Na Saleh Ally
SIKU chache zimepita tangu makala iliyokuwa
ikieleza namna ambavyo wachezaji wa Yanga imefikia nao wawajibike au kujifanyia
tathmini kuhusiana na suala la kutokuwa makini, itoke.
Maelezo ya makala yale yalifafanua namna ambavyo
Yanga imekuwa na uwezo mkubwa wa kutengeneza nafasi, lakini ikishindwa
kuzimalizia, hivyo kubakia na maneno mengi kuwa ilibaki kidogo tu.
Halafu baada ya hapo, mzigo wamekuwa
wakiangushiwa walimu kwamba hawana uwezo lakini wakati mwingine wanakuwa si wao
tu, badala yake tatizo ni la wachezaji ingawa ni vigumu sana kuonekana kwa
upande huo wa pili.
Ukifanya tathmini, utagundua Yanga ndiyo kikosi
kilichotengeneza nafasi nyingi sana za kufunga katika Ligi Kuu Bara, lakini
ndiyo walioshindwa kuzitumia nafasi hizo isipokuwa katika mechi chache.
Lakini timu kama Azam FC, imejitahidi kutumia
nafasi nyingi sana ilizozipata na wachezaji wake hasa Kipre Tchetche amekuwa
kama msumari kila anapopata nafasi hizo.
Anayeonekana ni bora zaidi katika utumiaji
nafasi hizo bila ya kujali ni mchezaji wa kigeni au mzalendo ni Amissi Tambwe
wa Simba ambaye amekuwa makini zaidi anapofika langoni, unaweza kusema si mtu
wa mchezo.
Lakini Hamisi Kiiza na Didier Kavumbagu wa
Yanga, wamekuwa na tatizo kubwa la utumiaji nafasi. Huenda ni papara au woga
kuwa mashabiki watasema imekuwa ni hali inayowatoa mchezoni, ndiyo makala hayo
yalisisitiza ni lazima wawe makini au walimu wachukue uamuzi mgumu.
Yanga ilionyesha ugonjwa huo kwa kiasi kikubwa
katika mechi yake ya kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ya
Misri. Baada ya hapo ikafanya hivyohivyo katika mechi ya pili jijini Alexandria
na mwishoni ikang’olewa kwa penalti katika mechi iliyoonekana kuwa ‘yao’
kabisa.
Iliporejea nyumbani kwenye Ligi Kuu Bara,
ilicheza mechi mbili ikianza na Mtibwa Sugar halafu Azam FC na ikapoteza nafasi
nyingi kabla ya kujilaumu kwa kuambulia sare hizo mbili.
Kocha Hans van Der Pluijm aliendelea kuwatumia
Kiiza na Kavumbagu bila ya kuwapa nafasi Jerry Tegete na Hussein Javu ambao
alikuwa akiwaingiza muda ukiwa umeyoyoma sana.
Lakini mambo yamebadilika wakiwa Tabora wakati
Yanga ikiivaa Rhino, amewapa nafasi na wote wamempa majibu kwamba wanazihitaji
nafasi hizo, ndiyo maana kila mmoja akafunga bao moja.
Tegete alifunga bao la kwanza na kusababisha la
pili baada ya shuti lake kuwababatiza mabeki. Javu alifunga la pili na kuongeza
idadi ya mabao kwa Yanga ambayo ilishinda kwa mabao 3-0.
Kumbe Tegete na Javu bado wazima! Wanaweza
kufunga na wameonyesha kwa vitendo na huenda walichokifanya kitakuwa changamoto
kwa wageni pamoja na benchi zima la ufundi la Yanga kwamba kuna sababu ya kutoa
nafasi kwa wengine.
Kusiwe na woga wa kuwapa nafasi wazalendo au
isiwe staili kwamba ni lazima wageni ndiyo waanze katika kikosi cha kwanza.
Kama kweli mtu anafanya vizuri bila ya kujali ni mzalendo au mgeni basi apewe
nafasi.
Lengo si kuwabana Kiiza na Kavumbagu, lakini
hali halisi inaonyesha kila kinachoelezwa. Basi hakuna haja ya kuwa na woga,
kwani kama wanafanya vizuri hakuna haja ya kuwabania.
Kikubwa mwendo wa upangaji vikosi uangalie ubora
wa kazi uwanjani na si huyu ni mchezaji mgeni ndiye anakuwa na nafasi kubwa ya
kucheza hata kama haonyeshi kiwango cha juu. Kwa mshambuliaji, ubora wake kuwa
juu ni kufunga tu, hilo halina mjadala.
Hii si kwa Yanga pekee, hata timu nyingine
kwamba kama mgeni anaboronga basi abaki benchi ikiwa kama ni sehemu ya
changamoto kwake na ikiwezekana ajiulize kwamba imekuwaje.
Hakuna sababu ya kuwaacha wanaoweza kufunga kwa
hofu kuwa ni wazalendo, lakini si sahihi kuwaacha wachezaji bila ya kuwa na
changamoto ya vitendo kama waliyoionyesha Tegete na Javu.
Wameonyesha wanaweza, basi wapewe nafasi tena na
ikiwezekana Kiiza na Kavumbagu wakiwa benchi, basi waone kuwa kutozitumia
nafasi ni kujiongezea ugumu wa kupata nafasi ya kucheza katika kikosi cha
kwanza na si kuwa na uhakika hata kama watavurunda.
Makocha wengi wenye timu zinazojumuisha wageni
wamekuwa wagumu kuwaweka nje, hivyo hilo la Tegete na Javu, basi liwe kwa
mabenchi yote ya ufundi yaliyolala yakajisahau sababu ya ugeni, lakini iwe
changamoto pia kwa wanaoshindwa kufanya vizuri kwamba wakikosea, kuna wengine
walio benchi wanaweza.
Kama ni uzalendo, Tanzania inahitaji
washambuliaji bora, pia ni vizuri kuona vijana wa nyumbani wanacheza na hasa
kama wana uwezo sawa na ule wa wageni, basi kipaumbele kiwe kwao. Wapeni nafasi
vijana bana!
0 COMMENTS:
Post a Comment