Mshambuliaji nyota wa Simba, Amissi Tambwe huenda
akavunja mkataba wake na klabu hiyo na kuondoka zake mara baada ya kumalizika
kwa msimu huu, ikiwa timu hiyo haitapata nafasi ya kuwakilisha taifa kwenye
mashindano ya kimataifa.
Tambwe ambaye ndiye kinara wa mabao katika Ligi Kuu
Bara akiwa na mabao 19, amesema kuwa matarajio yake wakati anajiunga na klabu
hiyo yalikuwa ni kuiona ikishiriki mashindano ya kimataifa, hivyo kukosa
kushiriki michuano hiyo kutamtibulia mipango yake na ametamka wazi anafikiria
kuondoka klabuni hapo.
Simba ipo katika nafasi ya nne na haina matumaini ya
kushika nafasi ya kwanza wala ya pili kwa kuwa imesaliwa na michezo minne,
ambapo imezidiwa pointi 10 na Yanga inayoshika nafasi ya pili.
Tambwe, raia wa Burundi amesema hatma yake ya
kuendelea kubakia Simba itajulikana baada ya kumalizika kwa ligi ya msimu huu
ambayo ipo katika hatua za lala salama.
Alisema anaweza kuondoka au asiondoke Simba lakini alisisitiza
kuwa kila kitu kitajulikana baada ya Aprili 19 ambapo ligi itakuwa inafikia
tamati.
“Wakati najiunga Simba, matarajio yangu yalikuwa ni
kushiriki mashindano ya kimataifa, lakini ndoto hizo zinaonekana kugonga mwamba
kutokana kwa kuwa hivi sasa timu yetu ipo kwenye nafasi mbaya ambayo haitupi
kabisa matumaini ya kumaliza ligi tukiwa kwenye nafasi mbili za juu ambazo kwa
sasa zinashikiliwa na Azam na Yanga.
“Kusema kweli hali hiyo inasikitisha na inaniumiza
sana kwani natamani kushiriki mashindano ya kimataifa kama walivyo wachezaji
wote wanaotaka mafanikio katika mchezo wa soka.
“Hata hivyo kwa sasa siwezi kuzungumza lolote kama
nitaendelea kubakia Simba au la ila hilo litajulikana baadaye baada ya
kumalizika kwa ligi kuu, lakini nafikiri juu ya hilo,” alisema Tambwe.
Simba ina pointi 36 nyuma ya Mbeya City yenye pointi
42, Yanga yenye ponti 46 na Azam inayoongoza msimamo ikiwa na pointi 50.
Wakati huohuo, Tambwe amesema kama atapata nafasi ya
kucheza kwenye mechi dhidi ya Azam katika ligi kuu keshokutwa kwenye Uwanja wa
Taifa, atapambana ili kuhakikisha Azam inafungika.
“Azam ni timu tu kama timu nyingine, naiheshimu
kutokana na ubora wake, tutahakikisha tunaivunja rekodi yao ya kutofungwa msimu
huu,” alisema Tambwe.
0 COMMENTS:
Post a Comment