 12 wakatoa adhabu zikiwemo penalti.
Robben pia aliweka rekodi ya kuwalaghai waamuzi kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita baada ya kujiangusha mara 14 na waamuzi wakaingia mkenge mara 6 na kutoa adhabu.
Mchezaji mwingine aliyeingia kwenye chati ya kuwa na tabia za kitoto ni Ashley Young wa Manchester United pamoja na Didier Drogba aliyekuwa Chelsea na sasa yuko Galatasaray ya Uturuki.
Hata hivyo, katika moja ya uchambuzi wake, nahodha wa zamani wa Manchester United, Roy Keane amewahi kusema kuwa alikuwa akikerwa na tabia za washambuliaji ambao wanaongoza kwa kudeka kwa waamuzi.
Akasema kama ni tabia za kiume, basi mabeki na viungo wakabaji wana tabia za kiume kweli kwa kuwa ndiyo wanakuwa ngangari na hata mara moja huwezi kuona wakijiangusha kama ambavyo wamekuwa wakifanya washambuliaji.
Halafu Keane aliyekuwa akijulikana kwa ukorofi akasisitiza: “Soka ni mchezo wa wanaume wa shoka, lakini inashangaza kuona watu wenye tabia za kitoto ndiyo wanaonunuliwa kwa bei kubwa, kawaida huwa sikubaliani na hilo.”
Lakini kiungo na kocha wa zamani wa Chelsea, Roberto Di Mateo naye aliungana na Keane, lakini akasema kati ya burudani za aina yake ni washambuliaji na tabia zao za kitoto.
Di Mateo alisisitiza burudani ya washambuliaji na ufungaji mabao, lakini ulaghai au utoto wao umekuwa burudani na mijadala mikubwa katika mchezo wa soka, hivyo anaona wanachokifanya ni kuongeza burudani zaidi.
Tabia za namna hiyo za wachezaji kupenda kujiangusha zimekuwa zikitokea duniani kote na kwa upande wa mabeki na viungo wakabaji, tabia hiyo imekuwa moja ya kero kubwa sana kwao.
Wakati fulani, mchezaji kikapu maarufu wa Marekani, Shaq O’neil aliwahi kusema wanasoka ndiyo wanamichezo wanaodeka zaidi kuliko binadamu yeyote anayeishi duniani.
O’neil  alisisitiza kuwa kwenye kikapu hakuna muda wa kudeka, lakini akawaponda wanasoka akisema hivi: “Wanadeka wakiwa nyumbani kwa wake au wapenzi wao, lakini wanafanya hivyo wakiwa uwanjani kwa waamuzi. Unaweza kusema hawana tofauti na watoto wanaodeka kwa wazazi wao, yaani baba na mama.”
Robben, Suarez, Drogba, Young wanaweza kuwa sehemu ndogo sana ya wachezaji wanaoweza kudhihirisha tabia hiyo ya kitoto. Ukitulia na kufuatilia vizuri katika mechi mbalimbali za nchini, Ligi Kuu Bara, England, Hispania, Italia na kwingineko duniani, utawagundua wengi zaidi.





0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic